HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 21 September 2017

TAMASHA LA SANAA BAGAMOYO KUANZA SEPTEMBA 23

 Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii 

Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imeandaa tamasha la kimataifa la 36 la Sanaa na Utamaduni litakalofanyika Septemba 23 hadi 30 katika viwanja vya TaSUBa mjini Bagamoyo mkoani pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Herbert Makoye amesema Tamasha la Kimataifa la 36 kwa mwaka huu litakuwa la kipekee kutokana na kupiga vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo dunia inapambana nayo.

Dk. Makoye amesema kaulimbiu ya ya Tamasha hilo ni “Sanaa na Utamaduni katika Kupiga Vita Madawa ya Kulevya” ikiwa ni mahsusi katika kuunga mkono mapambano ya vita dhidi ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
Tamasha la Kimataifa Sanaa na Utamaduni Bagamoyo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ikiwa na malengo ya Kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Mtanzania, Kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa Tasuba wanalitumia kupima kiwango chao cha umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.

Amesema malengo mengine ya tamasha Kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni, Kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa na pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya sanaa.

Aidha amesema tamasha la mwaka huu linafanyika kwa mara ya 36 na litapambwa na ngoma za asili, muziki, sarakasi na maigizo pamoja na maonyesho ya sanaa za ufundi. Pia kutakuwa na warsha na semina zitakazohusu mambo mbalimbali ya kijamii. Jumla ya vikundi vya Sanaa 68 vimethibitisha kushiriki na kati ya hivyo vikundi Saba ni kutoka nje ya nchi (Kenya, Ufaransa, Korea Kusini, Uingereza, Zimbabwe na Mayyote).

Mgeni rasmi wa ufunguzi wa tamasha hilo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Dk Harrison Mwakyembe (Mb), wakati Ufungaji wa Tamasha utafanyika na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.
Kampuni ya Michuzi Media Group ni moja ya wadhamini wa kufanikisha tamasha hilo la Kimataifa la 36
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dk. Herbert Makoye (katikati) akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza tamasha la kimataifa la 36 taasisi hiyo litakalofanyika mjini Bagamoyo , kushoto ni Mwenyekiti wa Tamasha, John Mponda , wa pili kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Rodney Thadeus kulia ni Afisa habari wa TaSUBa, Sophia Mtakasimba

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad