HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 18, 2017

PROF. MBARAWA MAWASILIANO YA SIMU YAPATIKANE WAKATI WOTE

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akikagua jenereta linalowezesha mnara wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), katika eneo la eneo la Gairo Hill,wilayani Gairo, Mkoani Morogoro. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bibi. Siriel Mchembe.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bibi. Siriel Mchembe, kabla ya kuzungumza na wananchi wa kata ya Leshata, wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akimsikiliza Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi Peter Ulanga (kulia) alipokagua minara ya simu wilayani Gairo, Mkoani Morogoro. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akitoa maelekezo kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania mara baada ya kufungua mnara wao katika kijiji cha Chakwale wilayani Gairo, Mkoani Morogoro. 


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameyataka makampuni ya simu nchini kuhakikisha mawasiliano ya simu yanapatikana wakati wote katika ubora unaotakiwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma inayowiana na thamani ya fedha wanayolipa.
Akikagua na kuzindua minara ya simu ya kampuni za TTCL, VODACOM, HALOTEL, na TIGO katika Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni za simu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF ili katika kipindi cha miaka mitatu ijayo sehemu zote za Tanzania ziwe zimefikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika.
"Tumieni mawasiliano ya simu kufanya biashara, kuboresha huduma za jamii kama elimu na habari ili kukuza ustawi wa maisha yenu", amesema Profesa Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amewaonya wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya simu kwani ipo sheria kali inayodhibiti matumizi mabaya ya simu.
Amezungumzia umuhimu wa kampuni za simu kujenga minara katika maeneo mapya na kukarabati minara ya zamani ili kuwezesha mawasiliano kuwa katika ubora maeneo yote ya nchi.
Amewataka wakazi wa vijiji vya Letugunya, Leshata na Chakwale kutumia fursa ya upatikanaji wa mawasiliano kuongeza uzalishaji wa mazao na kuyauza kwa bei nzuri na hivyo kukuza uchumi wao.
Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Mhandisi Peter Ulanga amemhakikishia Waziri Profesa Mbarawa kuwa  mfuko huo umejipanga kukamilisha miradi yote kwa wakati na kufanya uhakiki wa takwimu za mawasiliano nchi nzima ili kubaini maeneo ambayo yana changamoto kubwa ya mawasiliano na kuyatatua.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Siriel Mchembe  amemshukuru Waziri Mbarawa kwa kuboresha huduma za mawasiliano katika Wilaya hiyo na kumhakikishia wananchi watailinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad