HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 13 September 2017

MKURUGENZI WA MAENDELEO YA JAMII AWAONGOZA WANANCHI WA KIJIJI CHA MONDO KUSHIRIKI KATIKA UJENZI WA KITUO CHA AFYA CHA KATA YA MONDO, MISUNGWI.

Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW
Sera ya Maendeleo ya Jamii pamoja na mambo mengine, inaelekeza jamii kushiriki kazi za kujiletea maaendeleo yao wenyewe maana jamii ndiyo kitovu cha maendeleo.

Kwa kutambua hilo, Mkurugenzi wa Maendelo ya Jamii Bw. Patrich Golwike ametembelea katika Kijiji cha Mondo, Kata ya Mondo, kilichopo katika Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kuhamsha ari ya wananchi kushiriki katika ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya cha kijiji chao.Bw. Golwike alibainisha kuwa maendeleo ya mtu ni mtu mwenyewe na hakuna mtu kutoka nje ya eneo fulani ataleta maendeleo katika eneo husika.

“Sisi hatukuja hapa kijijini Mondo kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya Mondo, bali tumekuja kuhamsha ari ya wananchi wa kijiji hiki kuwa tayari kushiriki kazi za maendeleo yao kwa kutumia rasilimali zilizopo” alisema Bw. Golwike.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Mondo Bi. Aziza Omary alibainisha kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mondo uliibuliwa kwenye kikao cha Maendeleo ya Kata (WDC) ya Mondo, ndipo iliporidhiwa kujenga kituo hicho ili kupunguza tatizo la vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, na pia kuondokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya za rufaa zikiwemo za wazazi na wagonjwa wengine.

Awali wananchi walishiriki kubaini changamoto, kupanga, kutekeleza na kusimamia mradi wa ujenzi kuhakikisha kuwa wananchi wanajitolea kuchangia nguvu kazi zao katika zoezi la ujenzi. 

Kazi nyingine zinazofanywa na wananchi ni kukusanya vifaa vya ujenzi kama vile mawe, kokoto, mchanga, mafundi, na utoaji uchangiaji wa rasilimali fedha.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mondo Bw. Philipo Suleiman ameipongeza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuchagua kutembelea kijiji cha Monde mio ngoni mwa vijiji takribani 900 vilivyopo katika mkoa wa Mwanza.

Jengo la Kituo cha Afya cha Kata ya Mondo linakadiriwa kukamilika mwaka 2018 na litagharimu takribani shilingi 150,460,540/- fedha ambayo itatoka kwa wahisani na wananchi wenyewe.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akishiriki ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya katika Kijiji cha Mondo, kilichopo kata ya Mondo, Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza, mapema.
Mratibu wa Masuala ya Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI Bibi Mwajina Lipinga(kulia) aliyeshika chepeo) akishirikiana na wananchi kujenga jengo la Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mondo Wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza kutatua kero ya ukosefu wa huduma za afya katika kata ya Mondo kwa kutumia nguvu za wananchi wenyewe. 
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Bw. Atupele Mwambene(kushoto walioshika chepeo) akichanganya saruji kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mondo, Kata ya Mondo kilichoko Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza katika kuhamsha ari ya kushiriki kazi za maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika mazingira husika.
Mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Ufundi, Misungwi Mhandisi Harold J. Mtyana akishiriki kujenga jengo la Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mondo, kata ya Mondo, wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akikabidhi mifuko 50 ya simenti kwa niaba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mondo Bw. Marthias Lumwagila kwa ajili ya kusaidia kuendeleza ujenzi wa Kituo hicho cha Afya. 
Sehemu ya jengo la kituo cha Afya cha Mondo, Kata ya Mondo,Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kama linavyoonekana na wananchi wakiendelea na kazi ya ujenzi. Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WAMJW.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad