HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 5 September 2017

HALOTEL, FINCA WAZINDUA BENKI MKONONI, Wateja sasa kuweka akiba na kupata faida kupitia simu zao

 Mgeni rasmi katika uzinduzi wa huduma mpya ya HaloYako ya Kampuni ya Simu ya Halopesa kwa kushurikiania na Finca Microfinance Bank, Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, John Rubuga akiwa pamoja na Mkurugeni Mkuu wa Kampuni ya Simu ya Halotel Tanzania, Le Van Dai pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Finca Microfinance Bank, Issa Ngwegwe  wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam Septemba 5, 2017.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, Mgeni rasmi ambaye alimuwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, John Rubuga amesema kuwa serikali imeendelea kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili kurahisisha huduma na kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania hususan katika maendeleo ya kiuchumi.

 “Serikali iko tayari kushirikiana na kampuni mbalimbali zenye malengo ya kuondoa umaskini kwa watanzania kwa kukuza kipato chao ili kuboresha maisha. Tunaamini pia kupitia huduma hii ya Haloyako Watanzania wengi zaidi ambao hawatumii huduma za benki wanaweza kutumia ili kuweza kufanikisha malengo yao ya kifedha,” alisema na kuongeza kuwa “Halotel na FINCA wana malengo sawa, ambayo wanalenga kuwasaidia watanzania wenye hali ya chini na wakati ambao wengi wao wako maeneo ya vijijini, ni Imani yetu kuwa ushirikiano huu utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya Watanzania na tutajenga utamaduni wa kujiwekea akiba”.
Aidha, amezitaka kampuni hizo kuhakikisha zinatoa elimu ya kutosha ili Watanzania waweze kuelewa umuhimu wa huduma hiyo na kuweza kuitumia vyema huku akitoa wito kwa jamii ya Watanzania kuepuka kuhifadhi hela ndani na kujenga utamaduni ya kujiwekea akiba.

Kwa upande wa Halotel, Mkurugenzi Mtendaji wake, Le Van Dai alisema “Tunashukuru sana kwa uhusiano huu ambao tumeujenga kati yetu na FINCA ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakitoa huduma za kifedha kwa jamii ya Watanzania, Kwa uapnde wetu sisi hii ni hatua kubwa sana katika kuhakikisha tunatatua changamoto ya huduma za kifedha kwa Watanzania, Tumejitahidi kwa kiasi kikubwa kuhakikisha hatuishii kuwa tu kampuni ya Mawasiliano ila tunataka kuwa kampuni inayoishi maisha ya Watanzania”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Finca, Issa Ngwegwe Aliongeza kuwa lengo kubwa ya FINCA ni kutoa suluhisho la kutokomeza umaskini kwa kusaidia watu kujenga mitaji, kutengeneza ajira na kuboresha maisha.

“Haloyako sio tu huduma ya kifedha kupitia simu ya mkononi bali ni akaunti ya akiba ya malengo ambayo itakuwa jibu kwa Watanzania ambao wanataka huduma za kifedha ili kuweza kuweka akiba kutimiza mahitaji yao ya kifedha kama vile kulipa karo, kodi ya nyumba, kuwekeza, kulipia huduma za afya na pia kusafiri, Kupitia Haloyako mteja anaweza kuweka mipango na kuanza kuweka akiba ili kutimiza lengo lake na hivyo kuepuka madeni au kushindwa kukidhi mahitaji ya kifedha ya familia.  Alihitimisha Ngwegwe.

Huduma ya HALOYAKO inapatikana kupitia huduma ya HALOPESA inayotolewa na kampuni ya mawasiliano ya Halotel ambayo ni huduma ya kifedha inayomwezesha mteja kutuma na kupokea fedha kwa urahisi na kwa usalama.
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa huduma mpya ya HaloYako ya Kampuni ya Simu ya Halopesa kwa kushurikiania na Finca Microfinance Bank, Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, John Rubuga (katikati) akiwa pamoja na Mkurugeni Mkuu wa Kampuni ya Simu ya Halotel Tanzania, Le Van Dai (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Finca Microfinance Bank, Issa Ngwegwe wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam Septemba 5, 2017.
Picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi
Picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Kampuni ya ya Halotel na Finca Microfinance Bank.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad