HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 19 August 2017

Zuio Bodi ya CUF Lipumba lazingirwa na mapingamizi mahakamani

Maombi ya mbunge wa Malindi Zanzibar (CUF), Ally Saleh ya amri ya zuio dhidi ya wajumbe wapya wa bodi ya chama hicho, yamekumbana na mapingamizi matatu.
Mbunge huyo amefungua maombi hayo Mahakama Kuu, ikiwa ni sehemu ya kesi ya msingi aliyoifungua mahakamani hapo kupinga uhalali wa wajumbe wa bodi hiyo wanaotoka kambi ya mwenyekiti aliye kwenye mgogoro na CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.
Saleh anaiomba mahakama itoe amri ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa wote katika kesi hiyo, wakala wao wote wanaofanya kazi kwa maagizo yao, kutokujihusisha kwa namna yoyote na masuala ya chama hicho.
Hata hivyo, maombi hayo yamewekewa mapingamizi matatu yenye jumla ya hoja nne zikitaka mahakama iyatupilie mbali kutokana na kasoro za kisheria.
Pingamizi la kwanza limewekwa na Ofisa Mtendaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita), aliyewakilishwa na jopo la mawakili wanne wa Serikali likiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata.
Katika pingamizi hilo amewasilisha hoja mbili, akidai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa waombaji wamemshtaki mtu ambaye si sahihi na kwamba yamefunguliwa chini ya vifungu vya kanuni visivyo sahihi.
Pingamizi la pili limewekwa na bodi mpya ya wadhamini ya chama hicho na mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo, kupitia kwa wakili wao Majura Magafu.
Katika pingamizi lao, wawili hao wanadai kuwa hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo ina dosari za kisheria kwa kuwa imejumuisha hoja za kisheria, hitimisho na uvumi badala ya hoja za kiushahidi na kwamba hajataja chanzo cha taarifa zake .
Pingamizi la tatu limewasilishwa na wajumbe wa bodi hiyo ambao wanapingwa katika shauri hilo na wanawakilishwa na wakili Mashaka Ngole.
Akijibu hoja hizo, Mpale Mpoki, ambaye ni wakili wa Saleh katika shauri hilo, alidai kuwa mapingamizi hayo hayana mashiko kwa kuwa kisheria mjibu maombi wa kwanza ana haki ya kushtaki na kushtakiwa na kwamba vifungu hivyo walivyotumia ni sahihi.
Pia Wakili Mpoki alidai kuwa kiapo cha mwombaji hakina hoja za kisheria, hitimisho, maoni wala uvumi kama mawakili wa wajibu maombi walivyodai.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad