HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 22 August 2017

TCAA KUNUNUA RADA NNE ZA KISASA

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imeingia makubaliano  ya manunuzi ya rada Nne na kampuni ya Thales ya nchini Ufaransa  zenye thamani ya sh.bilioni 61.3.

Akizungumza leo na waandishi wa habari kabla ya kusaini makubaliano ya manunuzi ya rada hizo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Profesa  Makame Mnyaa Mbarawa amesema kuwa kampuni hiyo ifunge kwa viwango vilivyoainishwa katika mkataba na watakaosimamia mradi huo wanatakiwa kuwa na uadilifu kutokana fedha hiyo ni nyingi kutolewa na serikali.

Amesema kuwa kufungwa kwa rada hizo kutasaidia serikali kupata mapato ya sh. bilioni moja, kuongeza idadi ya ndege kutumia anga ya Tanzania pamoja na kuongeza idadi ya wataalii kutokana na anga kuwa salama.

Profesa Mbarawa amesema kuwa TCAA imetumia fedha zake pamoja na serikali kuepukana na mkopo ambapo wameweza kuokoa  sh. bilioni 10 ambazo zingetokana ulipaji mkopo katika taasisi ya fedha.

Amesema kuwa TCAA wameweza kujibana hadi kufikia ununuzi wa rada hizo na kutaka taasisi zilizo chini ya wizara kutumia vyanzo mapato vyao katika miradi mbalimbali kuliko kuangalia kukopa katika taasisi fedha  benki.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari  amesema kuwa rada hizo zitafungwa katika viwanja vya ndege vya Dar es Salaam , Kilimanjaro, Songwe -Mbeya  pamoja na Mwanza.

Amesema kuwa TCAA kwa kufungwa rada hizo inakwenda kimataifa kutokana na huduma zinazotolewa na mamlaka hizo kuzingatia viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).

Aidha amesema kuwa rada hizo ni matokeo ya  serikali ya awamu ya tano katika kufikia uchumi wa kati kufikia 2025 unaoendana na pamoja na usafiri wa anga.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi wa TCAA, Profesa Longinus Rutasitara amesema kuwa TCAA imejibana katika vyanzo vyake na kuweza kununua rada hizo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akizungumza  wakati wa hafla ya utiaji wa saini ya mkataba  wa ufungaji wa mitambo minne  ya Rada ya kuongozea ndege  baina ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Kampuni ya Thales  Air System  ya nchini Ufaransa. Hafla hiyo pia imeambatana na uzinduzi wa nembo ya mpya ya TCAA  leo jijini Dar es Salaam. Wengine kwenye picha ni Makamu Mwenyekiti Bodi ya TCAA, Prof. Longinus Rutasitara, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari na Meneja Masoko wa Kanda wa Kampuni ya Thales  Air System, Bwana  Abel Curr. 
  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(wapili kushoto aliyesimama), akishuhudia  utiaji wa saini ya mkataba  wa ufungaji wa mitambo minne  ya Rada ya kuongozea ndege  baina ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kupitia Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Hamza S. Johari (Kushoto) na Meneja Masoko wa Kanda wa Kampuni ya Thales Air System ya nchini Ufaransa, Abel Curr .wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa( katikati), akishuhudia Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Hamza S. Johari (Kushoto) na Meneja Masoko wa Kanda wa Kampuni ya Thales Air System Abel Curr wakibadilishana nyaraka baada ya kutia saini ya mkataba wa ununuzi wa rada nne za kuongozea ndege. wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(katikati)  akikata utepe kuashiria uzinduzi wa nembo mpya ya TCAA  huku akishuhudiwa na makamu  Mwenyekiti Bodi ya TCCA, Prof. Longinus Rutasitara,(kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamza S. Johari.(kushoto) wakati wa hafla ya utiaji wa saini ya mkataba  wa ufungaji wa mitambo minne  ya Rada ya kuongozea ndege  baina ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Kampuni ya Thales  Air System  ya nchini Ufaransa leo jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa(kulia)  na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hamza S. Johari. (Kushoto) wakishangilia mara baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa nembo mpya ya TCAA, wakati wa hafla ya utiaji wa saini ya mkataba  wa ufungaji wa mitambo minne  ya Rada ya kuongozea ndege  baina ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) na Kampuni ya Thales  Air System  ya nchini Ufaransa leo jijini Dar es Salaam. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad