HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, August 27, 2017

RAIS MSTAAFU KIKWETE AIBUA MJADALA WA UTAWALA BORA, DEMOKRASIA

Kauli ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kutaka serikali barani Afrika kutochukuliwa vyama vya upinzani kama maadui, imewagusa wasomi na wanasiasa nchini wakitaka ifanyiwe kazi nchini.
Wamesema ni vyema Serikali ikakutana na wapinzani wakajadiliana njia bora ya kuendesha siasa bila kukwaruzana.
Wasomi hao wamesema alichofanya Kikwete ni kama kuanzisha ajenda ambayo inapaswa kuendelezwa, hasa kwa vile katika kipindi chake cha uongozi alijitahidi kukuza demokrasia na kusikiliza hoja za wapinzani.
Siasa za ushindani zilipigwa marufuku nchini mwaka 1965 na nchi ikaongozwa na chama kimoja hadi mwaka 1992 wakati Serikali ilipokubali kurejesha mfumo huo, licha ya kamati iliyoundwa kukusanya maoni kuonyesha kuwa ni asilimia 20 tu ndiyo waliotaka siasa za ushindani.
Katika siku za karibuni, wapinzani wamejikuta katika mapambano na vyombo vya dola, hukuwabunge wao wakikumbana na adhabu za mara kwa mara, jambo ambalo limewafanya walalamike kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haiwejengei mazingira mazuri ya kufanya siasa, hasa baada ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara.
Wakitoa maoni kwa nyakati tofauti kuhusu kauli hiyo ya Kikwete, wasomi hao wamesema upinzani haupaswi kuchukuliwa kama uadui unaopaswa kuwekewa vibano na masharti yanayowanyima fursa ya kutimiza haki yao inayopatikana ndani ya Katiba.
“Vyama vyote vya siasa vipo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo ni jambo la kushangaza vinapowekewa mipaka kutimiza majukumu yake,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (Rucu).
Alisema katika kipindi cha uongozi wake, Rais Kikwete alijitahidi kukuza demokrasia na kwa maana hiyo, kauli yake ina maana kubwa kwa vile imetolewa na mtu aliyekuwa madarakani na tena kutoka chama tawala cha CCM.
“Naunga mkono kauli hii ya Kikwete kwa kuwa sikutarajia kama ingeweza kutolewa (naye), lakini kwa vile amesema, naunga mkono kabisa. Tatizo tunalo, kikubwa kinachopaswa sasa ni jinsi ya kulitatua,” alisema.
Alisema kuendelea kuwabana wanasiasa kufanya shughuli zao ni sawa na kuwasukuma watafute mbinu ambazo wakati mwingine zinaweza kusababisha mtafaruku katika jamii.
Msomi huyo alisema matatizo mengi yanayozikumba nchi za Afrika yanayotokana na ukandamizaji wa demokrasia na watawala kushindwa kuheshimu matakwa ya wananchi kupitia vyama vyao vya siasa.
“Afrika, amani inatoweka kwa sababu ya hali kama hiyo. Usipopata nafasi, unaweza kufanya mambo ambayo yanaweza kusababisha mvurugano katika jamii,” alisema.
Alisisitiza kuwa suala lililoibuliwa na Rais Kikwete linapaswa kuchukuliwa kama fursa muhimu ya kuanzisha majadiliano kwa vile imetoa sura ya kuleta matumaini.
Hoja hiyo inalingana na Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyesema Rais Kikwete amekisema kile alichokiishi miaka 10 ya utawala wake.
“Hatupaswi kufika mahali Serikali iwaone wapinzani kama ni maadui au wapinzani waiona Serikali kama adui yao. Hawa wote wanajaribu kujenga nyumba moja hivyo lazima kuwe na mahali wanashirikiana,” alisema.
Alisema vyama vya upinzani nchini vimebanwa kutekelezwa wajibu wake na kufika wakati hata baadhi ya wanasiasa wanakamatwa wakati wakiendesha vikao vya ndani.
“Tulipiga hatua kubwa katika kukuza demokrasia, lakini sasa tumerudi nyuma zaidi, yaani miaka 20 ya vyama vingi badala ya kuendelea kupiga hatua kwenda mbele sisi tumerudi nyuma. Kwa maana hiyo, lazima wadau wajadili ili kukomaza demokrasia,” alisema.
Akitoa maoni yake kuhusu suala hilo, mkurugenzi wa watetezi wa haki za binadamu, Onesmo Olengurumwa alisema ni wakati muafaka sasa kwa marais waliopita kumshauri Rais John Magufuli jinsi atakavyofanya kazi na wapinzani kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Alisema hakuna upande unachukia maendeleo, hivyo lazima washirikiane akitoa mfano wa siasa za Kenya ambako pamoja na tofauti zao, bado wanasiasa wameendelea kusisitiza haja ya kuishi kwa umoja na kushirikiana katika mambo ya msingi.
“Kauli ya Rais Kikwete ina maana kubwa katika kuujenga upinzani na lazima ifahamike kuwa upinzani ni sehemu ya nchi na unayo haki ya kutoa maoni yao kama Katiba inavyosema,” alisema.
Nayo CCM imesema Rais Kikwete yupo sahihi kusema hivyo kwa vile hakuna siasa za uadui zinaendeshwa nchini.
Katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alisema Serikali ya CCM ndiyo iliyoanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa na kwa maana hiyo haiwezi kuendesha siasa zenye sura ya uadui.
“Labda uadui mkubwa upo wakati wa mapambano ya kura lakini hakuna jambo jingine baya,” alisema.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad