HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 23, 2017

NCC YATAKIWA KUTOA ELIMU YA UTATUZI WA MIGOGORO

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amelitaka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kuandaa mkakati wa kutoa elimu kwa Taasisi, Wizara na Halmashauri katika masuala ya utatuzi wa migogoro inayohusiana na sekta ya ujenzi.

Ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea na kuzungumza na uongozi wa Baraza hilo ambalo moja ya lengo lake ni kusuluhisha migogoro inayojitokeza katika sekta hiyo na kuhimiza umuhimu wa kutoa mafunzo ili kuepuka ucheleweshwaji wa miradi mingi ambayo inakwama kutokana na migogoro ya mikataba.

"Andaeni programu zitakazowasaidia viongozi wa Halmashauri na wakuu wa Taasisi ili kuwajengea uelewa kuhusu mikataba na utekelezaji wake kwa ajili ya kupunguza au kuondoa migogoro ambayo inaweza kuepukika”, amesema Eng. Ngonyani.

Aidha, Naibu Waziri Ngonyani amesisitiza kuwa uandaaji wa mikataba mbalimbali ya ujenzi nchini inatakiwa kushirikisha kwa pamoja wataalamu wa masuala ya ununuzi, uhandisi na wanasheria kuanzia hatua za awali hadi ukamilishaji wake ili kwa pamoja kutengeneza mkataba ulio na sifa na vigezo vinavyotakiwa.

"Naamini wataalamu hawa wakishirikiana mkataba hautakuwa na kasoro zozote na hivyo kupunguza migogoro kwani mikataba mingi nchini imekuwa ikiandaliwa na wataalamu wachache ambapo mwisho wake huonekana kuwa na mapungufu", amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.
Amelitaka Baraza hilo kuhakikisha kuwa ndani ya mwezi mmoja linaandaa na kuwasilisha taarifa kwake itakayobeba idadi ya migogoro wanayoishugulikia na vyanzo vyake ili kuweza kuitafutia ufumbuzi kwa haraka.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa NCC Dkt. Samson Mturi, amesema kuwa licha ya changamoto ya uhaba wa rasilimali watu walionayo sasa lakini bado wanaendelea na
utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha kuwa migogoro iliyowasilishwa ofisini kwao inafanyiwa kazi haraka.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ngonyani, ametembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na kusisitiza kwa kampuni hiyo kufanya kazi kwa kujituma na kusambaza huduma zake mijini na vijijini ili kuweza kuteka soko la utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, amemhakikishia Waziri Ngonyani kujikita katika kutatua changamoto za mawasiliano na kuahidi kusambaza huduma bora katika mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani amezungumza na uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania na kuwahimiza kufanya kazi kwa kasi na viwango vya ubora katika ujenzi wa nyumba za watumishi na viongozi hasa mkoani Dodoma ambapo ndipo yalipo Makao Makuu ya Serikali.
Naibu Waziri Ngonyani amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ili kujionea utendaji kazi na kupata mrejesho wa changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi hizo kwa lengo la kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuwahudumia wananchi na kuleta maendeleo chanya ya Taifa.  
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na baadhi ya watendaji wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), wakati alipotembelea ofisi za baraza hilo katika kikao kazi, jijini Dar es Salaam.
 Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Dkt. Samson Mturi akitoa taarifa ya utendaji kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wakati alipotembelewa na Waziri huyo, jijini Dar es Salaam.
 Mwanasheria kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Elias Kissamo (wa pili kushoto), akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu namna baraza hilo linavyoshughulikia migogoro ya mikataba katika sekta ya ujenzi, wakati alipotembelea baraza hilo, jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Eng. Omary Nundu akimkaribisha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, katika ziara yake ya kikazi katika kampuni hiyo, jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani (kulia), akifafanua jambo kwa Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), wakati alipokutana nao katika kikao kazi, jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Eng. Omary Nundu akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, kuhusu azma yao ya kuimarisha huduma za mawasiliano nchini. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba.
 Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba, akizungumza katika kikao kazi kilichokutanisha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Bodi na Menejimenti ya kampuni hiyo, jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Elius Mwakalinga akisisitiza jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wakati alipotembelea wakala huo, jijini Dar es Salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad