HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 20 August 2017

Mahakama yapiga ‘stop’ bomoabomoa Dar

Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi imeziwekea kinga ya muda nyumba 286 zisibomolewe wakati operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizoko ndani ya umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya Barabara ya Morogoro ikiendelea maeneo ya Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa juzi na Jaji Leila Mgonya kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wakazi hao 286 wa maeneo ya Ubungo- Maji hadi Kiluvya wakiomba itoe zuio la muda hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Maombi hayo ya zuio la muda kusubiri uamuzi wa kesi ya msingi yamepangwa kusikilizwa Agosti 30 mwaka huu baada ya upande wa wajibu maombi (Serikali) kuwasilisha hati ya kiapo kinzani.
Hata hivyo, wakati wakisubiri usikilizwaji wa maombi ya zuio la muda, wananchi hao kupitia kwa wakili wao, Benito Mandele waliwasilisha maombi ya dharura wakioomba mahakama hiyo iamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi maombi hayo yatakaposikilizwa.
Wakili Mandele amesema kuwa waliamua kupeleka maombi hayo ya kudumisha hali iliyopo kwa sasa baada ya kuona Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wameanza kutekeleza operesheni hiyo wakati maombi yao ya zuio yakiwa bado hayajasikilizwa.
Jaji Mgonya anayesikiliza shauri hilo alikubaliana na maombi hayo na kuamuru hali iendelee kuwa kama ilivyo kwa sasa hadi tarehe hiyo ya maombi hayo yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kwa uamuzi huo, Tanroads ambayo ndiyo mtekelezaji wa operesheni hiyo haitaweza kuzigusa nyumba hizo hadi hapo mahakama itakapoelekeza vinginevyo baada ya usikilizwaji wa maombi hayo ya zuio la muda kusubiri kesi ya msingi kumalizika.
Wakili Mandele amesema kuwa watakachofanya baada ya kupata hati ya amri hiyo ya mahakama wataitoa nakala nyingine na kuwagawia kila mdaiwa kwa ajili ya kuiweka kwenye nyumba yake.
Katika kesi ya msingi namba 284 ya mwaka 2017, wananchi hao wanaiomba mahakama itamke kuwa wao ni wamiliki halali wa maeneo hayo yenye mgogoro na kwamba hawapo katika hifadhi ya barabara.
Maombi hayo yanasikilizwa na Jaji Crencecia Makuru na amepanga kutoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo Agosti 30, uamuzi ambao ndio utakaotoa hatima ya maombi hayo kama yataendelea kusikilizwa au yatatupiliwa mbali.
Awali Tanroads ilimetoa notisi kwa wakazi wote walio katika umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara ya Morogoro kila upande, kuanzia Ubungo Maji hadi mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani kuvunja nyumba zao kwa madai kuwa wapo kwenye hifadhi ya barabara.

Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad