HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 18 August 2017

Kampuni ya Yussuf Manji kufutiwa leseni na TCRA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kusudio la kufuta leseni ya Kampuni ya Mycell inayomilikiwa na Quality Group Limited (QGL) ambayo imekuwa ikiongozwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Yussuf Manji.
Kwa mujibu wa sheria, TCRA iliyoanzishwa mwaka 2003 ina jukumu la kusimamia, kutoa na kufuta leseni za mawasiliano kwa kampuni yoyote ambayo imeshindwa kutekeleza majukumu iliyoyabainisha.
“Kampuni ya Mycell imeshindwa kurekebisha ukiukwaji wa masharti ya leseni,” inasomeka taarifa iliyotolewa na kuwekwa kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.
Kutokana na upungufu huo, “TCRA inauarifu umma kuhusu kusudio la kufuta leseni za Mycell za kujenga miundombinu kitaifa, kutoa huduma kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao na kutumia masafa ya mawasiliano.”
Kuonyesha juhudi ilizochukua kabla ya uamuzi huo, TCRA imesema Januari 27, 2016 ilitoa amri ya utekelezaji kwa kampuni hiyo kwa kukiuka masharti ya leseni walizopewa na kushindwa kutoa huduma kinyume cha Kifungu 21 (a) na (b) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Epoca) ya mwaka 2010.
Hata hivyo, Mycell haimo kwenye orodha ya kampuni zilizopewa leseni na TCRA ambazo zimo kwenye tovuti ya mamlaka hiyo.
Mamlaka hiyo imeeleza kwenye taarifa yake ya kusudio la kuifuta Mycell kuwa iliipa kampuni hiyo leseni nne tofauti Novemba 21, 2008.
Inafafanua kuwa leseni hizo ni ya kujenga miundombinu kitaifa, kutoa huduma kupitia miundombinu hiyo, kutoa huduma kupitia mtandao wa mawasiliano na kutumia masafa ya mawasiliano.
Kwenye ujumbe wake alioutoa Oktoba, 2011 wakati Quality Group ikitimiza miaka 35 tangu ianzishwe nchini, mwenyekiti wake wakati huo, Yusuf Manji alitabainisha vipaumbele vya utekelezaji walivyonavyo.
“Mycell inatekeleza mpango biashara unaoiruhusu kukodisha masafa iliyopewa na TCRA kwa kampuni ya nje yenye uwezo na uzoefu mkubwa. Inatarajia kujenga miundombinu imara itakayofanikisha miradi mbalimbali,” alisema Manji.
Alisema mpango huo unatokana na fursa kemkem zilizopo kwenye sekta ya mawasiliano nchini hasa kwa kuzingatia njia za kawaida za kufikishiana ujumbe ambazo zimekuwa hazikidhi mahitaji yaliyopo kutokana na kukua kwa kasi kwa teknolojia hasa ya habari na mawasiliano (Tehama).
“Sekta hii ina fursa nyingi kwa kampuni zenye teknolojia ya kisasa kuwekeza na kukua. QGL inaona kwamba kuna haja ya kuwekeza kwenye miundombinu na kuziruhusu kampuni za mawasiliano kuongeza ufanisi. Gharama za kupiga simu na data zipo juu nchini ikilinganishwa na ilivyo kwa nchi za Asia zinazonufaika na Tehama kwa kiasi kikubwa,” alisema Manji kwenye ujumbe wake wa mwaka 2011.
Mwaka 1997, Manji alianza kuiongoza QGL akihudumu kama ofisa mtendaji mkuu kabla ya baadaye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kundi hilo, nafasi aliyojiuzulu lakini baadaye akarejea tena na kuendelea kuiongoza.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad