HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, August 4, 2017

Hafla ya uzinduzi wa Tawi la NBM Haydom Mkoa wa Manyara

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang akizindua jengo la tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa Haydom. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang (wa tatu kulia) kikata utepe kuashiria uzindua wa jengo la tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa Haydom. Wa pili kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Straton Chilongola.

 KILIO cha wakazi wa jimbo la Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara cha kukosa huduma za kibenki toka Tanzania ipate uhuru,kimepata ufumbuzi wa kudumu baada ya NMB benki, kufungua tawi katika mji mdogo wa Haydom. 

Kwa mujibu wa mbunge wa jimbo la Haydom, Flatei Massay, katika kipindi chote hicho, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakilazimika kufuata huduma za kibenki Mbulu mjini, umbali wa zaidi ya kilometa 90.  

Mbunge Massy alisema kitendo cha kufuata huduma za kibenki umbali mrefu kiasi hicho, kumekuwa na madhara mengi na makubwa, ikiwemo gharama kubwa ya usafiri na pia usalama wa fedha. “Umbali huo umesababisha wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, kutunza fedha zao majumbani. 

Miaka ya nyuma majambazi yalitumia bomu kubomoa kasiri (sefu) la kutunzia fedha mali ya hospitali ya rufaa ya misioni Haydom na yalifanikiwa kuiba fedha, Pia fedha nyingi ziliungua kwa moto wa bomu”, alisema na kuongeza; “Zipo hisia kwamba majambazi hayo yalihisi hospitali hiyo haipeleki fedha benki kwa wakati kutokana na umbali mrefu benki ilipo, kwa hali hiyo yalitarajia kupata fedha za kutosha”. 

Mbunge huyo alisema kufunguliwa kwa benki hiyo yenye mashine mbili za kutolea fedha, wananchi na wafanyabiashara, wanapaswa kuitumia kikamilifu, ili kupanua kilimo na biashara zao. Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufunguzi huo, kaimu mkuu wa mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally, ameihimiza benki ya NMB kuongeza juhudi zaidi katika kuendelea kutoa mikopo na huduma zingine kwa wakazi wa vitongoji vyote mkoani Manyara. Alisema serikali ya awamu ya tano imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini, hivyo mikopo inayotolewa na mabenki ikiwemo NMB, itasaidia kuendeleza kukuza uchumi na kuongeza ajira. 

Ameongeza kwa kuwahimiza wananchi wa Haydom, kuchangamkia uwepo wa benki ya NMB, ili kutumia huduma zao za kibenki kupata maendeleo yao binafsi, wilaya ya Mbulu na mkoa wa Manyara kwa ujumla. “Serikali inawapongeza NMB kwa kutambua umuhimu wa kusaidia jamii. Ni ulweli usiofichika kuwa faida mnayopata katika huduma zenu za kibenki, inatokana na wananchi. Hivyo kusaidia jamii ni njia nzuri ya kurudisha shukrani kwa waliosaidia mkapata faida”, alifafanua Sara. Awali meneja wa NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, alisema NMB tawi la Haydom, litahudumia vijiji na viitongoji vya Maghani, Labai, Maritadu, Endamilayi, Getanyamba na Dongobeshi. 

Aidha, alisema benki hiyo imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye kuzingatia mahitaji halisi ya soko kwa wakati husika. “Moja ya bidhaa hizo, ni kampeni ya ‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni mahususi kabisa kwa wajasiriamali wadogo wadogo. Wajasiriamali hao ni pamoja na baba/mama lishe, wauza chipis, wenye maduka ya biashara yakiwemo ya nguo”, alifafanua Chilongola. Akifafanua zaidi,alisema akaunti hiyo inampa fursa mteja kupata mkopo wa shilingi laki tano hadi shilingi 30 milioni. 

Pia meneja huyo, alisema wanayo akaunti nyingine ya ‘Wajibu’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto wenye umri wa miaka 0-18. “Kwa upande wa teknolojia, tuna akaunti ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii mteja anaweza kufungua akaunti kwa muda mfupi na papo hapo kupata kadi yake ya ATM, na kuanza kufanya miamala wo wote”, alisema Chilongola. Benki ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na mashine za kutolea fedha zaidi ya 700 nchi nzima.Ina wateja zaidi ya milioni mbili jambo linaloifanya kuwa benki pekee nchini yenye hazina ya wateja wengi kuliko benki zingine zilizopo nchini.

Burudani zikiendelea. Meneja wa NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, akitoa taarifa yake kwenye hafla ya uzinduzi wa tawi la NMB Haydom mkoani Manyara. Hafla hiyo imefanyika katika mji mdogo wa Haydom. Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Haydom,waliohudhuria uzinduzi wa tawi la NMB katika mji mdogo wa Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara juzi. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa tawi la NMB tawi la Haydom wilaya ya Mbulu uliofanyika juzi katika mji mdogo wa Haydom.Wa kwanza kushoto (waliokaa) ni meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola na mbunge wa jimbo la Haydom, Flatei Massy.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad