WATU
wengi wamekuwa wakikuta na kuvipita vifaa mithili ya mabomba ya kutoa maji pembezoni
mwa barabara, maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, viwanja vya ndege au viwanja
vya michezo bila kufahamu vinafanya kazi gani.
Wengine
hudhani ni mapambo ya barabara au alama Fulani kwenye maeneo hayo, ambapo baadhi
yao hudiriki kuyatumia kinyume na kazi yake kutokana na kutotambua matumizi yake.
Mabomba
haya (fire hydrants) sio mapambo bali ni mfumo uliounganishwa na mabomba makubwa
ya maji, na kuwa visima vya maji ambapo gari la Zimamoto huchukua maji. Visima hivi
vimejengwa makusudi kwa ajili ya kulirahisishia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kukabiliana
na majanga ya moto pindi yanapotokea.
Mabomba
hayo (Fire Hydrant) yana msukumo mkubwa wa maji na kusababisha maji yatoke kwa wingi
na kwamuda mfupi. Uwepo wa vifaa hivyo sehemu mbalimbali za makazi ya watu na
maeneo mengineyo hurahisisha zoezi zima la uzimaji moto, kwani pindi gari la
kuzima moto linapoishiwa maji hujazwa hapohapo badala ya kuyafuata mbali na eneo
la tukio.
Kwa
kawaida magari ya zimamoto yana ujazo tofauti wa maji kuanzia lita 2000 hadi lita
16,000 ambapo ni ujazo mkubwa zaidi. Magari haya hubeba maji ya awali kwa ajili
ya huduma ya kwanza ndio maana visima hivyo ni muhimu kuwepo.
Kwa
nini tunasema ni maji kwa ajili ya huduma ya kwanza, ni kwa sababu ujazo wa maji
yanayobebwa na gari la zimamoto ambao ni kati ya lita 2000 na lita 16000,
hutoka kwamsukumo mkubwa, ambao kwa dakika moja maji yatatoka zaidi ya lita
1000 ukiwa unatumia mstari mmoja wa mpira wa maji (hose) na kusababisha maji hayo
kuisha kwa muda mfupi.
Ukosefu
wa visima hivyo sehemu mbalimbali, unapelekea Jeshi kushindwa kukabiliana na majanga
ya moto kwa ufanisi baada ya maji yanayokuwa kwenye gari kuisha na kuwalazimu kwenda
eneo la mbali.
Ingawa
Jeshi la zimamoto na uokoaji linajitahidi kadri iwezekanavyo kuhakikisha linakabiliana
vya kutosha na majanga ya moto kwa kusambaza visima hivi vya maji, lakini marakadhaa
limekuwa linakumbana na changamoto mbalimbali hasa miundombinu.
Katika
kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa, tayari baadhi ya Mikoa kama vile Dar es
Salaam, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha na Tanga imejitahidi kuhakikisha miundombinu
yake inakidhi kuruhusu ujenzi wa visima vya maji ya kuzimia moto na utaratibu umeandaliwa
kuhakikisha mikoa Mingine inaboresha miundombinu yake kwa kuzingatia ujenzi wa huduma
hiyo.
Pamoja
na changamoto hizo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji bado linatekeleza wajibu wake kwa
kuwa elimisha wananchi namna ya kutunza miundombinu hiyo na kusambaza mifumo hiyo
kwa kiwango kinacho hitajika.
Wito
kwa wananchi tuyatunze mabomba hayo (fire hydrant) kutokana na kuwa na umuhimu
katika kurahisisha shughuli za kupambana na majanga ya moto, kwani kumekuwa na
wimbi kubwa la uuzaji wa vyuma chakavu.
Web site: www.frf.go.tz
IMEANDALIWA
NA KITENGO CHA HABARI NA ELIMU KWA UMMA-MAKAO MAKUU YA JESHI LA ZIMAMOTO NA
UOKOAJI.
No comments:
Post a Comment