HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 10 July 2017

WIZARA YA AFYA YAZINDUA MPANGO WA KUTEMBELEA HOSPITALI ZA UMMA NCHINI

Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezitaka hospitali nchini kutumia miongozo katika kutekeleza shughuli mbalimbali za huduma za afya  pamoja na kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuwapo kwa mawasiliano kati ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na hospitali nyingine za rufaa nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa wizara hiyo Dk. Mpoki Ulisubisya wakati akizindua mpango wa kufuatilia utoaji wa huduma za afya yakiwamo mafanikio na changamoto katika hospitali za umma nchini.

Dk Ulisubisya amesema mpango wa wizara yake ni kuzitembelea hospitali za umma nchini utaanzia kwenye hospitali za kibingwa ili ziwe kitovu cha kutoa mafunzo kwa hospitali nyingine nchini.

“ Malalamiko ni mengi yanapaswa kushughulikiwa kwa kuwekwa mifumo imara ya utekelezaji wa shughuli za huduma za afya kwa lengo la kuzuia kushuka kwa ubora wa huduma. Pia, hali hii itasaidia kuimarisha maadili miongoni mwa watumishi,” amesema Dk Ulisubisya wakati akizindua mpango huo leo.

Amesema wizara ya afya itaendelea kushirikiana na kitengo cha elimu ya afya kwa umma ili kuhakikisha watumiaji wa huduma za tiba wanafahamu mfumo na taratibu za upatikanaji wa huduma za tiba katika ngazi mbalimbali ili kuondoa usumbufu na malalamiko kutoka kwa wagonjwa.

Akizungumzia maslahi ya wafanyakazi, amesema serikali inafanyia kazi maombi ya kuboreshwa kwa maslahi yao na kwamba wachape kazi kwani inakumbuka suala hilo.

Pia, Dk Ulisubisya aliipongeza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa juhudi  kubwa ya kuboresha huduma za afya kwa kupanua huduma za afya, kusomesha wataalamu wa afya na kununua vifaa tiba.

“Muhimbili mnafanya kazi nzuri na kubwa, naamini taasisi nyingine zitajifunza kwenu, mna mambo makubwa ya kujivunia,” amesema.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Dorothy Gwajima amefafanua lengo la ziara yake ni kuwezesha kupatikana kwa taarifa kwa wakati na utasaidia katika utekelezaji wa  huduma za afya katika hospitali nchini.

Dk. Gwajima amesema kuwa mfumo huo utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa wa katika Hospitali ya Taifa  ya Muhimbili.

“Kutakuwa na ratiba ya kudumu ya vikao kati ya wizara na watoa huduma kuhusu utekelezaji wa huduma za tiba. Taarifa za halmashauri lazima zikutane ili kujua hali za huduma za afya kwenye halmashauri zenu, hivyo kutakuwa na kamati mbalimbali ili kuwasilisha ufuatiliaji wa shughuli za huduma za afya.

Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru akizungumzia juhudi za kuboresha huduma za afya, amesema kuwa upatikanaji wa dawa MNH ni asilimia 95 kutoka asilimia 40. Pia, amesema Muhimbili inatarajia kupata wataalamu 18 kutoka Cuba wa masuala ya mionzi, usingizi, macho na masikio.

Pia, Profesa Museru ameiomba serikali kuipatia Muhimbili kibali cha kuajiri wataalamu mbalimbali kwa kuwa ina upungufu wa wafanyakazi karibu 300 kutokana na baadhi ya wafanyakazi kustaafu, kupoteza maisha na wengine  130 kubainika kuwa na vyeti feki.

 Ziara hiyo imeanza rasmi leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na maofisa wa wizara hiyo wametembelea Idara ya magonjwa ya Dharura na Ajali, Idara ya Maabara Kuu na idara mbalimba ambako wamezungumza na wafanyakazi pamoja na wagonjwa.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya akizungumza katika mkutano wa kuzindua mpango wa kuzitembelea hospitali za umma nchini ili kujua mafanikio na changamoto zilizopo kwenye hospitali hizo. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru na Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Dorothy Gwajima wa wizara hiyo. Mpango huo umeandaliwa na wizara ya afya na ziara hiyo imeanza rasmi leo Muhimbili.
 Baadhi ya wataalamu wa afya kutoka Muhimbili na taasisi nyingine wakimsikiliza Katibu Mkuu, Dk Ulisubisya katika mkutano wa uzinduzi uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Dorothy Gwajima (kushoto) wa wizara hiyo pamoja na wataalamu wengine wakifuatilia mkutano huo leo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa mpango wa kutembelea hospitali za umma ili kujua mafanikio na changamoto  zilizopo kwenye hospitali hizo.
 Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dk Juma Mfinanga wa Muhimbili akimwelekeza jambo Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, Dk. Dorothy Gwajima (kushoto) wa wizara ya Afya wakati wa ziara ya kutembelea hospitali hiyo leo. Wengine ni maofisa kutoka wizara ya afya na hospitali ya Muhimbili.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Afya, Nsacris Mwamaja wakichukua maelezo kutoka kwa Sister Mushi  wakati wa ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad