HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 27 July 2017

Wafanyakazi Benki ya NMB Kilosa wamnunulia mguu wa bandia mtoto mlemavu

WAFANYAKAZI wa Benki ya NMB wilayani Kilosa, Morogoro kwa kushirikiana na Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) cha benki hiyo wametoa msaada kwa mtoto Sheila Bushiri (7) ambaye alizaliwa akiwa mlemavu wa mguu mmoja kufanyiwa upasuaji na kumnunulia mguu wa bandia ili aweze kutembea kama watu wengine. 

Akizungumza kuhusu msaada huo, Meneja wa tawi la benki ya NMB KIlosa, Dismas Prosper alisema walimjua mtoto huyo kupitia Bi. Shalphina Lipinga ambaye alikwenda ofisini kwao kuomba msaada wa kusaidia watoto wenye uhitaji na baada ya kuwaonyesha mtoto huyo waliona kuna haja ya kumsaidia. 

Alisema baada ya kumwona wao kama wafanyakazi walichangishana pesa na kutokana na utaratibu wa benki hiyo kuwa iwapo wafanyakazi wakichangishana pesa kitengo cha CSR kuwaongezea pesa sawa na kiwango walichotoa walifanikisha mtoto huyo kufikishwa kwenye hospitali ya CCBRT iliyopo Dar es Salaam ambapo alipatiwa matibabu.

Sheila akiwa katika picha na wafanyakazi wa tawi la NMB wilayani Kilosa, Morogoro ambao ndiyo waliotoa msaada kwa kushirikiana na Mkuu Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kumsaidia mtoto huyo kufanyiwa upasuaji kwenye hospitali ya CCBRT na kupewa mguu wa bandia ambao kwa sasa unamwezesha kutembea tofauti na awali.


 “Alikuja ofisini Shalphina kusema kuwa anasaidia watoto ambao hawajiwezi na katika maongezi alisema kuna mtoto alizaliwa na ulemavu wa mguu mmoja na anaishi na bibi yake na anampeleka shule kila siku akimbeba mgongoni hivyo kama kuna mvua hawezi kwenda shule, mimi nikaona hapo kuna shida kubwa, “Nilipoona picha hana mguu mmoja kama mzazi iliniuma sana, niliweza kuwasilisha kwa wafanyakazi wenzangu na nilipowauliza nini tumfanyie wengi walipendekeza baiskeli na tukakubaliana kuchanga, alipopelekwa CCBRT walishauri apate mguu wa bandia na wafanyakazi wengi wakalikubali,” alisema Prosper. 

Prosper alisema lengo la wafanyakazi hao kutoa msaada ni kumwona mtoto huyo akiwa na furaha na kuendelea na masomo yake vizuri na kwasasa wana mpango wa kuendelea kutoa msaada kwa watu wengine ambao wanahitaji kupata msaada ili kuendesha shushuli zao za kila siku kama watu wengine ambao hawana ulemavu.
 
Mwonekano wa mguu wa mtoto Sheila Bushiri kabla ya kusaidiwa na wafanyakazi wa Benki ya NMB Kilosa kufanyiwa upasuaji na kupewa mguu wa bandia.

 “Mwisho wa siku tulifanikiwa kuweka tabasamu kwenye uso wa yule mtoto kwa kutumia kile kidogo ambacho Mungu ametusajilia tumsaidie na sio kwa yule mtoto tu tuna malengo ya kuendelea kusaidia wengine ili na wao wapate tabasamu,” alisema Prosper. Kwa upande wa bibi yake Sheila, Habiba Said ambaye ndiyo anaishi na mtoto huyo alisema mtoto huyo alizaliwa na ulemavu huo na akiwa na miezi tisa mama yake alimwacha nyumbani na kuondoka huku baba wa mtoto akiwa hajulikani. 

Alisema alimlea mpaka anaanza shule lakini alikuwa akikabiliwa na changamoto ya kutembea jambo ambalo lilisababisha muda mwingine kushindwa kwenda shule na hata kushiriki michezo na wenzake lakini NMB wamempa msaada ambao utamsaidia kufanya mambo ambayo alikuwa anashindwa kuyafanya awali. 
 Meneja wa Kitengo cha Uwajibikaji (CSR) cha Benki ya NMB, Lilian Kisamba akizungumza na wanafunzi wa darasa ambalo Sheila anasoma.

“Sheila alizaliwa vilevile, mama yake alivyomzaa akiwa na miezi tisa aliondoka na nimemlea kama kawaida baada ya kukua nikampeleka shule kwa kumbeba mgongoni…nilikutana na mama Joy (Shalphina Lipinga) nikamwelea na akasema ataongea na NMB watamsaidia, “Mwanzoni alikuwa anapata shida kutembea lakini kwasasa anaweza kutembea vizuri yeye mwenyewe, naishukuru NMB kwa msaada huo, alikuwa hachezi na wenzake lakini kwa sasa hivi anacheza kama kawaida na anakwenda shule mwenyewe na kurudi vizuri, nawashukuru sana,” alisema Habiba. 
 Mkuu wa Shule ambayo anasoma Sheila ya Mazinyungu, Kajika Galani (kulia) akitoa taarifa ya maendeleo ya masomo ya Sheila kwa Meneja Kitengo cha Uwabikaji (CSR) cha Benki ya NMB, Lilian Kisamba.

Naye Mkuu wa Shule ambayo anasoma Sheila ya Mazinyungu, Kajika Galani aliishukuru NMB kwa msaada ambao imetoa kwa mwanafunzi wake Sheila na kwa shule hiyo kwa kuipatia msaada wa madawati 78 ambao yamesaidia kumaliza tatizo la madawati shuleni hapo. 

“NMB tunawashukuru sana pindi mtoto nakuja kuandikishwa hapa alikuwa kwenye mazingira magumu sana bila bibi yake alikuwa hawezi kuja lakini wafanyakazi wa NMB wamemsaidia na tangu amesaidiwa sijamwona tena bibi yake na hata akiwa shule anashiriki michezo na wenzake kama kawaida, “Mmemsaidia sana naamini hata kusoma kwake kutakuwa vizuri pia hata bibi yake mmemsaidia sana hasa kipindi cha mvua alikuwa lazima awahi kumchukua lakini sasa atatembea mwenyewe … pia napenda kushukuru kwa msaada wa madawati 78 ambayo mmetusaidia, asilimia kubwa ya wanafunzi kwa sasa wanakaa kwenye madawati,” alisema Galani.
 
Mwonekano wa mguu wa wa mtoto Sheila Bushiri baada ya kusaidiwa na wafanyakazi wa benki ya NMB Kilosa kufanyiwa upasuaji na kupewa mguu wa bandia.
 Baada ya kusaidiwa mguu wa bandia Sheila sasa anaweza kucheza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad