HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 18, 2017

TRA Yamkana Ngeleja Sakata la fedha za Escrow

Waziri wa Nishati na Madini wa zamani Ngeleja ni mmoja kati ya watu waliopokea mgawo wa fedha zinazodaiwa kuwa zao la kashfa ya Tegeta Escrow, lakini akatangaza kuzirejesha kwa TRA Jumatatu iliyopita.

Februari 2014, Ngeleja ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema (CCM) aligaiwa Sh. milioni 40.4 na mfanyabiashara maarufu James Rugemalira ambaye mwanzoni mwa mwezi alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 12, yakiwamo ya kughushi na utakatishaji fedha.

Hata hivyo, wakati Ngeleja akithibitisha kwa risiti mbele ya waandishi wa habari kuziingiza fedha hizo katika akaunti ya TRA, mamlaka hiyo imesema haizitambui. TRA imesema haina mpango wowote wa kufuatilia fedha hizo kwa sababu shughuli yake ni kukusanya kodi.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo inahusika na kuhakikisha serikali inakusanya kodi stahiki na siyo urejeshaji wa fedha za kashfa kama Escrow.

Kayombo alitoa ufafanuzi huo wakati alipoulizwa na Nipashe juu ya utaratibu rasmi uliopo wa urejeshaji wa fedha hizo endapo wanufaika zaidi wa mgawo wa Rugemalira watataka kufuata nyayo za Ngeleja.

Akifafanua zaidi juu ya suala hilo, Kayombo alisema TRA haihusiki na fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa hazikuwa mali yake.

Aidha, Kayombo alisema TRA haiwezi kuzizungumzia fedha hizo kwa kuwa hazijawahi kuwa mali yake na kuelekeza watafutwe wenye fedha hizo kwa ufafanuzi zaidi.

“Fedha za Escrow zinaihusu vipi TRA? Tunawezaje kukaa na kuzungumzia fedha ambazo si zetu?” Alisema Kayombo. “Mimi nashauri watafutwe wenyewe wazungumze kama wanataka kurejesha… siyo sisi.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu aliiambia Nipashe wiki iliyopita kuwa uamuzi wa Ngeleja kupeleka fedha za hizo TRA unazua maswali zaidi kwa kuwa alipewa na Rugemarila, na viongozi wa awamu ya nne ya serikali walisema siyo za umma bali mtu binafsi.

Lakini akizungumza jijini Jumatatu iliyopita Ngeleja alisema amerejesha mgawo huo kwa TRA kwa kuwa pamoja na sababu nyingine, ili kujiweka kando na kashfa.

Alisema aliyetoa mgawo huo ameshakamatwa na Takukuru na ana kesi inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Huku akionyesha stakabadhi ya malipo ya Benki ya CRDB tawi la Tower, Ngeleja alisema pia “nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa au tuhuma hizo.”

“Nimesononeshwa na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma.” 

Alisema alipokea mgawo huo Februari 12, 2014 na Januari 15, 2015 alilipa kodi kwa TRA kiasi cha Sh. 13,138,125 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya msaada huo aliopewa.
 
Hakusema ni kwa nini ulipita muda mrefu kati ya kupokea na malipo ya kodi.

Baada ya Ngeleja kurejesha fedha hizo palikuwa na wito kutoka kwa wanasiasa na wanaharakati waliotaka wote waliopata mgawo huo kurejesha fedha hizo kwa TRA kama alivyofanya waziri huyo wa zamani.

MASHTAKA 12
Rugemalira na mwenzake, mmiliki wa Kampuni ya Pan African Power (PAP), Harbinder Singh Sethi walisomewa mashtaka 12 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Julai 3.

Mashtaka hayo ni pamoja na ya kugushi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya dola zaMarekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4 kwa serikali.

Novemba 26, 2014, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliwasilisha mjini Dodoma ripoti ya uchunguzi wa kashfa Tegeta Escrow ambapo ilisema Sh. bilioni 306 zilichotwa kutoka Benki Kuu kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa kamati hiyo wakati huo, Zitto Kabwe alisoma ripoti na kulithibitishia Bunge kwamba viongozi na wafanyakazi wa Serikali, wafanyabiashara, viongozi na taasisi za dini, mabenki na watu binafsi walihusika katika ufisadi.

Ripoti ya PAC ilianika orodha ya waliopata mgawo huo kuwa mbali na Ngeleja ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge ambao kila mmoja alipata Sh. bilioni 1.6.

Wengine ni ofisa katika Ofisi ya Rais wakati huo, Shabani Ngurumo aliyepewa Sh. milioni 80, Jaji wa Mahakama Kuu, Eudes Ruhangisa alipata Sh. milioni 404.25 na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco), Dk. Enos Bukuku, aliyepewa Sh. milioni 161.7.

Katika ripoti hiyo Waziri wa Nishati na Madini wa serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, Mbunge wa zamani wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko na Jaji wa zamani wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Aloisius Mujulizi walitajwa kupatiwa Sh. milioni 40.4 kila mmoja.

Wengine ni ofisa wa TRA, Lucy Apollo Sh. milioni 80.8, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko Sh. milioni 40.2, maaskofu Methodius Kilaini Sh. milioni 80.9 na Eusebius Nzingirwa Sh. milioni 40.4, Padri Alphonce Twimannye Sh. milioni 40.4, maofisa wa Rita Placidus Luoga Sh. milioni 121.2 na Theophil Rugozobwa Sh. milioni 323.4.

BAJETI WIZARA
Mgawo waliopata wabunge, maofisa wa serikali na viongozi wa dini kutoka kwa Rugemalira unatosha bajeti ya mwaka mzima ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Nipashe imegundua.

Katika miaka mitatu iliyopita ya bajeti (2014/15, 2015/16 na 2016/17), wizara hiyo ambayo kwa sasa iko chini ya Waziri Dk. Harrison Mwakyembe, ilitengewa bajeti ya Sh. bilioni tatu kila mwaka, ikiongoza wizara zote 18 kwa kuwa na bajeti ndogo zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wakati wizara hiyo ikiambulia Sh. bilioni moja (theluthi ya bajeti yake ya maendeleo) hadi inapofika robo tatu ya mwaka wa bajeti katika miaka hiyo mitatu, imebainika Sh. bilioni 4.77 zinazodaiwa zao la kashfa ya uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow walizopatiwa waheshimiwa hao zingetosha kugharamia kikamilifu miradi ya maendeleo ya wizara hiyo kwa mwaka mzima na ‘chenji’
ya Sh. bilioni 1.7 ikabaki.

Katika mwaka uliopita wa fedha, kwa mfano, kati ya Sh. bilioni tatu zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo, ni Sh. bilioni 1.19 tu (asilimia 40) ndizo zilizokuwa zimetolewa hadi Aprili 30, mwaka huu kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe.

Chanzo: Nipashe

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad