HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 16 July 2017

TAMASHA LA KUSHAJIISHA ELIMU YA MAFUNZO YA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UHANDISH WA HESABU LAZINDULIWA ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akionyesha umahiri wake wa kucheza ngoma ya Ndege wakati akizindua Tamasha la kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu {STEM} kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein hapo Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Balozi Seif akizindua Tamasha la kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu {STEM} kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Baadhi ya wageni na walikwa kutoka Chuo Kikuu cha cha George Mason cha Nchini Marekani wakishuhudia uzinduzi wa Tamasha la kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu { STEM}.

Balozi Seif akisalimiana na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Profesa Mshimba nje ya Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi wakati wa mwanzo wa mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu { STEM.

Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Walimu wa Hesabu Tanzania Mwalimu Said Sima.


Mkuu wa Timu ya Wakufunzi kutoka Chuo Kikuu cha George Mason Nchini Marekani Profesa Padu kati kati akimpatia maelezo Balozi Seif juu ya ufundishaji wa masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hesabu kwa wanafunzi wa Fani hiyo. Nyuma ya Profesa Padu ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uwezeshaji kwa wote Zanzibar { JUZA }iliyoandaa Mafunzo hayo ya STEM Bibi Giftness Castico. Picha na – OMPR – ZNZ


                                                                                           Na Othman Khamis. OMPR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema ni dhahiri kwamba Maendeleo ya Nchi au Taifa lolote Duniani yanategemea juhudi zinazochukuliwa na Taifa hilo katika kukuza na kuendeleza Sayansi na Teknolojia.

Alisema fani hizo mbili ndio msingi imara katika kuwapata wahandisi waliobobea kwenye nyanja mbali mbali huku ikifahamika kwamba msingi wa mambo yote hayo kwa kiasi kikubwa unatokana na uweledi wa Taaluma ya Hesabu kama wataalamu walivyokubaliana kwamba Hesabu ni Mama wa Sayansi.

Dr. Shein alieleza hayo wakati akizindua Tamasha la kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu { STEM} katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar alisema Taifa lazima liwe na wataalamu wake wenyewe katika sekta mbali mbali pamoja na Teknolojia ya kisasa katika utekelezaji wa mipango ya Maendeleo iliyoandaliwa na Serikali katika sekta zote za Kiuchumi na Kijamii.

Alisema Serikali inahitaji Sayansi na Teknolojia katika kuendeleza sekya ya Kilimo, Afya miundombinu ya Bara bara pamoja na utekelezaji wa Mipango Miji iliyokwishaanzishwa.


Dr. Shein alieleza wazi kwamba mpango huo wa STEM unahitaji kuendelezwa kwa nguvu zote ili Taifa liweze kujitegemea kwa kuwa na Wataalamu Wazalendo katika fani tofauti na hatimae iweze kujiendesha na kusimamia mambo yake yenyewe.


Alisema kwa kutambua umuhimu wa Sayansi na Teknolojia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi za kuimarisha ufundishaji wa masomo hayo kuanzia elimu ya Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu huku ikiimarisha vyuo vya Ufundi kwa kujenga Vituo vipya vya Mfunzo ya Amali pamoja na kuviimarisha vilivyopo hivi sasa.

Alifahamisha kwamba Serikali Kuu tayari imeanza ujenzi wa chuo kipya cha Amali kiliopo Mtambwe Kisiwani Pemba na Makunduchi Kisiwani Unguja ili kuwawezesha Vijana wa Maeneo hayo kupata elimu ya Ufundi wa kazi mbali mbali na hatimae waweze kujiajiri watakapomaliza mafunzo yao.

Rais wa Zanzibar alielezea matumaini yake kwamba Vijana wengi Nchini watahamasika, kuupokea na kuuendeleza vizuri mpango huo wa kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi ya Hesabu { STEM} katika ngazi zote za Elimu kama wanavyofanya Vijana wengine katika Mataifa mbali mbali Duniani.

Dr. Shein aliwashauri wasimamizi wa mpango huo kuwatumia Wataalamu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania { COSTECH} ambao wamekubali kushirikiana nao kwa vile watendaji wa Tume hiyo ni mahiri na makikni waliobobea.

Alieleza kwamba lengo la kwenda sambamba na kasi pamoja na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia, ni lazima jamii yote ikubali kushirikiana ili kuhakikisha kwamba Vijana wanapenda kusoma na kuchagua mafunzo yanayohusiana na Taaluma hiyo ya Sayansi, Teknolojia na uhandisi wa Hesabu.

Dr. Shein amewahimiza Vijana wa Kike waendelee kuongeza bidii ili waweze kujijengea sifa waliyoidhihirisha katika matokeo yao ya Mitihani wakati wa kufaulu vyema mafunzo yao ya sekondari na vyuo mbali mbali yanayoendelea kushuhudiwa hapa Nchini.

“ Nawahimiza na kuwatia moyo Wanafunzi Wanawake waupokee vizuri mpango huu wa STEM kutokana na uwezo wao mkubwa wa kujifunza masomo ya Sayansi na Hesabu unaowapa fursa ya kuchukuwa zawadi za Wanafunzi bora wa masomo hayo ”. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitanabahisha Vijana wote Nchini umuhimu wa kutambua kwamba wasipoongeza kasi ya kujifunza mafunzo ya Sayansi na Teknolojia wanaweza kujikuta wameachwa nyuma na Vijana wenzao Duniani.

Alisema ni vyema wakazingatia kwamba Maendeleo ya haraka yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni katika baadhi ya Mataifa machanga kama China na India ni matokeo ya juhudi zao katika kushajiisha masomo na mafunzo ya Sayansi na Teknolojiapamoja naUhandisi na Hesabu.

Dr. Shein alifafanua wazi kuwa Mataifa hayo yaliyopiga hatua kubwa ya kiuchumi kwa kiasi kikubwa yameacha kuwategemea Wataalamu kutoka Nje ya Nchi zao na tayari yamejipanga vizuri katika kuendeleza rasilmali zao wenyewe bila ya kuyategemea Mataifa mengine.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar pamoja na Jumuiya ya Uwezeshaji kwa wote Zanzibar { JUZA } kwa juhudi walizochukuwa za kushirikiana na wadau wengine katika kufanikisha Tamasha hilo.

Dr. Ali Mohamed Shein kuunga mkono Mpango huo wa STEM amekubali kulipokea ombi lao la kuwawezesha kuanzisha Kituo muhimu na Maalum kwa Vijana katika kutoa Elimu, kushajiisha na kuendeleza Mpango wa STEM { STEM STOP CENTER – SSC } ili ifahamike na kutumika ipasavyo.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uwezeshaji kwa wote Zanzibar { JUZA } Bibi Giftness Castico alisema Jumuiya hiyo ikipata kuungwa mkono kiuwezeshaji ina uwezo na Taaluma ya kutosha ya kutoa mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Hesabu Maskulini Unguja na Pemba.


Bibi Giftness alisema licha ya JUZA kujipanga kufanya Tamasha kila Mwaka lakini mipango ya awali tokea kuanzishwa kwake mwaka 2017 yalielekezwa katika mapambano dhidi ya udhalilishaji wa Kijinsia.

Alisema mpango huo ulioungwa mkono na Wananchi na Taasisi mbali mbali ndani na nje ya Nchi umeleta mafanikio makubwa na Ripoti ya mpango wa Jumuiya hiyo utaufikishwa Serikalini kwa kuchukuliwa hatua zitakazostahiki.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Uwezeshaji kwa wote Zanzibar { JUZA } alifahamisha kwamba lengo la mafunzo hayo litapangwa na kuelekezwa kwa wanafunzi wa skuli za Msingi, Sekondari hadi Vyuo Vikuu.

Akitoa salamu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika uzinduzi huo wa Tamasha la kushajiisha Elimu ya Mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Uhandisi wa Hesabu Naibu Waziri wa Wizra hiyo Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri aliahidi kwamba Wziara ya Elimu itaendelea kujenga msingi mzuri utakaowawezesha Vijana kupendelea na kuendelea kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia na Hesabu.

Mh. Mjawiri aliwaomba Wafadhili na Wadau wa Sekta ya Elimu ndani na nje ya Nchi kuendelea kuiunga mkono Wizara hiyo na tayari imeshikitita kushirikiana na wadau hao katika kusimamia masomo ya Sayansi ambayo hayasomeshwi kwa kubahatisha.

Alisema Walimu na wakufunzi wa masomo na mafunzo ya Sayansi, Teknolojia na Hesabu lazima wajengewe misingi imara itakayowapa mbinu na fursa za kusomesha Kitaalamu na kwa uhakika.

Naibu Waziri huyo wa Elimu na Mfunzo ya Amali aliwahakikishia Walimu wa Hesabu kwamba Wizra ya Elimu iko tayari kuwawezesha walimu wa Somo hilo kuunda Chama chao endapo watafikia hatua ya kufanya hivyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad