HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 11, 2017

MAGEREZA KUPANUA KIWANDA CHAKE CHA VIATU CHA KARANGA MJINI MOSHI

Jeshi la Magereza nchini limeanza kutekeleza mpango wake wa kupanua shughuli za uzalishaji wa kiwanda cha Viatu cha Karanga  kilichopo mjini Moshi  mkoani Kilimanjaro  sambamba na kujenga Kiwanda Kipya cha Viatu  katika eneo hilo hilo ili kupanua huduma zake kwa wananchi na hivyo kukidhi mahitaji ya soko la sasa.
Hatua hii ni moja ya kati ya Mikakati ya Jeshi la Magereza nchini Tanzania linaloongozwa na Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa kuhakikisha fursa  zilizopo na wataalamu waliopo ndani ya Jeshi la Magereza nchini zinatumika na wanatumika  vizuri kwa manufaa ya watanzania wote sambamba na Jeshi hilo kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Tanzania inafikia uchumi wa viwanda.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini, Dr. Juma Malewa anasema baada ya upanuzi huo ambao umeanza kufanyika mapema mwezi Juni mwaka huu kiwanda hicho kitakuwa na  uwezo wa kuzalisha  jozi 400 kwa siku na hivyo kuongeza kasi ya upatikanaji wa viatu vinavyotengenezwa na Jeshi la Magereza kwa ubora kwa hali ya juu na kwa kutumia mitambo ama mashine  za kisasa.
Dk. Malewa anasema awali  kiwanda  hicho kilichopo Gereza la Karanga mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro kutokana na kutumia teknolojia ya zamani   kilikuwa na  uwezo wa kuzalisha jozi 150 kwa siku kiwango ambacho ni kidogo ukilinganisha na soko la sasa.
Anasema tayari Jeshi la Magereza limeingia Ubia na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF   kwa lengo la kupanua  shughuli za uzalishaji  wa Kiwanda  cha Viatu cha Karanga kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro sambamba na kujenga  kiwanda  kipya cha viatu katika eneo hilo hilo. 
Dk. Malewa anasema  katika kutekeleza azma yake ya ujenzi wa Kiwanda kipya  cha Viatu tayari zimetengwa ekari 20 kwa ajili ya kiwanda hicho katika eneo hilo la Karanga mjini Moshi na kwamba eneo hilo hilo litakalotumika kujenga Kiwanda  cha Viatu pia litatumika kujenga Kiwanda cha Soli na Kiwanda cha kuchakata Ngozi na kwamba Kiwanda hicho kinategemewa kukamilika mapema Julai mwaka 2018.
Katika kuinua hali ya uchumi kwa watanzania “Uzalishaji huu utaongeza ajira kwa watanzania,  lakini pia utaongeza soko la uuzaji wa viatu hivi kwa kuwa tunategemea kutengeneza viatu kwa wingi kwa ajili ya Majeshi yetu yote ya Tanzania pamoja na viatu kwa ajili ya shule za Sekondari za Serikali kwa hiyo hii ni fursa nzuri na kubwa katika Jeshi letu la Magereza”. anasema Dk. Malewa.
 Dk. Malewa anasisitiza kuwa sambamba na upanuzi wa Kiwanda  kilichopo  Gereza la Karanga  mjini Moshi  pia Jeshi la Magereza  limeanza upanuzi wa Viwanda vya Samani vilivyopo Ukonga, Arusha na Tabora ili viweze kuongeza uzalishaji wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi mbalimbali na majumbani.
Katika mwendelezo wa kupanua viwanda vyake ili viweze kuwa na tija kwa taifa na watanzania kwa ujumla kwa sasa Jeshi la Magereza nchini kwa kutumia rasilimali zake lina mpango wa kujenga Kiwanda Kikubwa cha Uzalishaji wa Samani  ambacho kitaweza kuhudumia  watanzania kwa kiwango kikubwa na tayari Serikali  imetenga  fedha  kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda hicho ambacho kitajengwa mkoani Dodoma.
“Kutokana na Serikali kuhamishia Makao Makuu ya Nchi yetu Mkoani Dodoma ni wazi kutakuwa na uhitaji mkubwa wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi na hata majumbani pia… hivyo tunategemea Jeshi la Magereza litajenga Kiwanda hiki kikubwa cha samani ili kukidhi mahitaji halisi ya samani hizo kwa watanzania wote na taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Dodoma ,’’ anasema Dk. Malewa.
Dk. Malewa anasema ili kukidhi mahitaji halisi  samani kwa ajili ya Makao Makuu ya Nchi  yetu  Jeshi la Magereza lina mpango wa kununua vifaa hususani mashine za kisasa  zitakazoweza kuzalisha  samani kwa wingi zaidi na hivyo kutosheleza  mahitaji  ya samani mjini Dodoma.
Kwa mujibu wa Dk. Malewa nguvu kazi itakayotumika katika uzalishaji kwenye kiwanda hicho itakuwa ya aina mbili ikiwemo wataalamu waliopo ndani ya Jeshi la Magereza na wananchi ambao wataajiriwa kutokana na utaalamu walio nao, hivyo Jeshi la Magereza linatarajia kuongeza fursa za ajira kwa wastani wa ajira 200 hadi 500.
 Katika kuhakikisha Jeshi la Magereza nchini linapanua wigo wa utoaji wa huduma zake kwa taifa  Jeshi la Magereza linategemea  kuingia ubia na GEPF  ili kutekeleza mradi wa upasuaji kokoto utakaofanyika mkoani Dodoma. 
Kwa mujibu wa Dk. Malewa Jeshi la Magereza linategemea kufunga mashine kubwa ya upasuaji wa kokoto ambapo kwa kiasi kikubwa inategemewa kukidhi mahitaji ya kokoto katika shughuli za ujenzi wa nyumba za wananchi hata Mashirika mbalimbali yanayohamia mkoani Dodoma.  
Dk. Malewa anasema, kwa kuwa tayari ujenzi wa nyumba za Taasisi na watu mbalimbali unaendelea  kutekelezwa  mkoani Dodoma, kupitia Mradi wa upasuaji wa Kokoto unaofanyika katika eneo la Msalato  mkoani humo, kokoto hizo zitauzwa kwa watu binafsi yaani wananchi na Serikali pia.
Dk. Malewa anasema Jeshi la Magereza ni Taasisi kubwa ambayo ina fursa nyingi za kiuchumi na endapo zitatumiwa vizuri zinaweza kuwa na mchango mkubwa kwa Taifa hili ambalo linaelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira anasema kuwa pamoja na Jeshi la Magereza nchini kutumia wataalamu wake pamoja na wafungwa ambao hufundishwa stadi mbalimbali na kutumika kama nguvu kazi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuthamini na kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazoonyeshwa na Jeshi la Magereza ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Jeshi hilo hapa nchini yanatekelezwa kama yalivyokusudiwa.
Kwa upande wake mwananchi mmoja Crispin Aloyce Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam anasema yeye ni mtumiaji na mteja mzuri wa viatu vya ngozi vinavyozalishwa na Jeshi la Magereza nchini na amekuwa akinunua viatu hivyo kwenye Duka la Magereza lililopo Mtaa wa Uhindini jijini Dar es salaam, ‘‘Ni kweli viatu vyao ni vizuri na vina ubora wa hali ya juu, ila Magereza wanapaswa kuzalisha kwa wingi viatu vya rangi ya ‘‘brown’’ ambayo watu wengi pia tunaipenda imekuwa ni kawaida mteja unapotaka viatu vya rangi ya ‘brown’ unaambiwa rangi hiyo imeisha… haiwezekani kila siku unakosa rangi hii’’ anasema Bw. Aloyce.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad