HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 28 July 2017

Benki M yasherehekea miaka 10 ya mafanikio

Benki M, nchini Tanzania inayokua kwa kasi imetimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2007.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, Jacqueline Woiso amesema kuwa benki hiyo imeendelea kukua kwa kasi katika kipindi cha miaka 10 ya uwepo wake na rasilimali zake zimefikia Trilioni moja ndani ya miaka kumi tu ilihali benki inayokaribia katika rekodi hiyo ilifikisha rasilimali zenye thamani ya Trilioni moja katika kipindi cha miaka 17. 

 “Wakati tunatimiza miaka 10 katika soko, tunachosherehekea sio idadi tu ya miaka tuliyotimiza, bali ni mafanikio makubwa tuliyofikia ambayo kila mtu amejionea. Tumeleta mapinduzi katika teknolojia ya kibenki, huduma kwa wateja, faida na kusaidia jamii” alisema.

Benki hii changa iliyoko katika benki kumi bora nchini imekuwa ikikua kwa kasi “Tumekuwa tukifanya vizuri katika masoko kwa muda mrefu na tulifanikiwa kuanza kupata faida ndani ya miaka miwili (2) tu toka kuanzishwa kwa benki yetu. Tumekuwa ni benki ambayo imefanikiwa kuwa na rekodi ya juu sana katika ukuaji kwa upande wa rasilimali na pia faida” aliongeza Bi. Woiso

Kwa upande wa huduma kwa wateja, Bi woiso alisema kuwa Benki M imekuwa ni benki ya kwanza kutoa huduma masaa 12 kila siku kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa mbili usiku, siku 7 za wiki yaani Jumapili hadi Jumapili.

Benki M ilianza kutoa huduma tarehe 27 Julai 2007 ikiwa na tawi moja lililoko barabara ya Nyerere, na baadae iliongeza matawi mengine jijini Dar es salaam, Arusha na Mwanza.Mkurugenzi mkuu wa Benki M Bi. Jacqueline Woiso akiongea katika mkutano na wandishi wa habari hapo jana jijini Dsm ambapo Benki M imetimiza miaka 10 na kupata mafanikio makubwa. Kulia ni mkuu wa idara ya mawasiliano wa Benki hiyo Bw. Allan Msalilwa.
Benki hiyo pia imekuwa ikishiriki kwa kiasi kikubwa katika kusaidia jamii ikiwa ni moja ya sera kubwa za benki hiyo ambayo huiita Money@heart, “tunashirikiana na taasisi mbalimbali katika kufanikisha miradi mingi kwenye jamii katika sekta ya Afya, Elimu, Maji Utunzaji wa mazingira na pia kuwainua wajasiriamali na wasanii wa michoro ya asili nchini”. 


Pia alisema kuwa wamefanikiwa kupata tuzo mbalimbali za kimataifa ikiwemo tuzo ya benki bora ya biashara kwa mwaka 2015 iliyotolewa katika soko la hisa la London, Benki bora katika sekta ya biashara za makampuni Afrika Mashariki, Benki bora inayoshiriki katika maendeleo ya jamii Afrika Mashariki na hivi karibuni Benki bora katika sekta ya biashara za makampuni Tanzania na Benki bora katika utoaji wa huduma kwa wateja zilitolewa na Banker Africa” alisema Woiso.

Bi Jacqueline aliongeza Benki M imeendelea kujivunia uwiano wa kijinsia kwa wafanyakazi walioajiriwa na Benki hiyo ambapo wamekuwa na uwiano wa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake mpaka sasa.

“Kwa niaba ya wafanyakazi na uongozi wa Benki M, tunapenda kuwashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuamini na kutufanya kuwa chaguo bora katika benki zinazotoa huduma kwa makampuni nchini, toka tulipoanza mwaka 2007. Tunayo furaha kuendelea kuwahudumia tutaendelea kuwapa huduma bora mnayostahili. Mafanikio yote tuliyoyapata yanatokana na wateja kama ninyi.” Alimalizia Bi. Woiso.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad