HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 19, 2017

PROF. JUMANNE MAGHEMBE AZINDUA MRADI WA UHIFADHI NA MAENDELEO YA IKOLOJIA YA PORI LA AKIBA LA SELOUS (SECAD) ULIOFADHILIWA NA SERIKALI YA UJERUMANI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na  Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari sita aina ya Land Cruiser ambayo ni sehemu ya Mradi aliouzindua wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD).
NA HAMZA TEMBA - WMU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe kwa kushirikiana na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke amezindua Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous SECAD (Selous Ecosytem Conservation and Development Program) ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, mradi huo utatekelezwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society).

Akizungumza katika hafla iliyofanyika jana, Matambwe na Tagalala Selous, Mkoani Morogoro, Waziri Maghembe alisema Serikali ya Ujerumani kupitia benki ya KFW imechangia Euro Mil. 18 (sawa na Shilingi Bil. 45.124) katika mradi huo wa miaka mitano huku mashirika ya WWF (World Wildlife Fund) na FZS (Frankfurt Zoological Society) yakichangia Euro laki 4 kila moja (sawa na Shilingi bil. 2.005) katika mradi huo. Pamoja na uzinduzi huo alizindua pia Mpango Kazi wa Dharura wa kuendeleza pori hilo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijaribu moja ya gari baada ya uzinduzi wa magari sita aina ya Land Cruiser ambayo ni sehemu ya Mradi huo.
"Mradi huu ni muhimu sana kwakua utasaidia kuongeza nguvu kwenye jitihada zetu za kuendeleza na kuimarisha hifadhi ya pori hili la Selous ikiwemo upatikanaji wa vitendea kazi muhimu pamoja na kutuongezea nguvu kwenye mapambano dhidi ya ujangili", alisema Prof. Maghembe.

Alisema jitihada ambazo Serikali imeshazifanya katika pori hilo ni pamoja na kuimarisha doria za ndege zenye rubani na zisizo na rubani (drones), kutoa mafunzo ya jeshi usu kwa askari, kuongeza maaskari pamoja na vitendea kazi ambapo katika mwaka ujao wa fedha Serikali itatoa magari mengine 15 kusaidia pori hilo.

"Pamoja na jitihada hizo tunawekeza dola za kimarekani Milioni 156 (sawa na Shilingi bilioni 349.441) kwa ajili ya kuboresha pori hili (Selous), Ruaha, Mikumi, Rungwa na Kitulo kuhakikisha watalii wanatembelea maeneo haya na kuondoa kile kikwazo cha wao kutotembelea hifadhi za kusini, hiyo inaenda sambamba na kuimarishwa kwa shirika la ndege la Serikali la Air Tanzania na kuondoa changamoto iliyokuwepo ya usafiri wa anga", alisema Prof. Maghembe. 
 Magari sita aina ya Land Cruiser yaliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kama sehemu ya mradi wa SECAD.
Akizungumzia changamoto ya ujangili katika pori hilo alisema Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo hilo ambapo majangili wengi wameshakamatwa katika maeneo ya Tunduru, Namtumbo na maeneo ya katikati ya Selous. Alisema changamoto hiyo bado ipo katika maeneo ya Mkoa wa Ruvuma ambapo imeripotiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa huo kuwa kuna upatikanaji wa silaha za kivita kutoka nchini Msumbiji ambazo zinapatikana kwa watu kubadilishana na magunia ya mchele changamoto ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.

Wakati huo huo, Prof. Maghembe akijibu swali aliloulizwa na wanahabari kuhusu hatua iliyofikiwa juu ya kauli aliyoitoa bungeni hivi karibuni ikiwa na dhamira ya kuunganisha taasisi zote za uhifadhi nchini alisema, tayari ameshaunda kamati ya watu sita ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Mweka, Prof. Japhary Kidegesho kwa ajili kuangalia namna bora ya kutekeleza azma hiyo. "Tayari kamati hiyo imeshaanza kazi na itaonana na wadau mbalimbali kupata maoni yao na katika kipindi cha mwezi na nusu watatuletea ripoti", alisema.
Kwa upande wake Balozi Konchanke alimuahakikishia Prof. Maghembe kuwa Serikali ya Ujerumani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili hifadhi hiyo ikiwemo ubovu wa miundombinu na uvamizi  pori hilo kwa faida ya jamii kwa ujumla. Aidha, alitoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zilizopo.

Meja Jenerali Gaudence Milanzi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema "Serikali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi imefanya kazi kubwa kuhakikisha Selous haiondolewi katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyopo hatarini kutoweka,  hiyo ni pamoja na kunzishwa kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyanapori Tanzania TAWA, kuanzishwa kwa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ujangili na miradi mbali ikiwemo huu wa SECAD uliozinduliwa leo ambayo kwa kiasi kikubwa imeasaidia katika kuendesha hifadhi zetu pamoja na kusaidia kwenye mapambano dhidi ya ujangili".

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, TAWA, Martin Loibooki aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa mradi huo na kusema kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika pori hilo ikiwemo ya uhaba wa vitendea kazi, miundombinu ya barabara na ujangili na hivyo kuifanya hifadhi hiyo iendelee kuwa miongoni mwa maeneo ya urithi wa dunia.

Pori la Akiba la Selous ni hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania ikiwa ukubwa wa Kilomita za mraba 50,000. Hifadhi hiyo ambayo ipo katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ina vivutio vingi vya utalii huku ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara, ujangili, rasilimali watu na vitendea kazi. 
 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akipokelewa jana katika uwanja mdogo wa ndege wa Matembwe uliopo Selous na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Loibooki (wa pili kushoto) alipowasili kwa ajili ya hafla hiyo. Nyuma yake anayeshuka kwenye ndege ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Prof. Alexander Songorwa (kushoto).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana katika kituo cha Tagalala, ndani ya Pori la Akiba la Selous Mkoani Morogoro.
Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Egon Konchanke akizungumza katika hafla hiyo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika hafla hiyo jana.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Prof. Faustin Kamuzora akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu, Hamis Semfuko akizungumza katika hafla hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Martin Loibooki akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jana, Tagalala, Selous.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akizindua Mradi wa Uhifadhi na Maendeleo wa Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD) ambao umefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika hafla iliyofanyika jana Matambwe, Selous Mkoani Morogoro. Wanaoshudia kulia kwake ni Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili, Meja Jenerali Gaudence Milanzi na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Faustin Kamuzora.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akimkabidhi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara hiyo, Prof. Alexander Songorwa Mpango Kazi wa Dharura wa Kuendeleza Pori la Akiba la Selous baada ya kuuzindua sambamba na mradi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Ikolojia ya Pori la Akiba la Selous (SECAD). Kulia kwake ni Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Faustin Kamuzora, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Martin Loibooki na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Dembe.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (kushoto) akijadiliana jambo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira Prof. Faustin Kamuzora (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu, Hamisi Semfuko (kulia).
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe (kushoto) akipokea zawadi ya picha yenye ujumbe wa Mashujaa wa Kuokoa Selous kutoka kwa Mkurugenzi wa Afrika wa WWF Ujerumani, Philipp Goltenboth (kulia). Anaeshuhudia katikati ni Mkurugenzi Mkaazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Mghembe (wa tatu kushoto), Balozi wa Ujerumani, Egon Konchanke (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakuu wa Wizara na Taasisi pamoja na washiriki wa hafla hiyo. Nyuma yao ni ziwa Tagalala ambalo ni sehemu ya kivutio cha utalii ndani ya hifadhi hiyo. 
 Baadhi ya watumishi wa Pori la Akiba la Selous wakiwa katika hafla hiyo.
Taswira mwanana ya baadhi ya Twiga ndani ya Pori la Akiba la Selous.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad