HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 20 June 2017

NAIBU WAZIRI KALEMANI AKUTANA NA WENYE NIA KUZALISHA UMEME WA UPEPO SINGIDA

Na Veronica Simba - Dodoma 
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani amekutana na Ujumbe kutoka Kampuni ya Wind East Africa, yenye nia ya kuzalisha umeme kutokana na nguvu ya upepo mkoani Singida. 
Ujumbe huo ulikutana na Naibu Waziri, hivi karibuni, Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.
Katika Kikao hicho, Naibu Waziri aliuambia Ujumbe huo kuwa, Serikali inayo dhamira ya dhati kuwezesha jitihada na miradi mbalimbali ya umeme nchini; hivyo iko tayari pia kutoa ushirikiano kwa Kampuni husika ili iweze kuzalisha umeme wa upepo mkoani Singida.
Hata hivyo, Dk. Kalemani aliutaka Ujumbe kutoka Kampuni hiyo, kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote zinazostahili, ikiwa ni pamoja na kuwajibika kwa jamii inayozunguka Mradi husika, kwa kujenga mahusiano mazuri (Corporate Social Responsibility – CSR)
Alimwagiza Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kukaa na watendaji kutoka Kampuni husika na kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria, ili Mradi uanze kutekelezwa mapema na hivyo kuwanufaisha wananchi wa Singida.
Kampuni ya Wind East Africa, imedhamiria kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa kutumia upepo, mkoani Singida.

 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani (kushoto), akiwa katika kikao na Ujumbe kutoka Kampuni ya Wind East Africa (kulia). Wengine kushoto ni maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
 Kutoka kushoto ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga, Afisa Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi John Kabadi, Afisa kutoka TANESCO, Mhandisi Amos Kaihula na Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Christopher Bitesigirwe wakiwa katika kikao cha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani na Ujumbe kutoka Kampuni ya Wind East Africa (Hawapo pichani).
Ujumbe kutoka Kampuni ya Wind East Africa, wakiwa katika kikao na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad