HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 2, 2017

MFUMO WA TAIFA WA TAKWIMU WASAIDIA KUBORESHA TAKWIMU RASMI NCHINI

Na Veronica Kazimoto,  Morogoro

Uratibu wa Mfumo wa Taifa wa Takwimu umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uzalishaji takwimu rasmi nchini.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Mpango Kabambe wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini, Philemon Mahimbo wakati wa mafunzo kwa Wanasheria wa Wizara na Taasisi za Serikali kuhusu Sheria mpya ya Takwimu No. 9 ya Mwaka 2015 yaliyofanyika leo mkoani Morogoro.

Mahimbo amesema mfumo huu unaoratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Na 9 ya mwaka 2015, umeweza kusaidia upatikanaji wa takwimu rasmi ambazo zinatumika katika kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kupunguza changamoto ya kukinzana kwa takwimu zilizokuwa zinatolewa na taasisi mbalimbali.

Kwa upande wake Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula amesema Sheria mpya ya Takwimu No. 9 ya Mwaka 2015 haimzuii mtu ama taasisi kufanya utafiti bali inamtaka mtu au taasisi kuwasiliana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupata kibali na miongozo kama anataka takwimu anazozikusanya ziwe rasmi.

“Sheria hii mpya ya Takwimu No. 9 ya Mwaka 2015 sio kwamba inazuia watu ama taasisi kuendesha shughuli za utafiti au za kukusanya takwimu kwa matumizi ya mtu binafsi au taasisi husika nchini bali inawataka kutumia miongozo kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu ili takwimu wanazozikusanya ziwe rasmi,” amesema Mangula.

Oscar Mangula amebainisha kuwa ni kosa kisheria kwa mtu ama taasisi kuendesha utafiti wenye miongozo isiyothibitishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na kuzitangaza kama takwimu rasmi.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu imepewa mamlaka kisheria ya kuratibu, kusimamia, kuchambua na kusambaza takwimu rasmi nchini.
Mratibu wa Mpango Kabambe wa Kuboresha na Kuimarisha Takwimu nchini (Tanzania Statistical Master Plan-TSMP) kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Philemon Mahimbo akiwasilisha mada wakati wa mafunzo kwa wanasheria kuhusu sheria mpya ya Takwimu ya Mwaka 2015 yaliyofanyika leo mkoani Morogoro.
Meneja wa Idara ya Mbinu za kitakwimu, Viwango na Uratibu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Emilian Karugendo akiwasilisha mada kuhusu takwimu na takwimu rasmi wakati wa mafunzo kwa wanasheria kuhusu sheria mpya ya Takwimu ya Mwaka 2015 yaliyofanyika leo mkoani Morogoro.
Baadhi ya wanasheria kutoka Wizara na taasisi za Serikali wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa mada zinazohusu sheria mpya ya Takwimu ya Mwaka 2015 wakati wa mafunzo kwa wanasheria kuhusu sheria hiyo yaliyofanyika leo mkoani Morogoro.
Baadhi ya wanasheria kutoka Wizara na taasisi za Serikali wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa mada zinazohusu sheria mpya ya Takwimu ya Mwaka 2015 wakati wa mafunzo kwa wanasheria kuhusu sheria hiyo yaliyofanyika leo mkoani Morogoro.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad