HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 22, 2017

UTT, GEPF kutoa mikopo kwa sekta isiyokuwa rasmi

Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha  ya UTT Microfinance PLC  imesaini makubaliano na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF kutoa fao la mikopo kwa wanachama wa mfuko huo ambao wanatokana na sekta isiyokuwa rasmi ili kuwawezesha kuanzisha au kuendeleza miradi ya biashara kuwaongezea vipato na kuondokana na hali duni za maisha.
Makubaliano ya utiaji saini ulifanyika Jijini Dar es Salaam kati ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw. James Washima na Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Bw. Daud Msangi ambapo makubaliano hayo yanalenga kutoa fao la mikopo kwa wanachama wa mfuko huo wanaotoka katika sekta hiyo isiyo rasmi  waweze kuanzisha au kuendeleza miradi ya biashara kuwaongezea vipato.
Bw. Washima alisema taasisi ya UTT imetenga Tsh. bilioni moja kwa ajili ya wanachama hao wa GEPF kupata fao la mikopo kwa riba nafuu ya asilimia 14 na wanalenga kuwafikia wanachama wengi wa mfuko huo hapa nchini.
“Taasisi yetu ni ya serikali na kwa kufanya hivi inatekeleza kwa vitendo dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuwawezesha wananchi kiuchumi,” kwamba kupitia fao hili la mikopo wataweza kuanzisha au kuendeleza miradi ya biashara kujiongezea kipato,aliongeza kusema ,Bw. Washima.
Alisema taasisi yao ina matawi 12 Tanzania Bara na Zanzibar na vituo 46, hivyo wamejipanga kuwafikia wanachama wote wa mfuko wa GEPF  ili waweze kunufaika na fao hilo na pia wote watakao pata fao hilo toka kwao watapata fursa ya kupata mkopo wa fao la bima ya afya.
Alifafanua kwamba wanachama wote wanaokopa katika taasisi yao wanapata fursa ya kupata mkopo wa Tsh. 76,800 kwa ajili ya kujiunga na Shirika la Taifa la Bima ya Afya (NHIF) kulingana na makubaliano ya taasisi hiyo na shirika hilo.
UTT inatoa huduma bora na nafuu za kifedha kwa watanzania wa kipato cha chini na kati na hadi kufikia sasa tayari imetoa mikopo kwa watanzania 27,000 kutoka makundi mbalimbali na sasa wameingia katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
Mkuu wa Mfuko wa Mafao ya Kustafu wa GEPF, Bw. Daud Msangi amesema mfuko huo unatoa mafao mbalimbali yakiwemo ya daka Mkwanja, Toka Kimaisha, kamata Madigrii na sasa makubaliano hayo yatawawezesha kutoa fao la mikopo kwa wanachama.
“Fao hili la mikopo limekuja katika wakati mwafaka, kwa vile lilikuwa kilio cha muda mrefu toka kwa wanachama wetu,” UTT wamefanya jambo jema kushiriki katika kutoa fao la mikopo kwa wanachama wao wanaotoka katika sekta isiyo kuwa rasmi, aliongeza kusema, Bw. Sangi.
Alieleza kuwa mfuko wa hifadhi ya jamii hauruhusiwi kutoa mkopo kwa mtu mmoja mmoja na kudai kuwa kazi hiyo ni ya benki, na wanaamini UTT itafanya kazi nzuri kwa wanachama wao.
Pia aliwasisitiza wanachama wa mfuko huo wa GEPF kuchangamkia fursa hiyo ya mikopo kwa kuwa ni nafuu kwa kila mmoja.
Alisema mikopo hiyo ni uwezeshaji utakaowasaidia kuanzisha miradi ya biashara na kupata kipato kitakacho wawezesha kuweka akiba ya baadaye katika maisha.
UTT hutoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo ya mikopo ambapo mikopo inayotolewa ni ya aina nyingi lengo kuwafikia wananchi wengi na kwa makundi mbalimbali.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha  ya UTT Microfinance PLC, Bw. James Washima kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF Bw. Daud Msangi kushoto wote waliokaa, wakisaini makubaliano ya kutoa mikopo kwa wanachama wa mfuko huo wanaotokana na sekta isiyo kuwa rasmi, kulia ni  Mkuu wa Kitengo cha Biashara na Masoko wa Taasisi hiyo, Bi. Mary Kipeja na kushoto ni Mwanasheria wa Mfuko huo,Bi. Safina Semvua.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha  ya UTT Microfinance PLC, Bw. James Washima kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF Bw. Daud Msangi kushoto Wakibadilishana nyaraka za makubaliano baada ya kutia saini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanachama wa mfuko huo wanaotokana na sekta isiyo kuwa rasmi 
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Huduma Ndogo za Fedha  ya UTT Microfinance PLC, Bw. James Washima kulia na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Mafao ya Kustaafu wa GEPF Bw. Daud Msangi kushoto wakionyesha nyaraka za makubaliano baada ya kutia saini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanachama wa mfuko huo wanaotokana na sekta isiyo kuwa rasmi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad