Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (wa pili kutoka kulia), akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani, wakati wa mafunzo maalum kuhusu usalama migodini yaliyofanyika hivi karibuni. Wengine pichani (kutoka kulia) ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania, Mhandisi Ally Samaje, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma na Fundi Sanifu Migodi kutoka Ofisi ya Madini Dar es Salaam, Stanslaus Basheka.
Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania, Mhandisi Ally Samaje, akiwasilisha mada kuhusu Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira katika Migodi ya Wachimbaji Wadogo wa Madini, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa eneo la Mererani yaliyozinduliwa rasmi hivi karibuni.
Fundi Sanifu Migodi kutoka Ofisi ya Madini Dar es Salaam, Stanslaus Basheka, akiwasilisha mada kuhusu Matumizi salama na utunzaji wa baruti migodini, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani hivi karibuni.
Ofisa wa Sheria kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Hadija Ramadhan, akiwasilisha mada kuhusu Ufafanuzi wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Ufafanuzi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2010, wakati wa mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani hivi karibuni.
Sehemu ya umati wa wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Mererani, wilayani Simanjiro, wakifuatilia mafunzo maalum kuhusu usalama migodini yaliyotolewa hivi karibuni wilayani humo.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini, eneo la Mererani, wilayani Manyara, wakiuliza maswali kwa watoa mada (hawapo pichani), wakati wa mafunzo maalum kuhusu usalama migodini, yaliyozinduliwa rasmi kitaifa wilayani humo hivi karibuni.
Na Veronica Simba
Serikali
imesema itaifungia migodi yote ya madini ambayo itapata ajali kutokana na
uzembe na haitafunguliwa hadi hapo Mkaguzi Mkuu wa Migodi atakapojiridhisha
kuwa hali ya usalama imeboreshwa na hatua stahiki za kisheria zimechukuliwa kwa
Meneja wa Mgodi au Msimamizi aliyehusika na uzembe huo.
Hayo
yalisemwa hivi karibuni na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin
Mchwampaka wakati akifungua mafunzo maalum kwa wachimbaji wadogo wa madini
nchini, kwa lengo la kuwakumbusha kuzingatia kanuni zote za usalama mahali pa
kazi ili kuepusha ajali za mara kwa mara zinazotokea na kusababisha vifo.
Mafunzo
hayo ambayo yameandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Idara yake ya
Madini, yalifunguliwa rasmi Mererani, wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara,
ambapo Kamishna Mchwampaka aliwaambia wachimbaji wadogo wa madini wa eneo hilo
kuwa, kwa sasa uchimbaji mdogo wa madini nchini umegubikwa na ajali nyingi
ambazo zinaweza kuepukika endapo tahadhari za kiusalama zitachukuliwa.
“Ajali
zinazotokea katika Migodi mingi ya wachimbaji wadogo hapa nchini, zimesababisha
vifo, vilema vya maisha na pia gharama kubwa wakati wa shughuli za uokoaji.”
Kamishna
Mchwampaka alisema kuwa, Serikali imelazimika kuchukua hatua za makusudi
kuhakikisha kuwa uchimbaji madini nchini, unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya
Madini kwa kuzingatia usalama na pia utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia
kuhusu takwimu za ajali migodini, Mhandisi Mchwampaka alifafanua kuwa, taarifa
zinaonesha kwamba kuanzia mwaka 2008 hadi mwezi Mei mwaka 2017, ajali
zilizotokea katika Migodi yenye leseni ya wachimbaji wadogo wa madini, nchini
ni 125 na wachimbaji waliopoteza maisha kutokana na ajali hizo ni 213.
Aidha,
aliongeza kuwa, ajali zilizotokea katika maeneo ya wachimbaji wadogo wasiokuwa
na leseni hususan maeneo ya mifumuko ya uchimbaji madini, katika kipindi hicho,
ni 56 na kusababisha vifo vya wachimbaji 140.
“Kwa
mwaka huu pekee, hadi kufikia tarehe 19 Mei, jumla ya ajali zilizotokea ni 11
na jumla ya wachimbaji waliofariki ni 26.”
Kamishna
Mchwampaka alisema kuwa, kutokana na takwimu hizo za ajali na vifo, Serikali
imeazimia kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa na usalama unaimarishwa katika
migodi yote ya wachimbaji wadogo nchini. Alifafanua kuwa, Wizara imepanga kutoa
mafunzo husika nchi nzima kupitia Kanda zote 10 za Madini na kwamba mafunzo
hayo yatasimamiwa na Maafisa Madini wa Kanda husika.
Akielezea
zaidi kuhusu mazingira ya ajali zinazotokea, alisema kuwa uchambuzi wa takwimu
unaonesha kuwa vyanzo vikubwa vya ajali hizo ni kuangukiwa na vifusi kutokana
na kukatika kwa ngema, kulipukiwa na baruti, kukosa hewa na kuteleza na
kuangukia mashimoni. “Hivyo, ni dhahiri kuwa ajali nyingi zingeweza kuepukika
kama tahadhari za kiusalama zingechukuliwa.”
Kamishna
Mchwampaka alitumia fursa hiyo kutoa maagizo kwa wamiliki wote wa migodi
nchini, kuhakikisha wanateua mameneja wa migodi kama Sheria ya Madini ya mwaka
2010 inavyoelekeza ambao alieleza kuwa mojawapo ya majukumu yao ya msingi ni
kusimamia usalama, afya za wachimbaji na uhifadhi wa mazingira migodini.
Alielekeza
kuwa, Meneja anapokuwa hayupo, lazima kuwe na msimamizi atakayewajibika na
kusimamia masuala husika na kwamba, ajali itakapotokea, Meneja au Msimamizi
atakuwa wa kwanza kuwajibika.
Aliwataka
Maafisa Madini wa Kanda nchi nzima, kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo
ambapo Msimamizi Mkuu wa suala hilo ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania.
Aidha,
Kamishna Mchwampaka alieleza kuwa, tayari amemwelekeza Mkaguzi Mkuu wa Migodi,
Mhandisi Ally Samaje, ambaye kwa upande wake ametoa maelekezo maalum kwa
wakaguzi wote wa Migodi nchini, kuhakikisha kuwa Migodi yote nchini inakaguliwa
ipasavyo na ile itakayobainika kuwa haina usalama, itafungwa mara moja hadi
pale marekebisho stahiki yatakapofanyika.
Kwa
upande wake, Mhandisi Samaje, akitoa mada inayohusu usalama migodini kwa
wachimbaji hao wa Mererani, alibainisha kuwa, inawezekana kuweka Migodi salama
iwapo kila mmoja kwenye Mgodi, kuanzia Meneja hadi mfanyakazi wa chini,
atajenga utamaduni wa kuheshimu sheria, kanuni na miongozo mbalimbali
inayotolewa.
Mada
nyingine zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Ufafanuzi wa Sera ya
Madini ya Mwaka 2009, Ufafanuzi wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Kanuni
zake za Mwaka 2010, Kanuni za Afya na Usalama Migodini, Matumizi salama na utunzaji
wa baruti pamoja na utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji wadogo na wa kati.
No comments:
Post a Comment