HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 5, 2017

Taa za kuongozea ndege zatandazwa uwanja wa ndege wa Dodoma, sasa kupiga kazi masaa 24

Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi wa kufunga Taa za kuongozea ndege ili kuruhusu Uwanja wa Ndege wa Dodoma kuweza kutumika masaa 24. 

Akizungumza hayo mjini Dodoma mara baada ya kukagua Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light) zilizofungwa uwanjani hapo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa uboreshaji wa uwanja huo katika kuruhusu ndege za aina zote kutua masaa 24 kwa wiki.
Muonekano wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Taa hizo zitatumika kuongozea ndege nyakati za Usiku na zina uwezo wa kuwaka masaa laki moja. 
“Hii ni hatua ya pili ya uboreshaji wa uwanja huu ambapo hatua ya kwanza tumeimaliza ya upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege (runway) hadi kufikia KM 2.5”, amesema Waziri Profesa Mbarawa. Aidha, ameongeza kuwa ufungaji wa taa hizo umegawanywa kwa hatua tatu ambapo awamu ya kwanza imekamilika kwa kujumuisha ufungaji wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), katika barabara za kuruka na kutua ndege na maeneo ya maegesho, hatua ya pili ni kufunga taa za kumsaidia Rubani kuweza kuona uwanja wote na hatua ya mwisho ni taa zitakazofungwa mita 400 kila upande uwanjani hapo.

Amefafanua kuwa Taa hizo za kisasa (Aviation Solar Powered Light) zitapunguza gharama za uendeshaji uwanjani hapo ikiwemo matengenezo yake kwani zinadumu muda mrefu. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuendelea kurefusha uwanja huo ambapo italipa fidia kwa nyumba zilizopo pembeni ya uwanja huo ili kuongeza usalama wa uwanja na ndege kwa ujumla.

“Tutaweka uzio katika uwanja huu kulingana na matakwa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na pia kupitia uzio huu taa zitakuwa salama”, amesisitiza Dkt. Chamuriho. Naye, Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), amesema mfumo wa taa hizo za kisasa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zimefungwa kwa siku 14 na zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka 12 na kuwaka kwa masaa laki moja ukilinganisha na nyingine ambazo zinawaka kwa masaa elfu kumi.

Mfumo wa uwekaji Taa za Kisasa ni mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha viwanja vyake vya ndege ili kukidhi viwango vianavyostahili katika usafiri wa anga.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), wakati alipokagua mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho na kulia ni Meneja wa Uwanja huo Julius Mlungwana.
Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), akionesha Taa za Kisasa za Umeme Jua (hazipo pichani), kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), zilizofungwa kwa ajili ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akionesha kifaa (Remote Controller) cha kuwashia Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa waandishi wa habari, wakati akikagua Taa hizo uwanjani hapo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (katikati), na Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Leonard Chimagu (kushoto), wakati alipokagua mfumo wa kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad