HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 29, 2017

PROF. JUMANNE MAGHEMBE ATEMBELEA CHUO CHA BTI TABORA

NA HAMZA TEMBA - WMU

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry kutumia fursa ya uwepo wa Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI mkoani humo kwa kuandaa utaratibu maalum utakaowawezesha wananchi hususan wafugaji wa nyuki kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji wa nyuki chuoni hapo kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa bidhaa hiyo na kuwaongezea kipato.

Waziri Maghembe ametoa kauli hiyo leo alipotembelea chuoni hapo wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tabora kwa ajili kujionea changamoto mbalimbali za uhifadhi na kuona namna kukabiliana nazo ikiwa ni ahadi aliyoitoa bungeni wakati akihitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

“Mkuu wa Mkoa, tafadhali andaa utaratibu maalum kwa wananchi wako, wale wafugaji wa nyuki wanaweza kuja kwenye chuo chetu hapa hata siku tatu, hata siku mbili, wafundishwe namna bora ya kufuga nyuki, yani watoke kabisa huko Skonge, waletwe hapa, walale hapa sku moja au mbili wafundishwe baadae warudi makwao wajue namna bora ya kufuga na kuvuna asali,” alisema Maghembe.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora alisema maelekezo hayo kwao ni faraja kwakuwa tayari kuna maelekezo ya kiserikali kusaidia makundi ya kinamama na vijana ikiwemo utoaji wa mikopo kwa vikundi vyao vya ujasiriamali.

 “Katika Mkoa wangu tuna makundi haya ya kinamama na vijana ambao tumetakiwa kuwasaidia kwa maana ya kutenga “percent” (asilimia) fulani katika “own source” (vyanzo vya ndani vya mapato), kwahiyo kwa maelekezo hayo hayo nitakachofanya mimi ni kuhakikisha kwamba tunaenda kuwaeleza katika hali ya kawaida kwamba tungeweza kuwapa mikopo lakini tungependa tuwape mikopo baada ya kupata taaluma na waweze kujua vizuri namna bora ya kufuga nyuki na kurina asali”, alisema Mwanri.

Mkuu wa Chuo hicho, Semu Daudi alisema chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 155 na kinatoa mafunzo ya Cheti na Diploma ya Ufugaji wa Nyuki.

Naye Mkuu wa Kituo kidogo cha Utafiti wa Ufugaji Nyuki chuoni hapo, Humphrey Natali alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo usafiria ambapo gari lililokuwepo limepelekwa matengenezo na kompyuta zilizopo nazo ni za muda mrefu.

Waziri Maghembe ameahidi kukipatia kituo hicho gari moja huku akimuagiza, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo kuona uwezekano wa kumaliza changamoto mbalimbali chuoni hapo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akizungumza na uongozi wa chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora BTI alipotembelea chuoni hapo leo. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho Semu Daudi na Mratibu Mkuu wa Mafunzo, Igunda John.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati akitoa maelekezo mbalimbali chuoni hapo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry baada ya kutembelea Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki, Tabora, BTI leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad