HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 29, 2017

MBAO WADAI MWAMUZI ALIWANYONGA

BAADA ya kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la FA mbele ya Simba kwa mabao 2-1, wachezaji wa Mbao FC wamemtupia lawama za waziwazi mwamuzi aliyechezesha mechi hiyo, Ahmed Kikumbo kutoka Tanga.

Juzi Jumamosi, Mbao FC ilikubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Simba katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Kilio cha Mbao kwa mwamuzi huyo wa kati ni namna alivyowazawadia penalti Simba dakika ya 118 ambayo Shiza Kichuya alifunga na kufanya matokeo kuwa 2-1 mpaka mwisho, wakidai kwamba hakukuwa na madhambi yaliyofanyika kwenye eneo la hatari.

Beki wa kulia wa timu hiyo, Boniface Maganga, amesema mwamuzi hakuwa makini kwenye uamuzi wake, kwani hakuna mchezaji aliyefanya madhambi kwa kushika mpira kwenye eneo lao la hatari kama alivyodai mwamuzi, jambo ambalo liliwatoa mchezoni.

“Ukiangalia vizuri utagundua kwamba hakuna mchezaji wetu aliyeshika, bali ulimgonga sehemu nyingine katika harakati za kuokoa hatari, lakini tukashangaa mwamuzi anaweka penalti,” alisema Maganga.

Naye kocha wa kikosi hicho, Etienne Ndayiragije, raia wa Burundi, amesema wamekubali matokeo hayo na amewapongeza wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyoifanya tangu mwanzo hadi mwisho wa michuano hiyo.

Ikumbukwe kuwa, wakati mwamuzi huyo anaamuru iwe penalti, wachezaji wa Mbao walimvaa na kutaka kumpiga mpaka askari walipoingia uwanjani na kumuokoa hali ambayo ilimfanya hadi Ndayiragije na benchi lake la ufundi kufanya kazi ya ziada ya kuwatuliza ambapo mchezo ulisimama kwa takriban dakika tatu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad