HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 24, 2017

Geita wapongeza huduma za NHIF

Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita ambapo mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya za huduma za Madaktari Bingwa. 

Na Grace Michael, Geita

Mamia ya wananchi mkoani Geita wamejitokeza kupata huduma za madaktari bingwa , mpango unaotekelezwa kwa ushiriiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mpango huo ulianza kutekelezwa siku ya Jumatatu wiki hii, katika mikoa ya Geita na Kigoma na unalenga kuwahudumia wagonjwa ambao wanahitaji huduma za kibingwa ambazo hazipo katika Hospitali hizo.

Madaktari bingwa wanaoshiriki katika mpango huo ni wa magonjwa ya watoto, mfumo wa mkojo, magonjwa ya ndani na moyo, magonjwa ya pua, masikio na koo pamoja na huduma za dawa za usingizi na huduma za wagonjwa mahututi.

Wakizungumza katika uzinduzi wa mpango huo uliofanyika katika viwanja vya hospitali ya mkoa wa Geita, wananchi waliojitokeza kupata huduma hizo wamesema ujio wa wataalamu hao umekuwa msaada mkubwa na umewaondolea usumbufu na gharama kubwa ambazo wangelazimika kuzitumia kufuata huduma hizo nje ya mkoa wao.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu na Ushauri wa Kitaalam Dk. Aifena Mramba ambaye alimwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benrard Konga , akitoa maelezo ya awali kwenye uzinduzi wa huduma hizo. 

“ … Mfuko umetenda jambo jema sana na unapaswa kupongezwa hasa kwa kuona umuhimu wa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi wengi wenye mahitaji kwa mfano mimi ni mjane hapa nilipo lakini mpango huu umeniwezesha kuwaona hawa wataalam ambao kwa hali ya kawaida nisingewaona hivyo napongeza Mfuko wa Serikali yetu inayoongozwa na Dk. Pombe John Magufuli,..” Alisema Bi. Leah Ezekiel.

Akitoa maelezo ya awali Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya , Dk. Aifena Mramba alisema kuwa kwa muda wa siku mbili za zoezi hilo katika mikioa ya Kigoma na Geita, jumla ya wagonjwa 1,204, wameonwa na kuhudumiwa na madaktari bingwa.

Alisema kuwa idadi hiyo imetoa taswira ya mahitaji ya wananchi katika huduma za kibingwa jambo linalotoa hamasa kwa Mfuko kuangalia namna ya kuendesha program hizo katika maeneo mengi zaidi.
Dk. Mramba akikabidhi Mashuka na Vifaa tiba kwa uongozi wa Mkoa wa Geita kwa ajili ya matumizi ya zoezi la Madaktari Bingwa.

“…Kwa madaktari tuliowaleta, wametuhakikishia kuwa wako tayari kufanya kazi kwa muda wowote ili wagonjwa wote waliofika kwa ajili ya mpango huo wahudumiwe na mfano mzuri jana kuna madaktari waliofanya kazi hadi saa sita usiku…” alisema Dk. Mramba.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Selestine Gesimba, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika uzinduzi wa mpango huo, ameomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuangalia namna ya kufanya huduma hizi kuwa endelevu kwa kuwa zimeonyesha mafanikio makubwa katika kuwahudumia wananchi ambao uwezo wao ni mdogo kufuata huduma mbali.

Aliviagiza vituo vya matibabu mkoani humo kuendelea kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika fursa mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili kuboresha huduma katika vituo vyao.

Aidha amewahimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii ili kujihakikishia upatikanaji wa kupata huduma kwa kuchangia kabla ya kuugua na kuepukana na usumbufu wa kutafuta fedha za matibabu wakati wanapougua.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Selestine Gesimba akihutubia wananchi waliofika katika uzinduzi huo.
Wananchi wenye uhitaji wa huduma za Kibingwa wakiwa kwenye mstari wa kuandikishwa.
Wananchi wakifuatalia hotuba ya uzinduzi wa zoezi hilo la madaktari Bingwa.
Wahudumu katika hospitali ya Mkoa wa Geita wakihesabu mashuka yaliyotolewa na NHIF.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad