HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 15 May 2017

BALOZI SEIF AFUNGUA TAMASHA LA TANO LA ZAHILFE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Tamasha la Tano la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar { ZAHILFE} kwenye Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Zanzibar Riziki Pemba Juma kulia akiteta na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Zanzibar Riziki Pemba Juma akitoa salamu za Wizara kwenye Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Michezo na Serikali walioshuhudia ufunguzi wa Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani.
Kutoka Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar {BTMZ}, Mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi Ayoub Mohamed Mahmoud na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas.
Balozi Seif akisalimiana na wachezi wa Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA} waliopambana na Mabingwa watetezi wa Kombe la ZAHILFE Timu ya ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu.
Mabingwa watetezi wa Kombe la ZAHILFE Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu { ZU} wakisalimiana na Balozi Seif ambae ni mgeni rasmi kwenye pambano lao dhidi ya Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA}
 Mashabiki wa Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu { ZU} wakishangiria kwa kujiamini wakati Timu yao ilipotoa kichapo cha Paka mwizi cha Goli 4 kwa Bila dhidi ya Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya juu Zanzibar { ZAHILFE} Timu ya Soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu {Zanzibar University - ZU} jana ilidhihirisha ubabe wake baada ya kuitandika bila ya huruma Timu ya soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA} Magoli 4-0.


Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua kwa muda wote wa dakika 90 ulifungua pazia la mashindao ya Tamasha la Michezo la Shirikisho hilo uliorindima ndani ya Uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Watetezi hao ZU walionyesha dalili za mapema za ushindi wa mchezo huo licha ya kuwa mpaka wanakwenda mapumziko hakukuwa na timu iliyoona mlango wa mwezake huku washabiki wa Timu zote mbili wakishindwa kukaa kwenye majukwa ya uwanja huo.

Kipindi cha pili kilianza kwa mikiki mikiki kwa timu zote mbili lakini uzoefu na utaalamu wa Timu ya ZU ukajidhihirisha pale wanandinga hao walipoanza kumimina karamu ya Magoli ndani ya kimia cha MNMA na hadi mwisho wa mchezo huo ZU 4 na MNMA 0.

Akiizindua michezo hiyo ya Tamasha la Tano la Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} tokea kuanzishwa kwake Mwaka 2013 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema utunzwaji wa vipaji vinavyoibuliwa ndani ya mashindao hayo lazima uendelezwe ili kupata wanamichezo bora watakakidhi kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.

Balozi Seif alisema mashindano ya Tamasha la Shirikisho la Zahilfe ni mwanzo wa kuelekea njia sahihi ya kupata vipaji hivyo sambamba na kuchangamsha akili za Wanafunzi katika kukabiliana vyema na masomo yao ya kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Sera ya Michezo Zanzibar ya Mwaka 2007 imeweka umuhimu wa kuimarisha Sekta ya Michezo Vyuoni na Maskulini Unguja na Pemba.

Alisema Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} kupitia Sera hiyo kimeanzisha mafunzo maalum yalaiyowezesha kutoa Wahitimu 9 wa Stashahada ya Michezo ambao tayari wameanza kusomesha katika maskuli mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alihimiza umuhimu wa kuimarishwa michezo Maskulini na Vyuoni kwa vile inasaidia kupatikana kwa matokeo mazuri ya Wanafunzi hasa kwenye mitihani yao pamoja na kuimarika kwa nidhamu miongoni mwa wanafunzi na walimu wao.

Alisema nidhamu inamuwezesha mtu sio mwanafunzi pekee kufanya kazi zake kwa mipango maalum na akafarajika na utaratibu wa kuanzishwa kwa mashindano ya Zahilfe yatakayofungua njia sahihi ya kudumisha nidhamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar kwa jitihada za watendaji wake kuwaweka pamoja Wanamichezo hapa Nchini.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pemba Juma ameipongeza Benki ya Biashara ya NMB kwa moyo wa kizalendo wa kuamua kwa makusudi kusaidia Sekta ya Elimi Visiwani Zanzibar.

Waziri Riziki alisema Benki ya NMB mbali ya kusaidia Sekta ya Michezo lakini pia juhudi zake za kusaidia Kompyuta 50 pamoja na Vikalio 450 kwa Skuli za Zanzibar ni ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba Uongozi wa Benki hiyo unaendelea kujali umuhimu wa Sekta ya Elimu inayofinyanga wataalamu wa fani zote.

“ Benki ya NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Sekta ya Elimu Nchini, mbali ya kusaidia michezo lakini pia kuongeza nguvu zake katika kupunguza uhaba wa Vikavio na vifaa muhimu maskulini kama Kompyuta”. Alisema Waziri wa Elimu Zanzibar.

Akitoa salamu katika uzinduzi huo wa Tamasha la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} Afisa Mkuu Wateja wadogo wadogo na wa kati pamoja uendeshaji Matawi ya Benki ya NMB Bwana Abdulmajid Nsekela alisema Taasisi hiyo ya kifedha itaendelea kusaidia huduma za Kijamii kadri mapato ya makusanyo yake yanavyoongezeka.

Bwana Nsekela alisema wadau wakuu wa Taasisi hiyo wengi wao ni Wananchi, hivyo hakuna budi wala kigugumizi kwa Uongozi wa Benki hiyo kuzipa kisogo changamoto zinazowakabili Wananchi hao katika maeneo yao wanayoishi.

Hilo ni Tamasha la Tano la Michezo inayoandaliwa na Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2013.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
15/5/2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad