HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 10 April 2017

MVUA YAHARIBU MIUNDOMBINU YA BARABARA YA VIGWAZA, BUYUNI MPAKA MWAVI, MBUNGE WA CHALINZE AAHIDI KUSIMAMIA KERO HIYO

Baadhi ya wananchi wanaotumia barabara ya Vigwaza, Buyuni na Mwavi wakipita kwa shida katika barabara hiyo iliyoharibika vibaya kutokana na mvua.

Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze

MVUA kubwa iliyoambata na upepo mkali, imekata mawasiliano ya miundombinu ya barabara eneo la Buyuni na kusababisha wakazi kutoka kata ya Vigwaza na Mwavi jimbo la Chalinze, kupata shida. Hali hiyo inasababisha wakazi hao, kuvushwa kwa kupata msaada wa kubebwa mgongoni na shingoni kwa gharama ya sh. 3, 000 na 2, 000 na pikipiki kupitishwa kwa sh. 5, 000 huku magari yakishindwa kupita kabisa.

Baadhi ya wakazi hao akiwemo Zaina Zuberi aliekuwa akienda Mwavi, alisema wapo katika hali ngumu. “Mvua hapa bado haijanyesha, maji haya yanatokea maeneo ya Msoga huko na kufika huku daraja la Mbiki, Buyuni na kukatiza katika hii barabara, sipati picha mvua ikipiga hapa kwa mwezi huu”

“Barabara ni mbovu kama mnavyojionea, haipitiki, watu tunapata shida kufuata mahitaji ya nyumbani tatizo ni mkandarasi, barabara imejengwa bila kuwekwa makaravati, kila akielekezwa kujenga kutokana na hali halisi ya barabara haiwi hivyo,” Nao baadhi ya vijana wanaosaidia kuwavusha watu na pikipiki akiwemo Rashid Juma, alisema tangu mvua ziharibu eneo hilo aprili 7 wanavusha watu kwa maelewano kulingana na uwezo wa mtu.
Mkazi wa Mwavi ,Zainab Zuberi akivushwa kwenye maji yaliyokata barabara eneo la Buyuni,kwa kubembwa shingoni .

“Tunapata fedha kulingana na kichwa cha mtu au pikipiki, kila mtu mmoja 3,000 au 2,000 na pikipiki 5,000 “alieleza. Aidha kutokana na mvua hizo, zimeathiri pia barabara nyingine ya kutoka Milo-Kitonga hadi Vigwaza.

Mbunge wa jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alitembelea barabara hizo na kujionea hali halisi. Ridhiwani alisema, hali iliyopo hairidhishi na kuwapa wakati mgumu wakazi wa maeneo hayo na ameahidi kuisimamia kero hiyo kwa kuifikisha bungeni na halmashauri ya wilaya ya Chalinze ili lifanyiwe kazi.

Alieleza kuna kila sababu ya mkandarasi kufanya kazi kulingana na uhalisia wa eneo husika hali inayosababisha wananchi kupata tabu na barabara kuharibika kila wakati. Katika hatua nyingine Ridhiwani aliunga mkono juhudi za ujenzi wa darasa lililobomoka kutokana na mvua iliyonyesha aprili 7 ambapo amechangia kiasi cha sh.100, 000, mabati 50, mifuko ya saruji 50 na nondo 20.
Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete (kushoto) akiangalia barabara kutoka Vigwaza-Mwavi iliyoharibika vibaya katika eneo la Buyuni hali inayosababisha magari kushindwa kupita.

Alibainisha kwamba shule hiyo imejengwa miaka 40 iliyopita hivyo miundombinu yake pia imechakaa. Ridhiwani alisema kuna kila sababu ya kuangalia namna ya kukarabati shule hiyo kwani majengo yake yamejengwa miaka mingi.

Afisa mtendaji wa Kidogozero, Lilian Mbwa alisema kila kaya itachangia matofali mawili na kila mjumbe wa serikali ya kijiji ni tofali 10. Hata hivyo alisema halmashauri ya kijiji itachangia jumla matofali 200 na wadau wa maendeleo matofali 300.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kaya zaidi ya 20 zimekosa makazi ya kuishi na nyumba zaidi ya 90 ziliharibika, kubomoka na nyingine kuezuliwa mapaa huko jimbo la Chalinze, kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali. Maeneo yaliyokumbwa na adha hiyo ni Chalinze Mzee, Bwawa la umwangiliaji la Msoga ambalo limetoboka, Msoga na shule ya Sekondari ya Imperial.

Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete,akizungumzia kero ya kuharibika kwa baadhi ya miundombinu ya barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha,ambapo mvua iliyonyesha april 7 na 8 imesababisha kuharibu barabara ya Vigwaza-Buyuni-Mwavi na ya Milo-Kitonga-Ruvu.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad