HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 18 April 2017

KISHAPU WILAYA YENYE FURSA LUKUKI ZA UWEKEZAJI

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza katika moja ya vikao. Wengine pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Stephen Magoiga na Mwanasheria wa wilaya, Wilson Nyamunda.
Mmoja wa mafundi wa bidhaa za ngozi katika kiwanda kidogo cha Badimi akiwajibika. 
Sehemu ya mifugo ambayo ni muhimu kwa uwekezaji wa viwanda vya bidhaa za ngozi wilayani Kishapu.

Serikali ya Awamu ya Tano iko katika mkakati wake kabambe wa kuhakikisha kuwa Sera ya Tanzania yenye viwanda inafanikiwa, lengo kubwa likiwa ni kukuza na kuinua uchumi wa nchi.
Yote hayo yanafanyika kwa kufufua viwanda mbalimbali ambavyo vilikuwa vimekufa na kusitisha uzalishaji wake kutokana na sababu mbalimbali hatua inayokwenda sanjari na kujenga vipya.
Tunashuhudia juhudi kubwa za Serikali zikizaa matunda katika maeneo kadhaa ya taifa letu ambayo tayari wawekezaji wameanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali. 
Katika kudhihirisha hilo, pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inayoongozwa na Waziri Charles Mwijage imejikita katika kuwezesha wajasiriamali ili wainuke na kutambulika katika soko la kitaifa na kimataifa.
Hilo linafanyika kupitia maonesho mbalimbali ya viwanda na biashara ambayo hufanyika kila mwaka lengo ni kuwapa fursa wajasiriamali hao kuonesha bidhaa zao haijalishi kama ni kubwa au ndogondogo. 
Katika hilo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu iliyopo katika Mkoa wa Shinyanga magharibi mwa Tanzania haiko nyuma kwani tayari imeanza utekelezaji wa sera hiyo muhimu kwa ustawi wa nchi.
Wilaya hiyo kupitia kikundi cha Badimi inajivunia kuwa na kiwanda kidogo cha kusindika na kutengeneza bidhaa za ngozi za wanyama zikiwemo viatu, mikoba na mikanda.
Tayari wakazi wa Kishapu wameanza kuona matunda ya kiwanda hicho kidogo ambacho kinatarajiwa kuwa nia mojawapo ya kujipatia maendeleo siyo tu ya kikundi bali pia kwa taifa.
 “Dhamira yetu ni kutengeneza ajira kwa wanakikundi, kuwezesha fursa za kiuchumi miongoni mwa wanakikundi na wananchi kwa ujumla waliomo ndani na nje ya Wilaya ya Kishapu,” ndivyo anavyobainisha Said Luhende ambaye ni katibu wa kikundi hicho.
Akifafanua zaidi anasema neno Badimi likiwa linamaanisha kundi la wafugaji ambao ni walinzi na wachungaji mifugo iliundwa Novemba 11, 2009 ikiwa na wanachama waanzilishi 10.
Kikundi hicho ambacho kina jumla ya wanachama 53 ambapo 27 kati yao ni wanaume na 26 ni wanawake, walianza kuuziana hisa, kusindika ngozi na kuogesha mifugo shughuli walizoendelea nazo hadi kufikia hatua ya kutengeneza bidhaa za ngozi.  
Katibu huyo wa kikundi hicho anaendelea kudokeza kuwa malengo hasa ya mradi au kiwanda hicho kidogo ni kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi ghafi ndani na nje ya wilaya hiyo.
Idara ya Mifugo na Uvuvi ambayo inaongozwa na Mkuu wake, Dk. Alphonce Bagambabyaki akishirikiana na wataalamu wake walioenea kata mbalimbali ndiyo wenye dhamana ya masuala yote ya bidhaa za ngozi za mifugo mbalimbali.
Wilaya ya Kishapu ina idadi kubwa ya mifugo kwa ujumla na ni kweli kuwa zao la ngozi litokanalo na mifugo halithaminiwi kwa kiwango kinacholingana na thamani yake.
Kupitia idara hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inahakikisha inalifanya zao hilo la bidhaa za ngozi liwe linatambulika na kuwa na thamani kubwa kwa mfugaji wa mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Kwa mujibu wa takwimu kwa wastani jumla ya ngozi za wanyama kama ng’ombe 350, za mbuzi 800 na kondoo 280 huweza kupatikana kwa kila mwezi ambazo zinaweza kusaidia utengenezaji wa bidhaa za kutosha. 
Baadhi ya ngozi ambazo zimekuwa zikitupwa kutokana na kukosa soko sasa zitakuwa zinaokolewa na wakati huo mfugaji kwa uapnde wake atakuwa anapata faida kubwa kwa kujipatia kipato kutokana na mauzo ya ngozi ghafi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Nyabaganga Taraba kwa upande wake anatoa pongezi za dhati kwa kikundi hicho cha wajasiriamali cha Badimi na kusema kuwa Kishapu ya viwanda inawezekana.
“Mara zote mwanzo huwa ni mgumu na mara nyingi huwa tunapenda kushiriki pale ambapo tunaona matunda ya jitihada fulani yanatokea lakini hatupendi kuonesha ushirikiano tangu mwanzo, hivyo sasa tufike mahali tutiane moyo,” anasisitiza
Anawakaribisha Watanzania wanohitaji kujenga viwanda wafike wilayani humo ili kuwekeza viwanda hatua itakayosaidia kuzidi kujenga uchumi imara na kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa ajira.
Taraba anaendelea kusema kuwa yapo maeneo yaliyopimwa yakiwemo Mwigumbi kwenye kata ya Bubiki ambayo yamekaa kibiashara na kimkakati hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha biashara.

Kwanini Mwigumbi?
Hili ni eneo ambalo kimsingi ni njia panda ya karibu zaidi ya kwenda nchi jirani ya Kenya kwa barabara ambayo huweza kurahisisha usafiri wa magari makubwa kama malori kusafirisha bidhaa.
Si hivyo tu bali pia ni njia panda ya kwenda mikoa jirani kama Simiyu, Mara, Manyara na Arusha hivyo kuwa kitovu kizuri cha biashara hali inayoweza kufanya mzunguko mkubwa wa fedha wilayani Kishapu.
Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli alizindua mradi wa ujenzi wa barabara kuu ambayo itaunganisha Mkoa wa Shinyanga na Simiyu hatua itakayorahisha na kupunguza usafirishaji kwenda Kenya.  
Itakumbukwa pia Mwigumbi ni eneo ambalo linatarajiwa kupitiwa na reli ya kasi ya ‘standard garge’ hivyo mkuu huyo wa wilaya anawakaribisha wawekezaji kujenga bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya maeneo ya jirani. 

Maeneo mengine ya uwekezaji 
Mbali ya Mwigumbi, Taraba anabainisha wilaya hiyo imejaliwa maeneo mengine ya uwekezaji kama mji mdogo wa Kishapu na mengine yakiwemo Nyasamba kwenye kata ya Bubiki, Mipa kata ya Mondo, Uchunga, Ukenyenge, Bunambiyu pamoja na Igaga.  
Pamba ndilo zao kuu la biashara linalotambulika katika wilaya hiyo lakini ukweli ni kuwa yapo mazao mengine yanayofanya vizuri na kuwainua wakulima yakiwemo mkonge, alizeti na dengu.
Anaagiza kila kata kubainisha fusra zisizopungua tatu ambazo wanaona kutokana na mazingira yanayowazunguka na kutoa rasilimali watu zinaweza kuchangia uanzishwaji wa viwanda.
Anasema lengo ni kuzitambua fursa hizo na hivyo kuanza michakato mapema ya kujenga viwanda wenyewe bila kutegemea wawekezaji kutoka nje kufika Kishapu na kuvijenga. 
Mkuu wa wilaya anawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika mazao hayo kwa kujenga viwanda kwa ajili ya kukamua alizeti kupata mafuta ya kupikia, kusindika mkonge na kutengeneza bidhaa mbalimbali pamoja na sabuni.
Anasema pamoja na hayo ni dhahiri kuwa viwanda havitajengwa na watu wa nje bali vitajengwa na wananchi wazawa kwa kutumia malighafi zinazopatikana ndani katika maeneo wanayoishi.
Kwa kutumia wananchi waliomo ndani wenye ujuzi tofauti tofauti au waliosomea katika vyuo mbalimbali na kupata mafunzo au wenye kuwa na ubunifu ambao unaweza kuleta mapinduzi ya viwanda.
Hivyo Kishapu ya viwanda inawezekana jambo muhimu ni wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kuendelea kujenga uchumi imara kama ilivyo kaulimbiu ya halmashauri ya wilaya hiyo. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad