HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 29 March 2017

WATUHUMIWA WA MAKONTENA WAPANDISHWA MAHAKAMANI

Watuhumiwa Sultan Ibrahimu kulia na Ramadhani Hamisi wakijiandaa kushuka kutoka kizimbani Mara baada ya kesi yao ya kuingiza magari kwa kificho na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya milioni 287.8 kuahirishishwa

Na Karama Kenyunko, blogu ya Jamii.
Wafanyabiashara watatu akiwemo raia wa Zambia mmoja  wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za uhujumi uchumi ikiwemo kusafirisha bidhaa kwa  kificho

Washtakiwa hao ambao wamefikishwa mbele ya Mahakimu wawili tofauti ni Sultani Ibrahimu, (36), mwarabu Mkazi wa Usalama Temeke, Augustino Kalumba (39) raia wa Zambia na Ramadhani Hamisi maarufu kama Ukwaju (48) anaishi Kinondoni Hananasifu.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na sheria ya Umoja wa nchi za Afrika Mashariki ya kudhibiti ushuru.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba washtakiwa Sultan Ibrahimu na Augustino Kalumba wamesomewa mashtaka matatu, la kula njama,  kusafirisha Mali iliyofichwa na kuitia hasara serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania zaidi ya  shilingi milioni 287.8.
Mwendesha mashtaka Nassoro Katuga akisaidiana na Wakili Batlida Mushi amedai kuwa kati ya Decemba 1 mwaka jana na Machi 1 mwaka huu katika eneo lisilojulikana washtakiwa hao wakiwa na wenzao ambao bado hawajakamatwa walikula njama ya kusafirisha mali.
Katika shtaka la pili imedaiwa kuwa kati ya Decemba 1 hadi 31, mwaka jana katika makao makuu ya Bandari ya Tanzania yaliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam washtakiwa waliingiza magari matatu ambayo ni Range Rover sports, Zenye naomba tofauti tofauti.
Imedaiwa kuwa magari hayo yalikuwa yamepakiwa pamoja na nguo za mitumba na viatu kwenye kontena namba MSKU 9914168 kwa nia ya kuwadanganya maafisa wa ushuru.
Aidha washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuingiza Mali hizo wakiwa wamezificha na kuisababishia serikali ya Tanzania kuingia hasara zaidi ya shilingi 287.8
Mbele ya Hakimu Respicious Mwijage washtakiwa Sultan Ibrahim na Ramadhani Hamis wamesomewa mashtaka matatu.
Imedaiwa kuwa kati ya Decemba Mosi mwaka jana na March 4 mwaka huu jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la Kuficha Mzigo wakati wakiuingiza nchini.
 Imeendelea kudaiwa kuwa, kwa pamoja washtakiwa hao waliingiza Mzigo wa magari matatu wakiwa wameyaficha ili kuweza kuwaficha maafisa ushuru.
Wakili Katuga amedai kuwa kitendo hicho kimeikosesha serikali ya Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania mapato zaidi ya shilingi milioni 190.9
Hata hivyo washtakiwa hao hawakuruhisiwa kujibu kitu chochote na wamerudishwa rumande kwa kuwa mashtaka dhidi yao yako chini ya sheria ya uhujumu uchumi ambayo Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kutoa dhamana.Aidha Wakili Katuga aliiarifu mahakama kuwa DPP bado hajatoa kibali kwa mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo.

Kesi hiyo itatajwa mahakamani hapo Aprili 12 mwaka huu. Upelelezi bado haujakamilika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad