HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 13 March 2017

Kasisi ashika nafasi ya Mokiwa

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dk Jacob Chimeledya (katikati) akizungumza na waandishi Dar es Salaam baada ya Ibada ya kutwaa Dayosisi ya Dar es Salaam na kumtangaza Kaimu Kasisi Mkuu, Jerome Napella (hayupo pichani), kuongoza Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam. Wengine ni Makamu Askofu Mkuu Oscar Mnunga (kushoto) na Askofu, Julius Lugendo wa Mbeya. (Picha na Yusuf Badi)

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Jackob Chimeledya amemtangaza Jerome Napela kuwa Kasisi Kiongozi wa Dayosisi ya Dar es Salaam ambaye atafanya shughuli za kiteundaji hadi hapo atakapopatikana askofu mpya wa dayosisi hiyo.
Uamuzi huo unatokana na kuondolewa madarakani aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa pamoja na msaidizi wake John Mlekano.
Shughuli za uaskofu wa dayosisi ya Dar es Salaam zinafanywa na Dk Chimeledya mwenyewe.
Dk Chimeldya alitangaza uamuzi huo katika ibada iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi katika Kanisa la Mtakatifu Albano, Dar es Salaam; huku baadhi ya waumini wakiweka ulinzi getini na kuwazuia wasiingie mapadiri wote ambao wamekuwa wanamuunga mkono Askofu Mokiwa ambaye ameondolewa madarakani.
“Natangaza rasmi kuwa dayosisi hii itakuwa chini ya uangalizi wa Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania ambaye ni mimi mwenyewe. Pia natangaza kumteua Vicar General mpya Jerome Napela.Huyu ndiye atasimamia shughuli za kila siku za dayosisi hii,” alisema Dk Chimeledya.
Dk Chimeledya alisema kuanzia leo ataongoza vikao vya kumtafuta askofu mpya wa Dayosisi ya Dar es Salaam ambaye ndiye atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk Mokiwa.
“Tumeanza safari ya kumtafuta askofu mpya, hivyo kuanzia kesho (leo) tufanya kikao na mapadri, wainjilisti, mashemasi na wafanyakazi wote wa ofisi yetu kuu hapa kanisani. Naomba wahusika wote wafike bila kukosa,” alisema Dk Chimeledya.
Dk Chimeledya pa alitangaza kutengua uteuzi wa wakuu wa makanisa wa wilaya (Achidikini) wa wilaya za Mtakatifu Albano, Temeke, Kinondoni, Kibaha na Ilala ambao walikuwa wameteuliwa na Askofu Mokiwa. “Natengua uteuzi wao hadi hapo nitakapoteua wengine,” alieleza.
Alisisitiza kuwa suala la Askofu Mokiwa limeshamalizika kwani sio askofu tena wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa hatua alizozichukua yeye kama askofu mkuu wa kufanya naye kikao na kumwomba ajiuzulu akagoma na barua aliyompa ya kumwachisha kazi zilizingatia katiba ya kanisa hilo.
“Tuache kuendelea na malumbano juu ya suala hilo, yale tuliyoyafanya yalipitia mchakato wa kikatiba, msidanywe na mtu kwamba maamuzi yale yatapelekwa tena kwenye nyumba ya maaskofu, hilo halipo na hakuna kipengele hicho kwenye katiba yetu,” alisema Dk Chimeledya.
Alisema kitendo kilichofanywa na Dk Mokiwa baada ya kupokea barua zile kumkashifu askofu mkuu na kutoa matusi dhidi ya uamuzi ule ni jambo la kusikitisha.
Hata hivyo alisisitiza kuwa katiba inampa fursa askofu mkuu kufanya maamuzi bila kuingiliwa na mamlalaka yoyote ila baada ya kufuata hatua zote zinazotakiwa.
Awaamuru mapadiri kutii agizo Aliwataka mapadiri kurudi makanisani mwao wakafanye kazi ya Mungu na watu waliopewa, waachane na makundi yanayoendelea huko aliyodai ni ya kuvuruga amani.
Alisema baada ya uteuzi huo aliofanya chochote kitakachofanywa kinyume na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo watashughulikiwa na mamlaka za kiserikali.
“Niwaombe hawa ninaowaweka ndio uongozi halali, niwaombe watu wa Mungu uongozi huu tunaouweka ndio uongozi halali. Uongozi wa halali haupo tena, hivyo Vicor General ndiye atahusika na mambo yote ya kila siku ya uendeshaji wa dayosisi kwa kushauriana na mimi. Dk Chimeledya alisema kila atakachofanya Kasisi huyo mkuu lazima atashauriana na yeye.
Alisema huyo atakuwepo kwa ajili ya mambo yote ya uendeshaji wa dayosisi hiyo Alisema katika kipindi hiki cha mpito baadhi ya mapadiri na waumini wengine huwa wanazuia matoleo ya sadaka yasiende ofisi kuu. Alionya kuwa hakuna wa kuzuia sadaka za waumini zisienda ofisi kuu, alisema kila kitu kitaenda vizuri.
Askofu mkuu huyo alisisitiza kuwa atakayejaribu kuzuia matoleo hayo atakuwa anavunja sheria za nchi na atachukuliwa hatua kwani atakuwa anafanya wizi. Alisema askofu msaidizi aliyewekwa pia atafanya matumizi ya fedha za kanisa kwa kushauriana na yeye askofu mkuu.
Pigo lingine kwa Dk Mokiwa Katika hotuba yake, Dk Chimeledya alisema Askofu Mokiwa sio tena mdhamini wa kanisa hilo kwa sababu amepoteza sifa hiyo baada ya kuvuliwa uaskofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam.
“Dk Valentino Mokiwa sio mdhamini tena wa Kanisa Anglikana kupitia Dayosisi ya Dar es Salaam. Hata Rita kule wameshamwondoa kwenye orodha ya wadhamini,” alieleza.
Aliongeza kuwa mdhamini wa Kanisa la Angilikana, sifa mojawapo lazima uwe askofu wa dayosisi, sifa ambayo Dk Mokiwa hana tena.
Amrejeshea ukasisi Jaji Ramadhani Askofu Mkuu huyo alisema Jaji Augustine Ramadhani anayo mahusiano ya karibu na Dayosisi ya Mpwapwa kwani ndiko alikokulia na kuanzia shule huko; kwa heshima hiyo Dayosisi ya Mpwapwa imempa leseni ya kuendelea kuwa kasisi wa kanisa hilo.
“Kwa kuwa sisi ndio wasimamizi wa Dayosisi hii ya Dar es Salaam, basi tunamtuma aendelee kuhudumu katika kanisa hili la St Albano kama alivyokuwa ananya wakati wote. Na kwa kuwa anayo leseni ya ukasisi, sasa ataweza kutumika sehemu yoyote ile katika Kanisa la Anglikana Tanzania.”
Mapadri watano wazuiwa Kutokana na ulinzi mkali waliouweka waumini hao, mapadri watano walizuiwa kuingia kwenye milango ya kanisa hilo.
Waliozuiwa ni Padri wa Muhimbili, Alex Apiyo ambaye polisi walimkamata na kuondoka naye baada ya kutotii amri ya kumtaka asiingie ndani.
Wengine ni Padiri aliyetajwa kwa jina moja la Mbulinyingi wa Kinondoni, Zinge wa Kibamba, Padri Cosmus Mhina wa Kibamba.
Wengine ni Padri Julius Kiondo wa Tegeta na Jackob Ngalomba wa Mbagala ambao waliomba msamaha na kuruhusiwa kuingia, lakini kwa sharti la kutovaa mavazi ya kipadri na wakae kwa waumini na sio kwenye eneo ambalo walitengewa mapadri kukaa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad