HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 4 February 2017

SERIKALI YATOLEA UFAFANUZI MADAI YA WALIMU NA RIBA KUBWA KATIKA MABENKI

Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu kero mbalimbali za Wabunge ikiwemo kuhusu maslahi ya walimu nchini na kadhia ya riba kubwa katika mabenki. Ufafanuzi huo umetolewa leo wakati wa vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini hapa.

Stahili za Walimu
Serikali imesema kuwa ni kweli inadaiwa na walimu madeni yasiyo ya mishahara yanayofikia  shilingi 26,042,581,697 hadi kufikia Desemba,2016. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo amesema deni hilo litaanza kulipwa hivi karibuni kwa kuwa deni hilo lote limeshahakikiwa.

Kuhusu madeni ya mishahara, Naibu Waziri Jafo ameliambia Bunge kuwa uhakiki wa deni la shilingi 10,034,495,540 umekamilika na kinachosubiriwa ni kulipwa kupitia akaunti ya mtumishi anayedai. Ameongeza kuwa, deni linalobaki ni shilingi 8,067,922,773 ambalo linaendelea kuhakikiwa ili nalo liweze kulipwa.

Upungufu wa Vyumba vya Madarasa na Maabara
Akijibu hoja kuhusu mkakati wa Serikali wa kupunguza tatizo la vyumba vya madarasa na maabara, Naibu Waziri Jafo amesema kuwa, Serikali katika bajeti ya mwaka 2016/17 imetenga jumla shilingi bilioni 29.3 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,306 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 16.3 zimetengwa kujenga vyumba vya madarasa 1,047 kwa shule za sekondari.

Ameliambia Bunge kuwa utekelezaji wa malengo hayo pia utafanywa kupitia Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES II) ambako pia zimetengwa shilingi bilioni 23.6 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba 1,642. Upande wa maabara Serikali imetenga shilingi bilioni 18.9 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba 2,135.

Kumuinua Mwanamke Kiuchumi
Serikali imesema kuwa hadi kufikia Desemba, 2016 Benki ya Wanawake imeshafungua matawi katika mikoa saba (7) ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma ambapo huduma mbalimbali za kuwainua akina mama kiuchumi zimetolewa. Katika huduma hizo, dirisha la kuhudumia maeneo ya Iringa na Makambako pekee hadi kufikia Desemba, 2016 jumla ya Wajasiliamali 6,850, wanawake 5,350 na wanaume 1,500 walipatiwa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangalla ambapo aliongeza kuwa Benki hiyo imefungua vituo vya kutolea mikopo 252 kufikia Desemba 2016.

Riba Kubwa katika Mabenki
Serikali imesema kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) haiwezi kuweka ukomo wa riba za mabenki kwani si tu inapingana na jukumu lake la msingi la kusimamia mabenki, bali pia hilo liinapingana na mfumo wa uchumi wa soko huria. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Dkt. Ashatu Kijaji ametoa kauli hiyo wakati akijibu hoja inayohusu uwepo wa riba kubwa katika mabenki.

Dkt.Kijaji ameeleza kuwa, suala la Benki Kuu kutoa maelekezo kwa mabenki kutumia viwango fulani vya riba katika biashara zao, kutaifanya Benki Kuu kukosa nguvu na mamlaka ya kuyachukulia mabenki hatua endapo yatapata hasara kwa kutumia riba ambayo Benki Kuu imeelekeza. “Benki Kuu haina mamlaka kisheria ya kuweka ukomo wa riba au riba elekezi itakayotumiwa na mabenki katika kutoa mikopo,” alisema.

Hali ya Kituo cha Biashara cha Taifa Nchini Uingereza
Serikali imesema kuwa imekifunga rasmi Kituo cha Biashara cha Taifa kilichopo mjini London, Uingereza kutokana na changamoto mbalimbali za kituo hicho ikiwemo ufinyu wa bajeti pamoja na upungufu wa rasilimali watu.

Akijibu hoja hiyo Bungeni leo kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema, badala yake, shughuli zote za kituo hicho zimehamishiwa Ubalozi wa Tanzania uliopo mjini London.


Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad