Mtaa Kwa Mtaa Blog

PROF. MBARAWA AKAGUA UJENZI FLY OVER YA TAZARA.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa kampuni ya Sumitomo Mitsui Eng. K Tsuji, anayejenga barabara ya juu (TAZARA fly over) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es salaam.
 Mkandarasi wa kampuni ya Sumitomo Mitsui Eng. Mitsui Eng. K Tsuji, (Wa pili kulia) akifafanua jambo kuhusu ramani ya ujenzi wa barabara ya juu (TAZARA fly over) kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Wa tatu kulia) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi huo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (Katikati), akikagua maendeleo ya Ujenzi wa barabara ya juu (TAZARA fly over), jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akisalimiana na baadhi ya mafundi wanaojenga barabara ya juu (TAZARA fly over), jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano


 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui anayejenga barabara ya juu (Fly over) ya Tazara kuongeza kasi ya ujenzi huo ili  kupunguza muda wa ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza katika eneo la ujenzi huo leo jijini Dar es salaam, Profesa Mbarawa amepongeza hatua iliyofikiwa sasa lakini pia amesisitiza kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili wananchi waweze kunufaika.
“Hakikisheni badala ya kutumia miezi 35 kujenga mradi huu, mnatumia miezi pungufu zaidi ili kuwawezesha wananchi na wadau wengine kunufaika na fursa za mradi huu”, amesisitiza Waziri Mbarawa.
Aidha, Amewataka wafanyakazi wote katika mradi huo kufanya kazi kwa bidii na uaminifu mkubwa kwa kuwa Serikali ina mpango mwengine wa kujenga Fly over kama hiyo itakayowawezesha kupata tena fursa ya ajira.
Hatua hiyo itapelekea kuwezesha wananchi kunufaika na mradi huo mapema, hivyo kupunguza gharama wanazozipata kutokana na msongamano wa magari uliopo sasa jijini Dar es salaam.
Naye, Balozi wa Japan nchini Bw. Masaharu Yoshida, amemhakikishia Waziri huyo kuwa ujenzi wa mradi huo utamalizika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo kuondoa changamoto ya msongamano katika barabara ya Nyerere na Mandela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa miradi kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Eng. Crspinius Ako, amesema kati ya nguzo 66 zinazohitajika kwenye awamu ya kwanza ya ujenzi huo, tayari nguzo 43 zimeshasimikwa ardhini, hali itayopelekea ujenzi huo kwenda kwa kasi.
Mpaka sasa mradi huo uliozinduliwa tarehe 1 Disemba 2015 umekamilika kwa asilimia 25.3 na zaidi ya shilingi bilioni 96.5 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa mradi huo ambao utakamilika mwezi Oktoba mwaka 2018.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Post a Comment

KAMERA YA MTAA KWA MTAA

[KAMERA YA MTAA KWA MTAA][carousel2]

HABARI

[HABARI][fbig1]

SHEREHE

[HARUSI][gallery1]

MKCT

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget