HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, February 4, 2017

NDUGU WAGOMEA MAITI YA MTOTO HOSPITALI YA AMANA JIJINI DAR ES SALAAM

Shangazi yake Julieth, Judith Christopher akielezea tukio hilo  kwa mwanahabari.
Julieth Daud (kulia) akiwa na dada yake nje ya wodi ya wazazi katika Hospitali hiyo.
Julieth (aliyekaa kushoto), akiwa na ndugu zake nje ya wodi ya wazazi katika Hospitali hiyo.
Mama mzazi wa Julieth, Veronica Lucas akiwa ameshika shavu kwa masikitiko kufuatia tukio hilo.
Mzazi Julieth Daudi (19) mkazi wa Tabata Relini, akiwa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na mwanahabari akidai amebadilishiwa mtoto aliyejifungua.


Na Dotto Mwaibale

MZAZI Julieth Daudi (19) mkazi wa Tabata Relini pamoja na ndugu zake wamegoma kuchukua mwili wa mtoto kwa madai kuwa mtoto huyo hakuwa wake kutokana na kubadilishiwa na wauguzi wa Hospitali ya Amana katika Manispaa ya Ilala  jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kujifungua.

Akizungumza kwa masikitiko nje ya viwanja vya hospitali hiyo Dar es Salaam jana, Daudi alisema kitendo alichofanyiwa kimemuumiza sana pamoja na ndugu zake wengine.

Alisema alifika Hospitalini hapo Februari 2 jioni akiwa amesindikizwa na mama yake Veronica Lucas na shangazi yake Judith Christopher.

"Nilipofika daktari aliponipima aliniambia kuwa hasikii mapigo ya mtoto isipokuwa ya kwangu hivyo alishauri siku iliyofuata nipate kipimo cha utrasaund lakini kabla ya kipimo hicho nilijisia uchungu na kujifungua" alisema Daudi.

Daudi alisema baada ya kupita muda kidogo muuguzi aliyemzalisha alimfuata na kumueleza kuwa mtoto wake alikuwa amefariki na alipomuuliza alikuwa wa jinsia gani muuguzi huyo alimweleza kuwa alikuwa hajui kama alikuwa wa kiume au wa kike.

Aliongeza kuwa wakati yupo wodini alimuona kijana mmoja aliyevalia koti la hospitali akiwa amembeba mtoto ambaye hakujua alikokuwa amempeleka.

Alisema baada ya kuambiwa mtoto wake amefariki aliomba aonyeshwe lakini hakuoneshwa ambapo alilazimika kwenda kuomba simu kwa mlinzi wa hospitali hiyo na kuwajulisha ndugu zake walipofika nao waliomba kuonyeshwa mwili wa mtoto huyo bila mafanikio.

Shangazi wa Julieth Judith Christopher alisema baada ya kutokea tukio hilo walikwenda kumuona Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo ambaye aliitisha kikao baina ya ndugu pamoja na maofisa wengine wa hospitali hiyo ambacho hakikufikia muafaka baada ya ndugu hao kukataa kuuchukua mwili wa mtoto huyo wakidai si wa kwao.

Aliongeza kuwa mganga mkuu huyo aliwaeleza kuwa mtoto huyo alikuwa amefia tumboni baada ya mama yake kuiharibu mimba hiyo kwa nia ya kuitoa na ndiyo sababu mtoto huyo alizaliwa akiwa mfu.

"Wanafamilia tumegoma kuuchukua mwili wa mtoto huyo na maamuzi yaliyofikiwa ni kufanyika kipimo cha DNN na ili mama wa mtoto aruhusiwe kutoka hospitali inatakiwa ipelekwe barua ya mwenyekiti wa mtaa wake anakoishi" alisema Christopher.

Muuguzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Beauty Mwambebule alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo hakuwa tayari kuzungumza kwa njia ya simu badala yake alimtaka mwandishi wetu kwenda hospitali kupata undani wa jambo hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad