HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 20, 2017

UWANJA WA TOTTENHAM HOTSPURS KUGHARIMU PAUND MILIONI 750


Uwanja huo utagharimu paund750m



Klabu ya Tottenham Hotspur ya Uingereza imetoa picha za kwanza za uwanja wa klabu hiyo ambao unaendelea kujengwa kaskazini mwa London ambao utatoshea mashabiki 61,000 na  utakuwa mkubwa zaidi  katika jiji kuu la London utakapofunguliwa mwaka 2018.

Miongoni mwa mengine, utakuwa na baa kubwa zaidi ya kuhudumia watu wote uwanjani, viti vyake vitakuwa na mitambo ya kubadili viwango vya joto na kutakuwa pia na kiwanda kidogo cha kutengeneza pombe, kiwanda kidogo cha kuoka mikate na keki.

Mwenyekiti wa Spurs amesema uwanja huo utaleta "taswira mpya kwa michezo na burudani". Uwanja huo utakuwa na sakafu iliyopandwa nyasi ambayo inaweza kuondolewa na chini yake kutokea sakafu ya mkeka.

Hilo litawezesha uwanja huo kuwa mwenyeji wa mechi za kandanda, NFL, matamasha pamoja na hafla nyingine.

Miongoni mwa mengine, uwanja huo utakuwa na:
.Njia iliyozingirwa kwa kioo cha kutumiwa na wachezaji kuingia uwanjani. Hii itawawezesha mashabiki kutazama yanayojiri kabla ya mechi.
.Eneo la kuuzia bia la umbali wa 285ft (86.8m) ambapo kila mtu atauziwa
.Mfumo mpya wa kusambaza bia ambao utawawezesha wauzaji kutoa painti 10,000 za bia kila dakika.
.Viti vitakuwa na mitambo ya kuongeza joto na sehemu za kuwezesha mtu kutumia vifaa vya USB.
Kutakuwa na sehemu moja ya kuketi watu 17,000, ambayo itakuwa kubwa zaidi Uingereza.

Ujenzi wa uwanja huo utagharimu £750m lakini utabuni nafasi 3,500 za ajira eneo hilo utakapokamilishwa, kwa mujibu wa klabu hiyo.Watu wataweza kuwatazama wachezaji wakiingia na kutoka uwanjani kupitia kiooWatu kwenye mgahawa wa ghorofa ya tisa wa Sky Lounge wataweza kutazama vizuri yanayojiri

Timu hiyo ambayo kwa sasa mkufunzi wake ni Mauricio Pochettino itahitajika kutumia uwanja mwingine msimu wa 2017-18 uwanja huo unapojengwa.

Chama cha Soka Uingereza(FA) kimewapa Spurs fursa ya kukodi uwanja wa Wembley ingawa pendekezo hilo limepingwa na mbunge wa chama cha Conservative Bob Blackman.

Chelsea, ambao wanajenga uwanja mpya wa Stamford Bridge kuweza kutoshea mashabiki 60,000 pia wamependekezewa uwanja huo wa Wembley.

Klabu za Uingereza zimekuwa zikijizatiti kuimarisha uwezo wa viwanja. Miaka kumi iliyopita Arsenal walijenga uwanja wao wa Emirates unaotoshea mashabiki 60,000.

West Ham walihamia uwanja wao wa Olimpiki unaotoshea mashabiki 57,000 eneo la Stratford, London mashariki. Uwanja wa sasa wa Stamford Bridge unaotoshea mashabiki 41,663 ndio wa saba kwa ukubwa miongoni mwa viwanja vinavyotumiwa na klabu za Ligi ya Premia huku uwanja wa Old Trafford unaotumiwa na Manchester United hutoshea mashabiki 76,000.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad