HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, January 18, 2017

KILIMANJARO MARATHON YAZINDULIWA RASMI MJINI MOSHI IKIWA NI MSIMU WA 15

 Mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2017 zimezinduliwa leo Mjini Moshi katika mkutano na wanahabari ulioandaliwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa kushirikiana na wadhamini wengine.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, Aliyewakilishwa na Meneja Mauzo wa TBL Kaskazini, Richard Temba,  alisema mbio hizo zitafanyika Februari 26, 2017 wilayani Moshi na zitahusisha wanariadha wa ndani na nje ya nchi kutoka pande mbalimbali za dunia.

“Kilimanjaro Premium Lager imeingia mwaka wake wa 15 kama mdhamini mkuu wa mbio hizi, kwa mafanikio makubwa na kuzifanya kuwa moja ya mbio kubwa zaidi za marathon barani Afrika, kwani kwa sasa hujumuisha zaidi ya wanariadha 8,000 kutoka nchi zaidi ya 45 kote duniani,” alisema Kikuli.

Kwa mujibu wa Meneja huyo wadhamini wengine wa mashindano hayo ni Tigo kwa 21km, Gapco kwa 10 km-viti vya magurudumu na baiskeli ya kunyonga kwa mkono na Grand Malt-5km. Wadhamini wengine ni pamoja na KK Security, TPC Limited, FNB, Kibo Palace, Kilimanjaro Water, CMC Automobile, Keys Hotel na pia wadhamini wapya Anglo Gold Ashanti na KNAUF Gypsum na mbio hizo zinaandaliwa  na kampuni ya Wild Frontiers  kwa kushirikiana na Deep Blue Media na kuratibiwa kitaifa na Kampuni ya Executive Solutions.

Alisema Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya Tsh milioni 500 katika mashindano haya na washindi  katika mbio za kilomita 42 watapata milioni 4 kila mmoja upande wa wanaume na wanawake huku jumla ya zawadi ikiwa Milioni 20.

Akizindua mbio hizo Mjini hapa,Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba aliwapongeza Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wengine na waandaaji kwa kazi nzuri kila mwaka, akiongeza kuwa mashindano yametokea kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya kimichezo ndani na nje ya nchi.

“Mashindano haya pia yamekwenda mbali zaidi katika kukuza utalii kwani wanariadha wa kimataifa na wageni wao hufanya utalii baada ya mashindano na hiyo kufaidisha uchumi wa nchi,” alisema huku akisisitiza kuwa mbio hizo zitatoa fursa nyingi sana hasa za kibiashara.

Mkurugenzi  wa Tigo Kanda ya Kaskazini, George Lugata , alisema huu ni mwaka wao wa tatu mfulululizo wa udhamini wa mbio za kilomita 21 na kuwa wamepata mafanikio makubwa kutokana na udhamini huu  kutokana na mashindano haya kukua mwaka hadi mwaka.

Alisema mwaka huu wamejiandaa vizuri na watatumia mbio hizi kuhamasisha uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro ili uendelee kuingizia fedha nyingi za kigeni kutokana na utalii huku akiongeza kuwa nia yao pia ni kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuleta mafanikio katika riadha na kuiweka Tanzania katika ramani nzuri ya kimichezo na kuongeza kuwa Kwa mujibu wa Bw. Lugata, jumla ya zawadi watakaotoa kwa washindi wa mbio hizo ni Tsh milioni 11.

Meneja Masoko wa GAPCO Tanzania Caroline Kakwezi alisema kwa mara nyingine watatoa usafiri, malazi na chakula kwa washiriki wa mbio za kilometa 10 kutoka Dar es Salaam na usafiri kwa washiriki kutoka Arusha na Moshi.

Kakwezi alisema, “Tanzania Paralympic Committee imeandaa shidano la mchujo ili kuwapata washiriki wa Kilimanjaro Marathon na mchujo huu utafanyika katika Uwanja wa Uhuru Jumamosi Februari 11 kuanzia saa mbili kamili. Tunawaomba washiriki wote wajitokeze ili waweze kupata nasfasi hii,” alisema huku akiwashukuru wateja wa GAPCO kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuwawezesha kudhamini Kilimanjaro Marathon kwa miaa sita sasa na kuongeza kwamba jumla ya zawadi watakazotoa kwa washindi ni Tsh milioni 10.4.

Meneja wa Grand Malt, Oscar Shelukindo alisema wanaona fahari kubwa kudhamini mbio za kilometa tano na kuwataka wale wote wanaoona hawataweza kushiriki kwenye mbio ndefu kujitokeza kwenye mbio hizo za umbali wa kilometa tano, akisema zina mvuto wa aina yake.

Alisema Grand Malt imepata mafanikio makubwa kutokana na matukio kama haya kwani ni kinywaji chenye afya cha watu wa rika zote.
Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu wa 15 wa mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathon 2017 ,uzinduzi uliofanyika Kibo Palace Home mjini Moshi.
Baadhi ya wageni waalikwa wakifuatilia uzinduzi huo.
Meneja Mauzo wa Kampuni ya TBL mikoa ya Kilimanjaro na Tanga ,Richard Temba akizungumza wakati wa uzinduzi huo,TBL ndio wadhamini wakuu wa Mbio hizo kupitia Bia yake ya Kilimanjaro.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mawasiliano ya simu za mkononi ya TIGO ,Kanda ya Kaskazini,George Lugata akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Marathon 2017 ,Tigo wanadhamini mbio hizo kwa upande wa Mbio za Kilometa 21
Baadhi ya wageni waalikwa katika hafla fupi ya uzinduzi wa mbio hizo.
Meneja Masoko wa Kampuni ya GAPCO Tanzania ,Caroline Kakwezi akizingumza wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2017, GAPCO wanadhamini mbio za Kilometa 10 kwa upande wa walemavu.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Executive Solution ,Aggrey Mareale ambao ndio waratibu wa mbio hizo akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mwakiishi wa Kampuni ya Sukari ya TPC,Allen Maro akizungumza wakati wa hafla hiyo,TPC pia ni wadhamini wa mashindano hayo ya kimataifa ambayo hufanyika kila mwaka.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya kuchimba Dhahabu ya Geita Gold Mining (GGM) Tenga B Tenga akizungumza wakati wa uzinduzi huo,GGM wakiwa ni wadhamini wapya katika mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Chama cha Riadha mkoa wa Kilimanjaro (KAA) Liston Methacha akizungumza kwa niaba ya shirikisho la Riadha Tanzania katika uzinduzi huo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Wildfrontiers,John Hudson ambao ndio waandaaji wa mbio hizo akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Kibo Palace,Vicent Lasway akizungumza katika hafla hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro,Wilbroad Mutafungwa akizungumza katika hafla hiyo.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akiwapongeza wawakilishi wa kampuni zilizojitokeza kudhamini Mbio hizo za kimataifa.
Mkuu wa wilaya ya Moshi,Kippi Warioba akiwa na wawakilishi wa kampuni zinazodhamini mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Marathoni 2017 pamoja na jeshi la Polisi ,akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mbio hizo.
Mgeni rasmi katika hafla fupi ya uzinduzi wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathoni 2017 akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini wa Mbio hizo.

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii kanda ya Kaskazini. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad