Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bw. Bernard Konga
akiongozana na baadhi ya wakurugenzi wa Mfuko na uongozi wa Hospitali ya Kairuki
walipotembelea maeneo mbalimbali ya hospitalini hapo kuangalia huduma zinazotolewa kwa
wanachama wa Mfuko. Pichani akimjulia hali mwanachama wa Mfuko aliyelazwa hospitalini hapo.
Na Grace Michael
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga
amezitaka Hospitali zote nchini zinazohudumia wanachama wake kuhakikisha zinatoa
huduma bora na zinazostahili kwa wanachama ikizingatiwa ukweli kwamba
wamekwishazilipia huduma hizo kabla ya kuugua.
Aidha amewahakikishia wanachama wa Mfuko kwamba, Mfuko umejipanga
kuwahudumia na kutatua kero wanazokabiliana nazo wakati wa kupata huduma ili
wajivunie huduma walizolipia.
Bw. Konga amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kujionea namna wanachama wa
Mfuko wanavyohudumiwa katika Hospitali ya Kairuki mjini Dar es Salaam ambapo mbali
na kuona huduma pia alipata fursa ya kuzungumza na wanachama waliofika hospitalini
hapo kupata huduma.
Bw. Konga akiwasikiliza wanachama wa Mfuko waliokuwa wakipata huduma za matibabu hospitalini hapo.
Akizungumza na wanachama katika Hospitali ya Kairuki, Bw. Konga alisema kuwa
ameamua kuanza ziara ya kutembelea hospitali zote ili kukutana na wanachama,
kusikiliza kero zao pamoja na kuzungumza na watoa huduma kwa lengo la kutatua
matatizo yaliyopo na kujenga uhusiano bora.
“Nimeamua kuanza rasmi ziara hizi za kikazi kuwaona moja kwa moja wanachama
wanahudumiwa ili nizungumze nao na kupata maoni kutoka kwao…wanachama kwangu
ndio kipaumbele cha kwanza kwa kuwa ndio wametupa dhamana ya kuwahudumia na
kukaa na fedha zao hivyo binafsi sitakubali kuona mwanachama akipata huduma
hafifu”. Alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa kitendo cha kutoka na kusikiliza wanachama kitasaidia kwa kiasi kikubwa
kuboresha huduma lakini pia kukutana uso kwa uso na wananchi ambao Mfuko
unawahudumia.
Wakiendelea kupata maelezo ya huduma hospitalini hapo.
Wakizungumza mbele ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo baadhi ya wanachama
waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo, kwanza wameupongeza Mfuko kwa hatua
hiyo ya kuamua kutoka nje kwa lengo la kukagua huduma lakini pia kwa maboresho
mbalimbali ambayo yamefanywa na Mfuko.
“Hii kazi ambayo umeianza Mkurugenzi Mkuu ni nzuri sana na tunaomba pia hata vituo
vya chini kwa maana ya Zahanati navyo vitembelewe ili kuwekewa utaratibu mzuri
zaidi…matatizo bado yapo lakini kwa kiasi kikubwa mmejitahidi sana kuyatatua,”
walisema wanachama hao.
Kwa upande wa Mwanachama wa Mfuko ambaye anahudumiwa na Mfuko chini ya Fao
la Wastaafu Injinia Emmanuel Olekambainei ambaye alifika hospitalini hapo kwa ajili ya
kupata huduma za macho, naye aliupongeza Mfuko na kumtaka Kaimu Mkurugenzi
Mkuu kuangalia zaidi huduma ambazo haziko katika kitita cha mafao.
Bw. Konga akipata maelezo ya namna wagonjwa wanavyopokelewa.
Aidha Injinia Olekambainei alisema kuwa huduma za afya hususan zinazotolewa na
Mfuko zimeboreshwa na hasa katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano.
“Nawapongeza kwa kweli maana kuna mabadiliko makubwa na inatokana na kasi ya
Serikali yetu hivyo hongereni sana maana mimi mwenyewe napata huduma hapa kwa
mwamvuli wa ustaafu chini ya NHIF,” amesema Bw. Olekambaini.
Akizungumza na Uongozi wa Hospitali ya Kairuki,Bw. Konga alisema kuwa ni muda
muafaka kwa Mfuko kushirikiana kwa karibu na watoa huduma kwa lengo la kutoa
huduma bora kwa wanachama wa Mfuko.
Kwa upande wa Uongozi wa Hospitali ya Kairuki ulioongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dr.
Asser Mchomvu, alisema kuwa hawana matatizo na uhusiano kati yao na Mfuko kwa
kuwa wanatambua mchango katika kuboresha huduma zao.
Wakipata maelezo kutoka katika chumba cha kuchakata madai ya huduma zilizotolewa kwa wanachama.
“Tuwe wazi kuwa bila NHIF hatuwezi kujiendesha hata siku moja na wagonjwa
tunaowahudumia hapa zaidi ya asilimia 90 ni wanachama wa NHIF hivyo tunao wajibu
wa kuhakikisha kwamba Mfuko hauyumbi kwa namna yoyote vile vile kwetu
wanachama wa NHIF ndio wateja wetu wakubwa hivyo tunawathamini na kuwaheshimu
sana,” alisema.
Alisema kuwa changamoto za kiutendaji kati yao na Mfuko zikiwemo za bei za huduma,
mifumo na ulipaji wa madai wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha
haziwakwamishi kutoa huduma kwa wanachama.
Akihitimisha ziara hiyo Bw. Konga alitoa wito kwa wanachama wote kuhakikisha
wanatoa taarifa wakati wowote wanapokutana na changamoto wakati wa kupata
huduma za matibabu.
Meneja wa Idara ya Ukjaguzi wa Kairuki akitoa maelezo ya huduma mbele ya wanachama na uongozi wa NHIF.
No comments:
Post a Comment