HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 1 October 2016

HIVI NDIVYO HALI ILIVYOKUWA WAKATI WA MCHEZO WA YANGA NA SIMBA UWANJA WA TAIFA LEO

HAKUNA mbabe, ule mtanange uliokuwa unasuburiwa kwa hamu kubwa uliohusisha mahasimu wawili Yanga na Simba umemalizika jioni ya leo kwa timu hizo kutoka sare ya 1-1.

Katika mchezo huo uliokuwa na presha kubwa kwa kila upande, Yanga walifanikiwa kupata goli dakika ya 26, baada ya Amisi Tambwe kumzidi mbinu beki Novat Lufungo wa Simba na kuandika goli la kuongoza huku nahodha Jonas Mkude akipewa kadi nyekundu baada ya kumpiga mwamuzi kwa kudai kuwa Tambwe aliushika mpira kwa mkono.

Mpira ulisimama kwa dakika takribani tano na vurugu kutokea ikiwemo mashabiki wa Simba kuanza kung'oa viti na kuvirusha uwanjani, hali iliyopelekea Jeshi la Polisi kuanza kupiga mabomu ya machozi ili kutuliza ghasia iliyojitokeza uwanjani hapo.

Mpaka ilipofika mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa goli 1-0, lakini kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa Kelvin Yondan aliyekuwa na kadi ya njano na kuingia Andrew Vicent "Dante", Saimon Msuva akachukua nafasi ya Juma Mahadhi, Haruna Niyonzima akiingia baada ya Deus Kaseke, Simba wakimtoa Laudit Mavugo na kuingia Fredrick Blagnon, Ibrahim Ajib na kuingia Mohamed Ibrahim na Novat Lufungo na kuingia Jurko Murshid.

Mchezo uliokuwa wa kasi kwa kila upande huku Yanga wakitafuta goli la kuongoza na Simba wakisaka la kusawazisha, ambapo dakika ya 89 Shiza Kichuya anawainua mashabiki wa Simba baada ya kupiga kona iliyoenda moja kwa moja wavuni na kusawazisha na kudumu mpaka dakika 90. Na Zainab Nyamka.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad