HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 14, 2016

Zaidi ya Bil. Moja zachangwa kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Kagera

Na Sheila Simba, MAELEZO 

Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimechangwa na mabalozi na wafanyabiashara kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Mkoani Kagera. 

Michango hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam katika harambee iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na kufanyika Ikulu. Akizungumza katika harambee hiyo Waziri Mkuu alisema jumla ya nyumba 840 zimebomoka na kuharibika kabisa, wakati nyumba 1264 zimepata hitilafu na zinaweza kufanyiwa marekebisho ili watu waendelee kuishi katika nyumba hizo. 

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa shule 4 za sekondari ambazo ni Nyakato, Ihungo, Kashange na Buhembe zimeharibika na mbili kati ya hizo yaani Ihungo na Nyakato zimefungwa kutokana na kuharibika sana. 

Madhara mengine yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kuharibika kwa vituo vya afya, miundombinu ya barabara, umeme na njia za mawasiliano na kufanya athari za tetemeko kuwa kubwa. 

Kutokana na athari hizo Waziri Mkuu amewaomba mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kusaidia waathirika kwani ni tukio ambalo halikutarajiwa na limeleta hasara kubwa kwa wanakagera na Taifa kwa ujumla. “Licha ya michango hii ninayowaomba leo, tutaandaa safari kwa anayehitaji kwenda kujionea hali halisi ili aone ni namna gani atakavyosaidia,”alisema Waziri Mkuu. 

Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa imefunguliwa akaunti ya kuchangia katika maafa hayo kwenye benki ya CRDB inayojulikana kama KAMATI MAAFA KAGERA akaunti namba 0152225617300 na swift code ambayo ni CORUtztz na kuwaomba wananchi na watu wengine kutumia akaunti hiyo kwa kusudi hilo. Majaliwa amesema pia kuwa utaratibu unaandaliwa ili kuwawezesha watu kuchangia kwa njia ya Mpesa, tigopesa na Airtelmoney. Utaratibu huo utakapokuwa tayari utatangazwa ili kuwarahisishia watumiaji wa mitandao hiyo kuchangia. 

Katika harambee hiyo wafanyabiashara waliochangia ni Mwenyeki Mtendaji wa kampuni za IPP Dkt Reginald Mengi aliyechangia Tsh million 110, Mohamed Dewji ametoa milioni 100, Subash Patel milioni 150 na Salim Turki aliyetoa mifuko 5000 ya saruji na mabati 3000. 

Wengine waliochangia ni kampuni mbali mbali zikiwemo kampuni ya bia ya Serengeti iliyotoa mifuko 800 ya saruji, Sahara Tanzania wametoa shilingi milioni 20, Camel Oil kupitia Camel Cement wametoa mifuko 1000 ya saruji ,Puma wamechangia shilingi million 50, Pepsi Cola wametoa milioni 50 na Azania Group wamechangia milioni 50. 

Baadhi ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini waliochangia ni pamoja na ubalozi wa China shilingi milioni 100 na kupeleka madaktari,dawa,mahema na vifaa vingine kwa ajili ya kusaidia waliopatwa na maafa hayo. Kuwait kupita ubalozi wao nchini wamechangi dola elfu 10 za Kimarekani na euro elfu 10, na Nchi ya Kenya iliyopeleka msaada wa mahema,magodoro na dawa. 

Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wametoa milioni 10, mwakilishi wa China Merchantile Group ametoa milioni 100, Toyota Tanzania milioni 10, Kamal Group milioni 50, Urban Group milioni 20, TBL milioni 100, IPTL 50, Tanzania Agriculturak Processing Zone milioni 30, Umoja wa wafanya biashara ya mafuta ya rejereja milioni 250 na Group Six wametoa tani 80 za saruji. 

Wengine waliochangia ni pamoja Jambo plastic milioni 20, Tanga Cement mifuko 1000 ya saruji, Agusta Tz milioni 10, Oryx milioni 50, Kagera Sugar milioni 100 na tani 10 za sukari, Tipper milioni 20 ambapo GBP, Oilcom na Moil watajenga shule mbili zilizoharibika. 

Uchangiaji huo umejumuisha pia na watu binafsi ambao ni wakili wa kujitegemea, Bwana Protase Ishengoma milioni 5 na Melisa Kataraiya milioni 20. 

Tetemeko hilo la ardhi ni kubwa kuliko yote ambayo yamewahi kutokea hapa nchini na hadi sasa limesababisha vifo vya watu 17 na kuharibu nyumba, majengo na miundombinu mkoani Kagera. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 100 kutoka kwa Charge d’ Affairs wa ubalozi wa China nchini, Bw. Haodong Gou wakati alipokutana na wafanyabiashara na mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini na kuwaomba wasaidie kuchangia ujenzi na ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko laardhi mkoani Kagera. Mkutano huo ulifanyika Ikulu jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016.Katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Suzan Kolimba. (Picha na Odisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Wafanyabishara na Mabalozi wa Nchi Mbalimbali hapa nchini kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.Alikutana nao Ikulu jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016. 
Baadhi ya Mabalozi na Wafanyabiashara wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao , Ikulu jijini Dar es salaam Septemba 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya mabalozi na wafanyabiashara baada ya kukutana nao Ikulu jijini Dar es salaam Septeba 13, 2016 kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati Miundombinu ilitoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kageza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya mabalozi na wafanyabiashara baada ya kukutana nao Ikulu jijini Dar es salaam Septeba 13, 2016 kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati Miundombinu ilitoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kageza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya mabalozi na wafanyabiashara baada ya kukutana nao Ikulu jijini Dar es salaam Septeba 13, 2016 kuwaomba wachangie katika kujenga na kukarabati Miundombinu ilitoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kageza. (picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad