Mtaa Kwa Mtaa Blog

WANACHAMA 106 PPF KANDA YA ZIWA WANUFAIKA NA KADI ZA MATIBABU KUPITIA MFUMO WA WOTE SCHEME

Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshack Bandawe akizungumza na wanachama wa mfuko huo jijini Mwanza jana kabla ya kuwakabidhi kadi za matibabu ya mfumo wa uchangiaji wa hiari(Wote Scheme).

Na Baltazar Mashaka,Mwanza

WANACHAMA 106 kati ya 7, 185 wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa kupitia mfumo maalum wa uchangiaji wa hiari wa WOTE Scheme wamekabidhiwa kadi zitakazo wawezesha kupata huduma za matibabu.

Akikabidhi kadi hizo kwa wanachama hao, Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa Meshach Bandawe alisema mfumo huo umewalenga wanachama waliojiajiri wenyewe katika Sekta isiyo rasmi ambao kwa mujibu wa takwimu za kitaifa ni zaidi ya asilimia  90 ya nguvu kazi ya taifa.

Alisema kuwa bahati mbaya kundi hilo lilisahaulika na halijakingwa kikamilifu na sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wanapatwa na majanga hatarishi sawa na wafanyakazi wa sekta rasmi.

“ Watu waliojiajiri kwenye Sekta isiyo rasmi wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji mali  na kuwaingizia kipato cha uhakika na kumudu kuendesha maisha yao.Bahati mbaya hawana akiba yoyote wanayoweza kunufaika nayo kwa maisha ya baadaye iwapo wangejiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii,” alisema.
Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshack Bandawe akimkabidhi Anastanzia Magere kadi ya matibabu ya mfumo wa uchangiaji wa hiari(Wote Scheme) jijini Mwanza jana. Mpaka sasa Kanda hiyo wamekwishajiunga wanachama 7185 kwa kipindi cha Agosti 2015 mpaka Agosti 2016. Picha na Lordrick Ngowi

Meneja huyo wa PPF alieleza kuwa mfuko kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) utatoa huduma ya matibabu kwa wanachama baada ya kuchangia sh.60,000  na watatibiwa magonjwa yaliyoanishwa kwenye sera ya kitaifa.

Bandawe alisema wanachama hao watapata huduma hiyo ya matibabu katika hospitali zaidi ya 6,000 nchini ambazo zimeingia mkataba na NHIF na wanastahili kuwa na kadi watakazotumia kupata huduma hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja na akatoa wito kwa makundi mbalimbali yaliyoko katika sekta isiyo rasmi yajiunge na mfumo huu kwa faida ya maisha yao na wanufaike na huduma mbalimbali zinazotolewa na PPF .

“Wafanyakazi walioajiriwa kwenye sekta rasmi serikali kuu,serikali za mitaa,taasisi zote ,mashirika  na makampuni ya umma , mashirika yasiyo ya kiserikali na makampuni binafsi wajiunge na mfumo wa uchangiaji kwa hiari wafaidike na huduma za mikopo ya elimu na maendeleo,” alieleza.


Pia alisema kuwa mafao ya pensheni ya uzeeni yatalipwa baada ya mwanachama kuchangia miezi 180 sawa na miaka 15  na kufikisha umri wa miaka 55 ya kustaafu  huku wanachama 7,185 wakijiunga na mfumo wa WOTE Scheme tangu Agosti 2015 hadi Agosti 2016.

Aidha, alieleza zaidi kuwa wanachama watapata huduma ya mkopo wa elimu wao binafsi ama watoto watakaogharamiwa kuanzia shule ya awali hadi kidato cha sita baada ya kuchangia kwa miezi sita na ataurejesha mkopo huo kuanzia mwaka mmoja hadi mitano kutegemea kiwango cha ada kilichoanishwa.Post a Comment

KAMERA YA MTAA KWA MTAA

[KAMERA YA MTAA KWA MTAA][carousel2]

HABARI

[HABARI][fbig1]

SHEREHE

[HARUSI][gallery1]

MKCT

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget