HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 30, 2016

SERIKALI KUBORESHA SERA YA UBORESHAJI WA VIWANDA VYA DAWA VILIVYOPO HAPA NCHINI.

 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo akitoa hotuba katika ufunguzi wa kongamano la 49 la Chama cha  Wafamasia Tanzania.
 Rais wa Chama cha wafamasia Tanzania (PST) Ndg. Michael Kishiwa (aliyesimama)akitoa taarifa ya Chama kwa kifupi kwa  Mgeni Rasmi Mhe. Mrisho Gambo katika Kongamano la 49 la wafamasia Tanzania linalofanyika Jijini Arusha.
 Wanachama wa PST wakifuatilia ufunguzi wa Kongamano.
Wajumbe wa kongamano wakiendelea kufuatilia Hotuba ya Ufunguzi  katika Kongamano la wafamasia linalofanyika katika Jiji la Arusha.

Na Nteghenjwa Hosseah, ARUSHA
SERIKALI imesema kuwa inaanza kufanya maboresho kwa kuandaa na kuhakikisha  Sera ya Uboreshaji wa Viwanda vya Dawa vilivyopo nchini  kwa kuwawezesha na kuwajengea uwezo  wenye viwanda nchini ili waweze kuzalisha dawa na kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo kwa niaba ya Waziri  wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza katika Kongamano la  49 la Chama Cha Wafamasia Tanzania (PST),linalofanyika jijini hapa kwa siku mbili.

Akizungumza kwa niaba ya Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo,alisema kuwa kutokana na umuhimu wa sekta hiyo ya dawa, Serikali inaangalia taaluma hiyo kwa macho mawili kwa lengo la kuiboresha ili iweze kutoa huduma bora.

"Wizara yangu inaangalia taaluma hii kwa macho mawili katika kuhakikisha kuwa sekta ya dawa inaboreka na inakua na hatimaye kuweza kukuza uchumi wetu, kwa kuwawezesha na kuwajengea uwezo wenye viwanda nchini ili waweze kuzalisha zaidi ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia soko ndani ya nchi na kupunguza uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi na hivyo kuwa na dawa bora, salama na zenye ufanisi"

"Endapo tutazalisha dawa zetu wenyewe hii itatupunguzia gharama zisizo za lazima kuagiza dawa nje ya nchi, sambamba na hili pia tunaboresha vyuo vya Wafamasia ili waweze kutoka wataalamu bora wa masuala haya ya madawa,”alisema Gambo.

Akizungumzia suala la wizi wa dawa katika hospitali za serikali,alisema kuwa Serikali haina mchezo na yoyote atakayokiuka maadili ya taaluma hiyo na kuwa watawachukulia hatua kali za kisheria ili wananchi wapate huduma bora za dawa.

"Mbali na changamoto ya upungufu wa dawa, wafanyakazi wasio waadilifu ambao wanatumia nafasi zao vibaya wanashirikiana na baadhi ya wafanyabiashara na kuuza  dawa, hili ni suala muhimu PST jadilianeni suala la maadili kwani hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa"alisema

Awali Rais wa PST, Michael Kishiwa, aliiomba Serikali kuongeza udahili wa wanafunzi wa famasia wakiwemo mafamasia wasaidizi ili kutoa dawa sahihi kwa wagonjwa.

Alisema hivi sasa idadi ya watanzania ni kubwa, lakini wataalamu wa dawa Wafamasia ni 1,200, hali inayochangia kuwepo kwa watoa huduma hiyo wasio na sifa.

Alisema kutokana na kukosekana wanataaluma kumekuwepo na changamoto kubwa ya baadhi yao kukiuka maadili na wengine kufanya kazi ya utoaji dawa pasipokuwa na uelewa nayo, hali ambayo hatari kwa afya za binadamu.

Kishiwa alisema kazi kubwa ya chama chao kuhakikisha inasimamia ubora wa utoaji huduma ya dawa na kusimamia maadili, ili wananchi wapate dawa sahihi na kuzitumia ipasavyo.

“Tunashirikiana na baraza la usajili la wafamasia katika kukemea vitendo hivyo vya ukiukwaji wa maadili na ndiyo maana tunaiomba serikali iongeze udahili na vyuo vinavyotoa taaluma hii"alisema
Naye Msajili wa Baraza la Wafamasia, Elizabeth Shekalage alisema kwa sasa wananchi wengi wamechukulia huduma ya dawa ni biashara na kuwa baraza limejipanga kupambana na watu wanaofanya huduma hiyo ni biashara huku wakikiuka  maadili.

"Uchache wa wanataaluma unasababisha kika mtu aone hii ni biashara huria na yeyote anaweza kuifanya,kuna uhaba mkubwa wa fundi dawa sanifu,mafundi dawa wasaidizi,dawa ni sumu hivyo tunasimamia hili ili kuepusha madhara kwa watumiaji"alisema Elizabeth
Kongamano la Mwaka huu linaenda na kauli mbiu isemayo kuelezea ubora,usalama,ufanisi na upatikanaji wa huduma bora za kifamasia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad