HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 15, 2016

MAKALA MICHEZO: MFAHAMU MCHEZAJI MWINYI HAJI NGWALI

Na Zainab Nyamka.


MWINYI Haji Ngwali ni beki wa kushoto wa timu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam aliyesaini kuitumikia timu hiyo.

Yanga ilimsajili beki huyo ili kuongeza nguvu katika kikosi chao kwa kusaidiana na beki wa muda mrefu wa timu hiyo Oscar Joshua.

Mwinyi alisajiliwa na Yanga akitokea katika timu ya KMKM iliyopo visiwani Zanzibar baada ya kocha Hans Van de Pluijm kuvutiwa na kiwango chake .

Beki huyo ameonekana kuwa tegemeo katika timu yake ya Yanga pamoja na Taifa baada ya kuonekana kuwa na uwezo mkubwa uwanjani huku akiisaidia vema safu ya ulinzi.

Nyota ya mchezaji huyo ilianza kung'ara pale alipoitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ilipokuwa chini ya Mart Nooij.

ELIMU
Mwinyi alipata elimu yake ya msingi katika shule ya Amani na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya Kwereke ambapo hakufanikiwa kumaliza kidato cha nne baada ya kutofanya vizuri katika mtihani wa kidato cha pili na kuamua kujiingiza rasmi kwenye soka.

SAFARI YAKE KATIKA SOKA
Mwinyi alianza kujihusisha na soka wakatiyupo  shule ya msingi akiwa na umri wa miaka 10.
Mwinyi amepitia katika vituo mbalimbali na kushiriki ligi visiwani Zanzibar.

TIMU ALIZOWAHI KUCHEZEA
Mwinyi alifanikiwa kujiunga na kituo cha Jiva Nile ambacho kilimsaidia katika kuendeleza kipaji chake.
Baadaye Mwinyi alijiunga katika kituo cha Junior Naturally alipokaa kwa misimu miwili na kufanikiwa kujiunga na timu ya Mapunda inayoshiriki ligi daraja la pili visiwani Zanzibar.

Akiwa na timu hiyo mwaka 2011 aliitwa katika kikosi cha Kombaini ya U-20 ya Mjini Magharibi ambapo walishiriki mashindano ya Copa Coca Cola. 2012 akiwa na timu ya Chuoni ilishiriki mashindano ya Mapinduzi Cup na kufanikiwa kuwa mchezaji bora na 2014 alisajiliwa na timu ya KMKM ya Zanzibar iliyoshirikushiriki mashindano ya Kagame 2015 na Yanga kuvutiwa nae na kumjumuisha katika kikosi chao.

NJE YA SOKA
Nje ya soka Mwinyi ana ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa wa ndani na nje. Anasema kwa sasa ameweka mikakati thabiti na atahakikisha mikakati hiyo inafanikiwa ili aweze kutimiza ndoto alizonazo katika maisha yake ya baadaye.

NAPENDA
Mwinyi anapenda kuona familia yake inafuraha kwani hiyo ndo imekuwa msingi mzuri wa mafanikio. Anasema mara nyingi anapokuwa nyumbani hupenda kuangalia filamu mbalimbali hasa zile anazokuwa wameshiriki Mboto na Gabo pamoja na kusikiliza muziki Bongo fleva wa hasa pale anapokuwa amechoka.

SIPENDI
Mwinyi anasema kuwa hapendi kukaa maeneo yanayokuwa na vurugu au kelele kwani mara nyingi anapenda kupumzika. Anasema yeye kama mchezaji muda mwingi hupumzika hasa baada ya mazoezi hivyo hujitahidi kuepuka kukaa sehemu zinazokuwa na kelele.

MALENGO
Malengo ya Mwinyi Haji ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwani ana amini kuwa yeye ni mchezaji mwenye kiwango kikubwa katika soka na anauweza wa kuchezea timu yoyote itakayomuhitaji. Anasemakuwa atakapofanikiwa kucheza soka nje ya nchi anaamini kuwa ndoto zake alizoweka katika maisha zitafanikiwa kwa urahisi.

AJIRA KWA VIJANA
Mwinyi anasema kuwa suala la ajira limeendelea kuwan tatizo kubwa kwani vijana wanaomaliza vyuo kila mwaka ni wengi ukilinganisha na ajira zinazotangazwa. Anasema vijana wanatakiwa kubadili mtazamo wao na kutafuta njia mbadala za kuweza kujikwamua kimaisha ikiwemo kujiajiri au kuunda vikundi vya vitakavyoweza kupatiwa mikopo na kujiingiza kwenye miradi itakayowasaidia kutengeneza ajira zao binafsi na kuajiri wengine.

USHAURI KWA WIZARA YA MICHEZO
Mwinyi anasema kuwa angeomba kuboreshwa kwa viwanja vya michezo ili viweze kuwa na hadhi kutokana na vingi kuwa katika hali mbaya kwani endapo Tanzania tungekuwa na viwanja vizuri basi vipaji vingi zaidi vingeendelea kujitokeza na kuacha dhana kuwa watu wanacheza mpira kutokana na kukosha shughuli maalum za kufanya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad