HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 27, 2016

Dkt Kalemani aipa Onyo kampuni ya usambazaji Umeme Vijijini

Na Teresia Mhagama, Arusha

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani ametoa onyo kwa  kampuni ya SPENCON inayosambaza umeme vijijini katika mikoa ya Kilimanjaro na Singida na kuitaka kuhakikisha kuwa inakamilisha kazi ya kusambaza umeme katika mikoa hiyo ifikapo tarehe 15 Oktoba, 2016 baada ya kuonekana inasuasua katika kazi hiyo.

Dkt. Kalemani alitoa onyo hilo mkoani Arusha wakati alipokutana na Watendaji wa kampuni hiyo kabla ya kuanza kwa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa  miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili (REA II), wilayani Simanjiro katika vijiji vya Losinyai na Kilombero.

“ Kasi yenu ya usambazaji umeme vijijini hairidhishi katika maeneo yote mnayosambaza umeme, utekeleaji wa miradi yenu umekuwa ukisuasua na ni chini ya asilimia 76, pia nimefuatilia na nikakuta Fedha zenu za kazi mmeshalipwa hivyo ifikapo Oktoba 15 kazi iwe imemalizika na msipokamilisha tutachukua hatua za kisheria,” alisema Dkt. Kalemani.

Aidha akiwa katika kijiji cha Losenyai na Kilombero wilayani Simanjiro, Dkt Kalemani  aliiagiza kampuni inayosambaza umeme vijijini ya CCC Nigeria Engineering International  na  Meneja TANESCO mkoa wa Manyara kuhakikisha kuwa wanawasha umeme katika vijiji hivyo tarehe 27 Septemba, 2016 baada miundombinu ya umeme kukamilika.

Sanjari na hilo, Naibu Waziri aliwaagiza Watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 1 Oktoba 2016,  wanaanza kubandika   majina ya wakandarasi wanaosambaza  umeme vijijini kwenye ofisi za Shirika hilo ili wananchi wawatambue  na hivyo kuepusha wakandarasi vishoka wanaowaibia wananchi fedha kwa ahadi ya kuwaunganishia umeme.

Awali Mbunge wa Simanjiro,  James Millya alimueleza Naibu  Waziri kuwa kuwashwa kwa umeme katika vijiji hivyo kutawawezesha wananchi kufanya shughuli mbalimbali za maedeleo  ikiwemo biashara na kwamba wananchi wengi ambao ni wafugaji wataweza kujisomea nyakati za jioni mara baada ya kumaliza shughuli zao za ufugaji.

Vilevile Millya alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha kuwa wanalinda miundombinu ya umeme kwani  Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika ujenzi wake na kuiomba  Serikali kuendelea kusambaza umeme katika vijiji vyote ambavyo havijapata umeme kwenye Jimbo hilo.

Aidha Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza Watendaji wa TANESCO kote nchini, kutokaa ofisini na badala  yake wawafuate wananchi pale walipo na kuwahudumia.

 “ Wafanyakazi wa TANESCO hawatakiwi kufuatwa ofisini na wananchi, wao ndiyo wanaopaswa kuwafuata wananchi pale walipo na kuwapa huduma mbalimbali na kutafuta wateja wapya wanaotaka kuunganishiwa umeme,  hii itapelekea Shirika kuboresha  huduma kwa wananchi na kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani alisema kuwa wananchi wengi bado kipato chao ni kidogo hivyo  ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wanazotumia kufuata huduma katika Ofisi za Serikali ni lazima watumishi wajenge utaratibu wa kupelekeka huduma hizo kwa wananchi kwa kushirikisha  Ofisi za Serikali za Mtaa, Vijiji  na Kata.

Aliongeza kuwa Serikali ina mpango wa kujenga ofisi za TANESCO katika nchi nzima kwa ngazi ya wilaya na Ofisi nyingine ndogondogo  ili kusogeza huduma kwa wananchi, hata hivyo alisema kuwa utekelezaji wa agizo la kuboresha huduma kwa wananchi hautasubiri ujenzi wa Ofisi hizo.
Mkazi wa Kijiji cha Losinyai, wilayani Simanjiro, Looki Kembele (kulia) akimshukuru Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mwenye suti nyeusi), mara baada ya kukabidhiwa kifaa kijulikanacho kama UMETA ambacho kitamwezesha Mwananchi huyo kuwashiwa umeme ndani ya nyumba bila kuingia gharama ya kusuka nyaya za umeme. Wanaoshuhudia ni Mbunge wa Simanjiro, James Millya (kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula (kushoto kwa Naibu Waziri).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (mwenye suti nyeusi) akizungumza na Wananchi katika kijiji cha Losinyai wilayani Simanjiro wakati alipokwenda kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji vijijini, Awamu ya Pili (REA II).
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akipungia mikono wananchi katika Kijiji cha Kilombero wilayani Simanjiro mara baada ya wananchi hao kumvalisha shuka na kumkabidhi fimbo ikiwa ni ishara ya shukrani kwa Serikali kwa juhudi za kupeleka umeme katika kijiji hicho. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (aliyenyanyua mikono) akizungumza na Wananchi katika Kitongoji cha Sajila wilayani Simanjiro wakati alipokuwa akikagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji vijijini, Awamu ya Pili (REA II). Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad