Na Mathias Canal, Singida.
Wakuu
wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa
vijiji na wenyeviti wa vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi Mkoani
Singida hii leo wamepatiwa mafunzo ya kutambua mipaka ya majukumu yao
kiutendaji katika kikao cha kazi kilichofanyika katika ukumbi wa shule
ya sekondari Ikungi.
Mafunzo
hayo yameandaliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na
kubainika kuwa asilimia kubwa ya watendaji hususani wenyeviti wa vijiji
na vitongoji wamekuwa wakiingilia katika majukumu ya kiutendaji.
Akifungua
mafunzo hayo yaliyodumu kwa zaidi ya masaa matano yaliyojikita zaidi
kutoa ufafanuzi juu ya majukumu ya watendaji wa Kata, Wenyeviti wa
Vijiji na Watendaji wa Vijiji, Mkuu wa Wilaya hiyo Miraji Jumanne
Mtaturu amebainisha kuwa pamoja na mafunzo kwa ajili ya ufahamu wa
majukumu ya watendaji hao lakini amesema kuwa Wilaya ya Ikungi ipo nyuma
kielimu kutokana na shule kuwa mbali na maeneo ya watu, wanafunzi wa
kike kuachishwa shule na kuolewa, baadhi ya viongozi na wataalamu
kutotimiza wajibu wao na wakati mwingine uzembe wa baadhi ya watumishi
wa serikali katika kutatua kadhia za wananchi.
Pamoja
na hayo pia DC Mtaturu amesema kuwa kuna baaadhi ya maeneo kuna shule
ambazo zina majengo mazuri na Hosteli kwa ajili ya wanafunzi lakini
wazazi wanakataa kuwapeleka wanafunzi shuleni ikiwa ni pamoja na shule
ya Sekondari Mkinya iliyopo Kata ya Dung’unyi, Shule ya Sekondari
Mtunduru, Shule ya Sekondari Mwaru na Wembere , huku shule ya Sekondari
Issuna ikiwa na Majengo na Hosteli nzuri lakini wanafunzi wanaosoma hapo
ni wale wanaotoka Wilaya nyingine huku wenyeji wakiwa wamejichimbia
ndani.
Dc
Mtaturu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
kwa kushirikiana na Polisi kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua
baadhi ya Watendaji wa Kata, Waratibu wa elimu wa Kata, Wenyeviti wa
Vijiji na Watendaji wa Vijiji wanaoshirikiana na baadhi ya wazazi
kuwaachisha wanafunzi shule ili wakaolewe ambapo amebaini kuwa katika
Kata ya Mwaru na baadhi ya Kata zinazozunguka katika Kata hiyo viongozi
wake kwa kushirikiana na Waratibu elimu Kata wamekuwa wakifanya biashara
ya kuruhusu wanafunzi kuolewa kwa kupewa Ng’ombe.
Hata
hivyo pia amewaagiza Watendaji wa Kata ya Makilawa na Iyumbu kumpatia
taarifa ya kamati ya maendeleo ya Kata (WDC) ili kubaini mpango wa
mikakati katika kujenga shule za Sekondari katika Kata hizo mbili ambazo
zimesalia ilihali Kata 28 tayari zina shule za sekondari kati ya Kata
30 zilizopo katika Wilaya hiyo.
Katika
shule 28 ni shule 3 tu zenye maabara, shule ya Sekondari ya Puma na
Wembere ambao nao walijenga maabara baada ya kupata msaada kutoka Benki
ya dunia Mwaka 2013, shule ya Sekondari Mkinya ina maabara 2 ambazo
zilijengwa kwa msaada wa SADC mwaka 2009 hivyo kupelekea Wilaya nzima ya
Ikungi kuwa na Maabara 4 pekee zilizojengwa kwa msaada wa wahisani
ambapo hakuna hata maabara moja iliyojengwa na wananchi ikakamilika
kutokana na zuio la kuchangia walilolipata wananchi kutoka kwa Mbunge wa
Jimbo la Singida Mashariki Tundu Lissu.
Sawia
na hayo pia Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza Watendaji wa Kata na Vijiji
kwa kushirikiana na Wabunge, Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji
kuwaelimisha wananchi kukaa vikao na kupitisha maadhimio ya kuendelea
kuchangisha michango ya ujenzi wa maabara kwa mujibu wa waraka wa Elimu
namba 6 wa mwaka 2015 wa elimu msingi bila malipo.
Hata
hivyo agizo limetolewa pia kwa Wazazi/Walezi pamoja na wanafunzi
wenyewe kuchukuliwa hatua kali za kisheria kutokana na utoro wa
wanafunzi shuleni jambo ambalo linapelekea kuwa na ufaulu duni wa
wanafunzi Wilayani humo.
Dc
Mtaturu pia amemuagiza Afisa Mtendaji wa Katana Afisa Mtendaji wa
Tarafa kutumia siku 14 kuhakikisha madawati yanafika katika shule zenye
uhaba wa madawati ili kuondokana na adha ambayo inaendelea kuwakumba
wanafunzi shuleni ilihali madawati tayari yamepatikana.
Aidha
ndani ya siku tano viongozi hao wameagizwa kuhakikisha kuwa Masoko
pamoja na stendi zinaenda katika maeneo yaliyopangiwa ili ushuru
upatikane kwa wakati na kwa kiasi kilichokusudiwa.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka
amewashukuru Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Watendaji wa
Vijiji kwa kujitokeza kwa wingi katika mafunzo hayo jambo ambalo
limeonyesha kuwa wananchi hao wana imani na serikali ya awamu ya nne
hivyo amewaomba kuachana na siasa na kufanya kazi kwa moyo na nguvu
zaidi.
Amewataka
viongozi wote wa ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata, Vijiji na vitongoji
kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na serikali kwa haraka na kwa
ukamilifu.
Turuka
amesema kuwa kila kiongozi anapaswa Kutatua kero za wananchi kwa
kutenda haki, kutofanya kazi kwa mazoea, kutoa majawabu sahihi ya
wananchi na kama hawafahamu wanapaswa kuuliza sehemu husika ili
kutozungumza jambo wasilokuwa na uhakika nalo.
Kupitia
kikao hicho kilichoitishwa na mkuu huyo wa Wilaya kilichokuwa na
dhumuni la kufahamiana na kukumbushana majukumu na wajibu wa viongozi na
kueleza mtazamo wa Ikungi mpya inavyotakiwa kuwa Afisa utumishi wa
Wilaya sawia na Mkuu wa Polisi Wilaya wamepewa nafasi ya kuelezea
majukumu na wajibu wa kila mmoja katika maeneo yao.
Kwa
upande wao baadhi ya Watendaji wa Kata, Vijiji na wenyeviti wa vijiji
101 vilivyopo Wilayani humo wamesema kuwa mafunzo waliyoyapata
watayatumia vyema kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi na kuwaelimisha
zaidi ili kutambua mipaka yao na majukumu yao katika kuishauri serikali.
Aidha
Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa vijiji na wenyeviti wa
vijiji wote ambao hawajahudhuria kikao hicho cha kazi wametakiwa
kuandika barua za maelezo kwanini wameshindwa kuhudhuria na zimetakiwa
kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ikungi hadi kufikia tarehe
10 ya mwezi huu wa nane.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwasilisha mtazamo wa namna ambavyo anataka Wilayahiyo iwe.
Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji
Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Evodius Buberwa akifafanua na kutofautisha majukumu ya watendaji wote ngazi ya Wilaya, Tarafa, Kata na Vijiji
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akisisitiza umuhimu wa kuchangia maabara kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi wanaotaka kusoma masomo ya sayansi lakini kikwaza inakuwa maabara
Kutoka Kushoto ni Mustafa Mtopo kaimu Afisa usalama wa Taifa Wilaya ya Ikungi, Fortunatus Ndalama Mshauri wa Mgambo Wilaya ya Ikungi, Dijovson Ntangeki Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya ikungi Rustika Turuka, na Mkuu wa poiisi Wilaya ya Ikungi Milton Nkyalu wakifatilia mafunzo kutoka kwa wawasilishaji waliotoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya ikungi Rustika Turuka aliyesimama akizungumza na Wakuu wa Idara na vitengo, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Vijiji, na Wenyeviti wa Vijiji wakati wa kikao hicho cha kazi.
Afisa utumishi wa Wilaya ya Ikungi Ahmed Mussa akiwasilisha madawakati wa mafunzo hayo.
Kaimu katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi Dijovson Ntangeki akielezea ratiba ilivyo ya mafunzo hayo.
No comments:
Post a Comment