Na Mwene Said.
Upande wa utetezi, katika rufani ya kesi inayomkabili Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanaokabiliwa na mashtaka ya kujipatia Dola za Marekani million sita, leo uliomba kuahirisha kusikilizwa rufani hiyo baada ya mawakili wawili kuwa na udhuru ikiwamo ugonjwa.
Dk. Masumbuko Lamwai alitoa maombi hayo leo mbele ya Jaji Edson Mkasimongwa aliyepangiwa kusikilizwa rufani ya kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha pamoja na maombi ya dhamana ya washtakiwa hao katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Dk. Lamwai alisema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa rufani ya Jamhuri kupinga kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha lakini Wakili Majura Magafu alikuwa na kesi nyingine katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha. Pia, alidai kuwa mwingine mwenye udhuru ni, Wakili Alex Mgongolwa ni mgonjwa ameshindwa kufika mahakamani kuendelea na kesi hiyo kwamba ni busara Mahakama ikapanga tarehe nyingine ili kusikiliza rufani pamoja na maombi ya dhamana.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Osward Tibabyekomya akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Awamu Mbaga na Theophil Mutakyawa, alidai kuwa hana pingamizi na ombi la utetezi.
Mbali na Dk. Lamwai, mawakili wengine wa utetezi ni, Dk. Ringo Tenga, Misangi Nzerahula, Godwin Nyaisa na Alex Mshumbusi.
Jaji Mkasimongwa alisema baada ya pande zote mbili kukubaliana kuahirisha kesi hiyo, Mahakama yake itasikiliza rufani pamoja na maombi ya dhamana Julai 29, mwaka huu.
Awali Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru, ilifuta shtaka la nane la kutakatisha fedha dhidi ya washtakiwa.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri ulikata rufaa kupinga uamuzi wa kuliondoa shtaka hilo kwamba haukuridhika na uamuzi uliotolewa na Hakimu Mchauru.
Hoja nyingine, Hakimu Mchauru alikosea kusema hati ya mashtaka ina dosari wakati siyo kweli.
Hoja ya tatu, upande wa Jamhuri unaeleza kwamba uliomba nafasi kwa kuwa kifungu cha 234 kidogo cha (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hakimpi hakimu madaraka ya kuruhusu kubadilisha hati kama kweli mahakama iliona ina dosari za kisheria.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wote wanasota rumande ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996 Shose Sinare na mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha Dola za Marekani milioni 6 mali ya Serikali.
No comments:
Post a Comment