HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 24, 2016

Taasisi ya Brigite Foundation yazindua Mradi wa Kisasa wa Taa za Solar Katika Kituo cha Albino cha Buhangija Shinyanga

Julai 23,2016 Taasisi ya Brigite Foundation imezindua mradi wa taa za solar katika kituo cha walemavu wa ngozi cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya kuimarisha usalama katika kituo hicho ambacho sasa kina jumla ya watoto albino 220,wasiosikia 61 na wasioona 33.

Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ambapo mbali na uzinduzi huo wa mradi wa umeme mbadala,watoto katika kituo hicho walishiriki michezo mbalimbali pamoja na kula chakula cha pamoja na viongozi wa taasisi ya Brigitte Alfred Foundation na CSI Electrical Limited.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo,Rais na Mwanzilishi wa Brigitte Alfred Foundation bi Brigitte Alfred alisema mradi huo mkubwa wa kisasa wa taa za sola utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa watoto hao katika kituo hicho.
Brigitte ambaye ni Miss Tanzania mwaka 2012 alisema baada ya kuguswa na hali iliyopo katika kituo hicho mwaka jana aliomba Kampuni ya Wakandarasi wa Umeme wa ndani -CSI Kusaidia kufunga umeme katika kituo hicho wakakubali na hatimaye leo mradi huo umezinduliwa.

“Tunaushukuru uongozi wa CSI Electrical Limited kwa namna walivyopokea maombi yetu na hatimaye kuchukua hatua za haraka kwa kutoa msaada huu pia viongozi wa serikali na chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ushirikiano wenu uliosaidia kukamilika kwa mradi huu”,alieleza Alfred.

“Mradi huu umetimiza na kuunga mkono malengo ya Millenia namba 7 inayolenga upatikanaji wa nishati salama “Affordable and clean energy”,tunatarajia mradi huu utahamasisha na kuchochea ari ya wanafunzi katika elimu ya mazingira na matumizi ya nishati mbadala na watawawezesha kusoma na kushiriki kwa vitendo katika kufikia malengo ya kitaifa na ya kidunia kama kizazi na viongozi wa kesho”,aliongeza.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba jamii kuunga mkono juhudi za serikali na kusimamia kauli mbiu ya pamoja ya kuhimiza amani,upendo na kutokomeza kabisa matukio maovu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na kuifanya Tanzania endelee kuwa mahala pazuri na salama pa kuishi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya wakandarasi wa umeme -CSI Electrical Limited Joan Kahwa alisema wamefunga Panel 13 na mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 75.88.

“CSI ilipokea ombi la taasisi ya Brigitte Alfred Foundation kwa moyo wote ili kuungana nao katika kuboresha maisha ya watoto wetu hapa Buhangija,Mkurugenzi Mtendaji wa CSI Elecrical Limited alitembelea kituo hiki mwaka 2015 ili kutafiti jinsi ya kukisaidia,katika ziara hiyo tuligundua changamoto nyingi zinazowakabili watoto pamoja na walimu na walezi waishio hapa kituoni”,alieleza Kahwa.


“Kwa awamu ya kwanza tuliona ni vyema kuboresha ulinzi wa eneo hili,kwa kudhamini ununuzi,uingizaji,usafirishaji na ufungwaji wa taa za sola shuleni hapa ili kuwe na mwanga wa kutosha nyakati za usiku”,alifafanua.

“Katika awamu ya pili tutalenga kuboresa mfumo wa maji ili upatikanaji wa maji uwe rahisi zaidi kwa kufunga pump ya sola yenye uwezo wa kutosha kwa kituo hiki,jitihada hii itasaidia kuboresha hali ya usafi katika shule hii kwa kurahisisha shughuli za usafi,kufua,kuosha vyombo,kuandaa chakula na usafi wa watoto kwa ujumla”,aliongeza Kahwa.

Naye Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro aliyezindua mradi huo aliipongeza taasisi ya Brigitte Alfred Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya wakandarasi wa umeme CSI Electrical Limited kufanikisha kumaliza changamoto ya umeme katika kituo hicho.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha baadhi ya watu wanaowinda watu wenye albinism kwamba serikali haitasita kuwachukulia hatua huku akiwataka wazazi na walezi wa watoto hao kutowatekeleza kituoni watoto hao.

Brigitte Alfred amefanikisha zoezi la kufunga umeme wa solar katika kituo cha Buhangija mwaka mmoja tu baada ya kukamilisha ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi katika kituo hicho cha Buhangija mwaka 2015 linalowezesha kuishi watoto 70 ambalo lilizinduliwa na kukabidhiwa mwaka 2015. Na Malunde1 blog










No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad