Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Akcson amekutana
na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ulioongozwa na Spika Mhe
Zuberi Ali Maulid na kuahidi kuendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina na Vyombo hivyo viwili vya
kutunga sheria.
Akizungumza na ugeni huo uliomtembelea kwa lengo la kufahamiana na kubadilishana uzoefu katika
utendaji kazi Naibu Spika amesema ili mahusiano ya Vyombo hivi viwili yaboreke zaidi kuna haja ya kuwa
na mafunzo ya pamoja ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza ambazo nyingi zinafanana.
Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson akizungumza na Ugeni kutoka Baraza la Wakilishi
Zanzibar walipomtembelea Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam. Ugeni huo uliongozwa na
Spika wa Baraza la Wakilishi Zanzibar Mhe Zubeir Ali Maulid.
Naibu Spika aliongeza pia kuwa Bunge la Jamhuri ya Muuumgano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi
Zanzibar ni Vyombo vinavyofanya kazi zinazofanana hivyo kujifunza na kubadilishana uzoefu ni jambo la
muhimu katika katika kuboresha utendaji kazi.
“Mahusiano tuliyonayo yanawekewa nguvu tunapokuwa na mafunzo yale ya pamoja kwa sababu fursa
inapatikana ya kubadilishana uzoefu lakini pia kujifunza mambo kwa pamoja kuliko kukiwa na
uendeshaji ambao ni tofauti sana wakati Vyombo hivi vinafanya kazi inayofanana,” alisema Naibu Spika
wakati akizungumza na Ugeni huo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam.
Dkt Tulia pia ametumia fursa hiyo kumpongeza Spika na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa
kuchaguliwa kushika nyadhifa hizo na kusema kuwa Bunge lipo tayari kutoa ushirikiano wakati wowote
utakapohitajika.
Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid amesema Baraza la
Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kitu kimoja hivyo wameona ni
muhimu kuja kusalimiana, kufahamiana na kuimarisha mahusiano yaliyopo ili kurahisisha utendaji kazi
wa Vyombo hivyo.
Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson akimsikiliza Spika wa Baraza la Wakilishi Zanzibar
Mhe Zubeir Ali Maulid wakati alipofanya mazungumzo naye Ofisini kwake Jijini Dar es
Salaam.
Adiha alisema kuwa Baraza la Wawakilishi litaendelea kujifunza na kuomba ushauri toka Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ili hilo lifanikiwe kuna haja ya kuboresha zaidi mahusiano ya
mihimili hiyo miwili ya kutunga sheria.
Pia Mhe. Maulid amempongeza Naibu Spika Dkt Tulia kwa umahiri wake wa kupambana na changamoto
zilizojitokeza wakati wa uendeshaji vikao vya Bunge na kusema kuwa kuna mambo mengi wamejifunza
kutoka kwake.
Pamoja na Watendaji wengine wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Spika wa Baraza hilo aliamabatana pia
na Naibu Spika wa Baraza Mhe Mgeni Hassan Juma na Katibu wa Baraza Ndg. Raya Issa Msellem.
Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson (katikati ya waliokaa) katika picha ya pamoja na
Ujumbe kutoka Baraza la Wakilishi Zanzibar wakiongozwa Spika wa Baraza la Wakilishi
Zanzibar Mhe Zubeir Ali Maulid (wa pili toka kulia).( Picha na Ofisi ya Bunge)
No comments:
Post a Comment