Wito
umetolewa kwa Taasisi,mashirika, makampuni na watu binafsi kuanzia
ngazi ya familia kuendelea kuitumia Siku ya jumamosi ya kila mwisho wa
mwezi kufanya usafi wa mazingira, kupanda miti na kutunza vyanzo vya
maji kwa hiari bila kusubiri kushurutishwa na sheria kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara na
wafanyakazi wa taasisi na mashirika mbalimbali waliokuwa
wakitekeleza wakifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es
salaam leo wamesema kuwa hatua ya Serikali kuirasimisha Siku ya
jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa siku ya usafi wa mazingira
kitaifa inaweka msisitizo kuhusu jukumu la kila mwananchi kuwa mlinzi
na mwangalizi wa mazingira katika sehemu anayoishi.
Wamesema
Suala la usafi wa mazingira linawahusu watu wote, hivyo kila mwananchi
anao wajibu wa kushiriki kikamilifu kufanya Usafi wa Mazingira kwenye
Makazi yake, Maeneo ya Biashara, maeneo ya Taasisi za Umma na maeneo
yenye mikusanyiko ya watu mbalimbali kama masoko na minada.
Bi.
Zaituni Musa mkazi wa Mwananyamala, Kinondoni jijini Dar es salaam
aliyekuwa akisafisha mifereji eneo la mtaa anaoishi akishirikiana na
wananchi wenzake amesema kuwa suala la usafi wa mazingira ni jukumu la
kila mwananchi bila kuangalia cheo au nafasi yake katika jamii kwa kuwa
kuishi katika mazingira machafu kuna athari kubwa kiafya hususan
kuchangia milipuko ya magonjwa ikiwemo Kipindupindu.
"
Suala la usafi wa mazingira linatuhusu sote, ni wakati wa kuchukua
hatua na kuacha kuishi kwa mazoea,nawaomba watanzania wenzangu tufanye
usafi bila kulazimishwa na Serikali kila mmoja atimize wajibu wake"
Amesisitiza Bi.Zaituni.
Nao
baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka eneo la Mwananyamala na wale
wa Soko la vyakula la Buguruni, Manispaa ya Ilala waliokuwa wamefunga
maduka na biashara zao kupisha muda wa kufanya usafi wa mazingira
kuanzia saa 12 hadi saa 4 asubuhi wamesema kuwa uamuzi wa Serikali
kuitangaza Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa Siku ya Usafi wa
mazingira unatoa fursa kwao Kufanya Usafi wa mazingira katika maeneo
wanayofanyia biashara tofauti na awali.
"
Watanzania wote wa Mijini na Vijijini tujenge desturi ya kuweka
mazingira yetu katika hali ya usafi wakati wote na katika jambo hili
kila mmoja wetu awe mlinzi wa kukemea watu wenye tabia za kutupa taka
hovyo ili maeneo yetu yawe katika hali ya usafi na yakuvutia wakati
wote" Amesisitiza Bw. Haule John mmoja wa wafanyabiashara hao.
Aidha,
wamesisitiza kuwa ili kuyaweka maeneo mbalimbali katika hali ya usafi
Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 lazima itumike kwa mtu yeyote
atakayekaidi kufanya usafi siku hiyo kutozwa faini isiyopungua shilingi
elfu hamsini au kifungo cha kuanzia miezi mitatu mpaka miaka saba, faini
ya shilingi laki mbili ya papo hapo na shilingi milioni tano kwa
kampuni au taasisi itakayotupa taka hovyo atatozwa.
Ikumbukwe
kuwa Desemba 23 mwaka jana, Serikali kupitia kwa Naibu Waziri, Ofisi ya
Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Luhaga Mpina ilitangaza kuwa
usafi wa mazingira nchi nzima utakuwa ukifanyika kila Jumamosi ya mwisho
wa mwezi.
Mhe.Mpina
alisema kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya viongozi na
watendaji wanaopuuzia kusimamia shughuli za usafi katika siku hiyo pia
kwa wananchi wanaoshindwa kufanya usafi katika maeneo yao kwa mujibu wa
sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake pamoja na Sheria ndogo.
Aidha,
kabla ya jumamosi ya kila mwezi kutangazwa kuwa siku ya Usafi nchini,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa
kuzingatia sheria ya Sikukuu za Kitaifa, aliamua maadhimisho ya sherehe
za Uhuru , 9 Desemba 2015 kwa upande wa Tanzania Bara yatumike kufanya
usafi wa mazingira nchi nzima na kuhamasisha watu kujituma kufanya kazi.
Wafanyabiashara na wananchi katika soko la vyakula la Buguruni, Ilala wakiendelea na shughuli zao mara baada ya kumalizika kwa muda uliotengwa wa kufanya usafi wa mazingira leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya vijana wanaofanya biashara ya kubeba abiria kwa kutumia pikipiki ( Bodaboda) wakifanya biashara katika eneo chafu, karibu na reli ya kati eneo la Tazara hali inayoonesha kuwa wamekaidi agizo la kufanya Usafi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment