Na Raymond Mushumbusi-MAELEZO
Serikali inafanya jitihada kubwa kuimarisha upatikanaji wa Huduma za Uzazi salama katika mikoa mbalimbali kwa kujenga na kukarabati vyumba vya upasuaji,majengo ya Huduam za Afya ya Mama na Mtoto na nyumba za watumishi.
Akijibu swali la Mhe.Fatuma Hassan Taufiq Mbunge wa Viti Maalum (CCM) lililouliza serikali lini itamaliza jengo la kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto lililopo katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ili kunusuru maisha ya wakina mama wakati wa uzazi,Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Hamisi Andrea Kigwangalla amesema serikali imelipa kipaumbele suala la kupunguza vifo vya akina mama na Watoto vinavyotokana na uzazi kwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika vituo vya kutolea huduma za Afya nchini.
” Kwa upande wa Hospitali ya Dodoma,Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI inakamilisha ujenzi wa Martenity Complex katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na kazi hii iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mifumo ya maji,kupaka rangi na kazi ndogo ndogo za nje ya jengo hilo na ununuzi wa samani.
“ Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto itashirikiana na na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati ili kuwezesha wananchi wa mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani kupata huduma bora za uzazi salama” Alisema Mhe.Kigwangalla.
Mhe. Hamisi Andrea Kigwangalla ameongeza kuwa Wizara yake ilifanya tathmini na kubaini mikoa ambayo ina idadi kubwa ya vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na uzazi na katika kuondoa tatizo hilo mradi wa kuharakisha kupunguza vifo vya akina mama wajawazito vinavyotokana na uzazi(Strengthening Martenity Mortality Reduction Program-SMMRP) na program hii ilielekezwa katika mikoa mbalimbali.
Ameitaja mikoa ambayo ilibaikika kuwa na idadi kubwa ya vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na uzazi kuwa ni Mtwara,Tabora na Mara na jitihada zinaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za uzazi salama katika mikoa mbalimbali kwa kujenga na kukarabati vyumba vya upasuaji,majengo ya Huduma za Afya ya mama na Mtoto na nyumba za watumishi ili kupunguza ama kuondoa kabisa tatizo hili.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ikishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kuboresha Huduma za Afya ili kuwapa wananchi unafuu wa kupata huduma hizo katika ubora unaotakiwa ikiwa pamoja kuhakikisha wananchi wanakuwa na Bima ya Afya zinazotumika katika madaraja yote ya vituo vya Afya.
No comments:
Post a Comment